Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limewaeleza waagizaji na wauzaji wa magari kutoka nje ya nchi kuwa, kuanzia Machi Mosi, 2021 utaratibu wa kukagua magari kutoka nje ya nchi utafanyika baada ya kuwasili hapa nchini (destination inspector),anaripoti Mwandishi Diramakini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyoonwa na Mwandishi Diramakini kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa TBS, Roida Andusamile, magari yote yatakayosafirishwa kuanzia tarehe tajwa hapo juu yatakaguliwa katika Bandari ya Dar es Salaam.
"Kwa sasa TBS inakagua magari kutoka nje ya nchi kupitia mawakala watatu kutoka Japan na mmoja kutoka Dubai ambao mikataba yao itakoma hivi karibuni. Hivyo vyeti vya ukaguzi vitatolewa na mawakala tajwa kwa magari yatakayosafirishwa kuanzia Machi Mosi, 2021 havitatambuliwa na TBS,"TBS imeeleza.
Aidha, kwa mujibu wa TBS magari yatakayopimwa bandarini na kutokidhi matakwa ya kiwango yatahitaji kufanyiwa matengenezo nje ya bandari na kisha kuletwa na kupimwa tena kwenye yadi ya UDA mkabala na Bandari ya Dar es Salaam.
"Shirika litaendelea kuhakikisha kuwa, magari yote yaliyotumika na kuingizwa nchini yanakidhi matakwa ya kiwango cha magari yanayotumika,"imeongeza TBS.