CHADEMA waja kivingine, wafanya mabadiliko makubwa

Baada ya ukimya kutawala kwa muda katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),imeelezwa kwa sasa wamefanya mabadiliko makubwa katika muundo wake wa Sekretarieti ya Kamati Kuu (CC) ambayo imebeba dhamana kubwa ya kuhakikisha Uchaguzi Mkuu ujao wanafanya vizuri, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Mheshimiwa Freeman Mbowe. (Picha na Maktaba).

Hatua hiyo imefikiwa katika kikao cha siku kadhaa kilichofanyika jijini Zanzibar ambapo kwa mujibu wa mtoa taarifa kwa sharti la kutoandikwa jina lake, mabadiliko hayo yameenda sambamba na kuziunganisha baadhi ya kurugenzi ambazo zilikuwepo awali.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa hizo ndani ya chama amemueleza Mwandishi Diramakini kuwa,hatua hiyo imelenga kuleta ufanisi mkubwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

"CHADEMA ni taasisi kubwa ambayo lazima ianze kujiwekea malengo ya muda mfupi na muda mrefu, sasa hayo malengo kama taasisi imara katika kuhakikisha demokrasia inaendelea kuwa nguzo muhimu hapa nchini, imeona ifanye mabadiliko ambayo yatatuwezesha kuyafikia malengo yetu.

"Kuna baadhi ya watu au wakurugenzi ambao wamekuwa wakifanya kazi vizuri sana katika kuhakikisha chama kinasonga mbele, lakini wengine wamekuwa wababaishaji, hivyo kwa maana nyingine watu wa aina hiyo, kwa CHADEMA hii mpya ijayo sidhani kama watakuwa na nafasi,"amesema mtoa taarifa huyo kwa sharti la kutoandikwa jina lake.

Amesema, katika mkutano wao wa Zanzibar wamejiwekea mikakati mipya ambayo inatosha kusema kuwa, CHADEMA kimezaliwa upya na kipo tayari kwa maandalizi ya mchakamchaka wa kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Chini ya Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Mheshimiwa Freeman Mbowe, viongozi wakuu wa chama hicho cha upinzani nchini wakiwemo wajumbe wa Kamati Kuu inaelezwa kuwa, walipiga kambi jijini Zanzibar kwa ajili ya kuja na mikakati kabambe ya ushindi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news