Rais Dkt.Mwinyi:Nendeni mkakomeshe uzembe na ufisadi

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewata Makatibu Wakuu wapya kutekeleza majumuku yao ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuzisimamia fedha za serikali na kupamabana na uzembe na ufisadi, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Baadhi ya Makatibu Wakuu na Manaibu wateule wakipitia hati ya Kiapo kabla ya kuaza zoezi la kuapishwa kuwa Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali za SMZ, hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya Ikulu jijini Zanzibar. (Picha zote na Ikulu/Diramakini)

Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Januari 25, 2025 katika viwanja vya Ikulu jijini Zanzibar mara baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni wakiwemo Makatibu Wakuu.

Amesema kuwa, ameamua kupunguza idadi ya Manaibu Makatibu Wakuu kwa lengo la kupunguza ukumbwa wa Serikali pamoja na kupunguza matumizi ya Serikali.

Amesema kuwa, Makatibu Wakuu ndio Maafisa Masuuli ambao ndio wasimamizi wa fedha za Serikali ambapo amewataka fedha za mahuduli za Serikali zinapatikana kwani bado kuna taasisi zinakusanya kwa njia ya risiti za mkono na kutaka fedha kukusanywa kwa mtandao.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akimuapisha Ndg. Mussa Haji Ali kuwa Katibu Mkuu Afisi ya Rais Kazi,Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, wakati wa hafla hiyo iliofanyika katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar. 

Amewataka kuondoa matumizi yasiyokuwa na tija kama vile semina na makongamano pamoja na kuwataka kuondoa aina zote za ubadhirifu, matumizi nje ya bajeti kwani mifumo ya bajeti ya fedha za serikali zimekuwa zikichezewa sana.

Amesema kuwa, hali hiyo imepelekea wahasibu kadhaa kuuchezea mfumo huo na kuchukua fedha nyingi na kusema kuwa tayari ameshatoa agizo kwa wahasibu wote waliotuhumiwa kufanya mchezo huo kusimamishwa kazi kati ya wahasibu zaidi ya 80 ambao bado walikuwa Serikalini.

Ameutaka uongozi wa Wizara ya Fedha kurekebisha mfumo huo mara moja huku akiwataka Makatibu Wakuu hao kuyafanyia kazi mambo hayo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akumuapisha Ndg. Seif Shaban Mwinyi kuwa Katibu Mkuu Afisi ya Rais Katiba,Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, wakati wa hafla hiyo iliofanyika katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar.

Katika maelezo yake, Rais Dkt. Mwinyi amewataka Makatibu Wakuu hao kuondoa uzembe, uvivu, utoro na kuwataka kuchukua hatua kwa wale wasiowajibika mara moja kwani wao ndio wenye dhamana.

Amesema kuwa, Makatibu Wakuu hao ndio wenye Mamlaka na dhamana ya wafanyakazi hivyo amewataka kuhakikisha wafanyakazi wanaokwamisha kazi kutokana na urasimu wao wanafanyiwa kazi.

Rais Dkt. Mwinyi amewataka Makatibu Wakuu hao kuhakikisha nidhamu inajengwa katika maeneo yao ya kazi huku akiwataka kuhakikisha suala la haki za wafanyakazi linapewa kipaumbele zikiwemo posho zao, muda wa ziada wa kazi pamoja na fedha za likizo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi Hati ya kiapo Bi. Abeida Rashid Abdalla, kuwa Naibu Katibu Mkuu (Ustawi wa Jamii,Wazee,Jinsia na Watoto) Wizara ya Afya Ustawi wa Jamii Wazee Jinsia na Watoto Zanzibar, wakati wa hafla hiyo iliofanyika katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar, baada ya kumaliza kula kiapo.

Amewataka kuhakikisha safari za kikazi zinakuwa zenye tija na zisiwe na upendeleo kwani taasisi nyingi zipo ambazo wanakwenda wao kwa wao sambamba na nafasi za masomo ambazo wamekuwa wakienda hao kwa hao na kuwataka kutofanya hivyo kwani hali hiyo inaondoa utendaji na morari ya kazi.

Ameeleza kuwa ipo haja ya kusimamia vizuri kamati za manunuzi na kuwataka kila kinachonunuliwa kiwe na thamani ya fedha zinatolewa huku akitolea mfano wa pampu zilizonunuliwa na Mamlaka ya ZAWA ambazo zimefanya kazi kwa muda wa kati ya miaka miwili na mwaka mmoja wakati zipo ambazo zinakaa zaidi ya miaka kumi.

Amewataka kuchukua hatua na kutomsubiri yeye na kusema kwamba iwapo watashindwa wao kuchukua hatua yeye atachukua, lakini akiwamaliza atawachukulia hatua na wale viongozi wa wizarani.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akimuapisha Dkt.Omar Dadi Shajak kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya Ustawi wa Jamii Wazee Jinsia na Watoto Zanzibar,wakati wa hafla hiyo iliofanyika katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar. 

Ametoa mfano wa taa zilizowekwa na mradi wa ZUWSP awamu ya kwanza barabarani, mradi wa MRI katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, vifaa vya kupimia mizigo uwanja wa ndege kati ya 12, tisa ni vibovu,

Amesema kuwa, hatua zinapochukuliwa hazichukuliwi kwa sababu anachukiwa mtu kwa sababu anaonewa mtu kwa sababu wakati serikali inajenga na kutoa fedha wengine wanakwaza hivyo ni vyema wakati kunajengwa wengine wasiwepo.

Rais Dkt. Mwinyi ametolea mifano miradi michache ikiwemo ile ya maji ambayo haikufanywa vizuri na badala yake jukumu linawaangukia Wabunge na Wawakilishi hivyo, ametaka hayo yasifichwe yasemwe na wale waliotuhumiwa wasimamishwe kazi na hawafukuzwi kwani baada ya uchunguzi ikithibitika hawajahusika watarejeshwa kazini na iwapo wakithibitika hatua zitachukuliwa.

Amesema kuwa, manunuzi ni eneo ambalo ni lazima lifanyiwe kazi na kuwataka Makatibu hao Wakuu kuchukua hatua za haraka na kufuata taratibu za tenda.

Sambamba na hayo, ameitaka kila mamlaka iliyokuwa chini ya wizara yake ni jukumu lao kuzifanyia kazi na kuchukua hatua na kuhakikisha kuna utendaji mzuri katika Mamlaka zao na hakuna rushwa, hakuna wizi wa fedha za umma hususan katika manunuzi.

Amesema kuwa mikataba yote ni lazima iwe na maslahi kwa umma na kuwataka mikataba yote ipite kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ikiwemo ile inayohusu mikopo ambapo ni lazima ipate kibali cha Waziri wa Fedha na kuwataka kusimamia hali hiyo.

Rais Dkt. Mwinyi amewataka kusimamia miradi yote ya uchafu ukiwemo mradi wa ZUSP ambao mradi huo haukusaidia na mpaka leo mji bado haujawa msafi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimuapisha Bi. Suzan Peter Kunambi. kuwa Mkuu wa Wilaya ya Magharibi "A" Unguja , hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar.

Akieleza kuhusu taarifa za Mkaguzi wa ndani na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amewataka Makatibu Wakuu kufanya kazi na Wakaguzi wa ndani na kutafuta wakaguzi watakao wasaidia huku wakihakikisha kasoro zote zinafanyiwa kazi.

Pamoja na hayo, amesema kuwa kumekuwa na mtindo wa kuchukuliwa fedha za fidia ambazo zimekuwa zikichukuliwa na wahusika wa kulipwa fidia wamekuwa hawazipati wakiwemo wale wanaobomolewa nyumba zao kupitisha miradi ya barabara.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi na kulia kwake ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na (kushoto kwa Rais), Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdalla akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Serikali waliokaa na waliosimama nyuma Makatibu Wakuu na Manaibu katika picha ya pamoja baada ya kuwaapisha katika viwanja vya Ikulu jijini Zanzibar.

Amewataka Makatibu Wakuu hao kufanya uhakiki wa fedha za Pencheni za wazee, fedha za TASAF, fedha za ruzuku za kilimo, fedha za uwezeshaji wananchi kiuchumi na nyenginezo na kuwataka kuhakikisha hayo ni majukumu yao na wanayafuatilia vyema.

Sambamba na hayo, amewataka kutokuwa vikwazo kwa miradi ya uwekezaji huku akiitaka ZIPA kuwa ni kituo kinachukusanya wahusika wakuu wote wa uwekezaji na kutowabughudhi wawekezaji.

Amesisitiza haja kwa kila Wizara kuandaa miradi ya maendeleo na iwepo bajeti yake hivyo wote wawe tayari kuhakikisha wanatekeleza miradi ya maendeleo huku akiwaahidi kwamba atazitembelea wizara zote.

Sambamba na hayo, Rais Dkt. Mwinyi amewataka kila Katibu Mkuu kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM pamoja na kufuatilia ahadi zote zilizotolewa kwa wananchi.

Kwa upande wa Katibu Mkuu Kiongozi, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa, kumekuwa na utamaduni wa kuzorota kwa kazi zile zinazopangwa kwa Wizara zaidi ya moja kwa kawaida kazi zinakuwa haziendi hivyo alimtaka Katibu Mkuu Kiongozi kutekeleza majukumu hayo ipasavyo.

Nao Makatibu Wakuu hao walioapishwa leo wameahidi kwenda mwendo kasi wa Rais Dkt. Mwinyi na kueleza kuwa wako tayari kutekeleza majukumu yao na kubwa wanaloliomba ni ushirikiano kati yao na watendaji wengine katika sehemu zao za kazi.

Post a Comment

0 Comments