MADIWANI GEITA MJI WAMSIMAMISHA KAZI MHANDISI WA UJENZI

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya mji wa Geita limemsimamisha kazi Mhandisi wa ujenzi wa Halmashauri hiyo Emmanuel Mhiliwa ili kupisha uchunguzi baada ya kutuhumiwa kupotea kwa Milioni 6 zikizotengwa kununua mafuta ili kukarabati barabara katika kata mbalimbali kwenye Halmashauri hiyo na kununua vipuli bandia(fake) kwa Milioni 4 kwa ajili ya kukarabati mitambo ya kuchonga barabara, anaripoti Robert Kalokola (Diramakini) Geita.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Geita Constantine Morandi akitangaza maazimio ya baraza la Madiwani la kumsimamisha kazi Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri hiyo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Geita Constantine Morandi amesema kuwa, maazimio hayo yamefikiwa baada ya fedha hiyo kuonekana kutumika kununua mafuta na mhandisi huyo kutoa majibu kwamba barabara zilichongwa, lakini ukweli ni kwamba hakuna barabara hata moja iliyokarabatiwa.

Morandi amesema kuwa taarifa ya Mhandisi huyo ilionyesha fedha hizo zilitumika kununulia mafuta ya kuweka kwenye mitambo ya kujenga barabara, lakini kuna kata kama sita ambazo ujenzi huo haukufanyika.

Amesema, baraza limemuagiza Mkurugenzi kuchunguza matumizi hayo ya fedha ili kupata ukweli wa matumizi hayo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango miji Salome Ndekeja ambaye pia ni Diwani wa kata ya Bulela akitoa taarifa ya kamati yake kuhusu miundombinu ya barabara.

Salome Ndekeja ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya Mipango Miji ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Bulela alisema taarifa ya Mhandisi huyo inaonyesha barabara kwenye kata hiyo zimekarabatiwa lakini hakuna hata moja iliyokarabatiwa .

Diwani Salome Ndegeja alisema taarifa hiyo ya Mhandisi ni ya uongo na haina uhalisia kwasababu hakuna mtambo wa kuchonga barabara ambao umeisha fika kwenye kata hiyo hivyo fedha hiyo imetumika kinyume na taarifa ya Mhandisi huyo.

Aidha Diwani wa Kata ya Bombambili Leonard Bugomola alisema kuwa taarifa hiyo inamchonganisha na wananchi wa kata yake kwasababu inataja kukarabatiwa baadhi ya barabara katika kata hiyo lakini siyo kweli.

Baraza la Madiwani liliazimia kwa pamoja Mhandisi huyo kusimamishwa kazi na kuagiza mkurugenzi achunguze matumizi hayo ya fedha na kutoa taarifa kwa Madiwani.

Mapema katika Baraza hilo, Mhandisi Emmanuel Mhiliwa alipotakiwa kutoa maelezo kuhusu matumizi ya fedha hizo za kununua mafuta na kukarabati barabara,aliishia kudai utaratibu wa kujadili hoja hiyo haujafuatwa na kuomba ufafanuzi zaidi kwanza

Post a Comment

0 Comments