Mbunge wa Tarime Mjini, Michael Kembaki afanya ziara ya kutembelea miradi ya elimu

Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini, Michael Kembaki (CCM), viongozi wa CCM wa wilaya hiyo, na viongozi wa halmashauri kwa pamoja wamefanya ziara ya kutembelea ujenzi wa miradi ya elimu ikiwemo ujenzi wa jengo la vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Sekondari Nkende pamoja na ujenzi wa shule shikizi ya Legoryo ambapo wameridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo ambayo imechangiwa pia na michango ya wananchi kwa kushirikiana na Mbunge huyo, anaripoti Amos Lufungulo (Diramakini) Mara.

Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini Michael Kembaki mwenye Suti akiwa katika picha ya pamoja na Wanafunzi wa Sekondari ya Nkende waliokaa, Nyuma yake Ni Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Daniely Komote.(Picha na Amos Lufungilo/ Diramakini).

Ziara hiyo imefanyika Februari 25, mwaka huu, ambapo wakiwa katika shule ya Sekondari Nkende waliweza kujionea ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa vilivyojengwa kwa nguvu ya wananchi hadi hatua ya lenta.

Pia amepokea taarifa ya ujenzi wa vyumba hivyo kutoka kwa Mwalimu Mkuu wa Sekondari hiyo, Samson Hagai ambaye amesema, wananchi walichangia zaidi ya Shilingi Milioni 9 na fedha zilizotumika hadi kufikia hatua hiyo ni Shilingi Milioni 7, huku kiasi kilichosalia kimewezesha ukarabati wa madawati.

Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini, Michael Kembaki kulia akipokea taarifa ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa kutoka kwa mkuu wa Shule ya Sekondari Nkende, Samson Hagai alipofanya ziara shuleni hapo akiwa ameambatana na viongozi wa CCM Wilaya ya Tarime na viongozi wa halmashauri hiyo Februari 25, mwaka huu. (Picha na Amos Lufungilo/ Diramakini).

Mwalimu Hagai amesema kuwa, hatua ya kujenga vyumba hivyo ilitokana na idadi kubwa ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza wapatao 277.

Ambapo upungufu ukiwa ni vyumba viwili huku vyumba vitatu akisema kwa sasa vinatumika kama ofisi za walimu na Maktaba hivyo kusababisha msongamano mkubwa wa wanafunzi darasani wakati wa masomo.

"Tulikubaliana na wazazi wa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza kuchangia Elfu 60, 000 kila mmoja kwa ajili ya madarasa pekee, na pia Shilingi 15, 000. kwa ajili ya kukarabati madawati kwa sababu mzazi kuchangia dawati ni kazi kutokana na gharama. Tulikusanya zaidi ya Shilingi milioni 9 na Shilingi Mil.7 zimewezesha kufikia hatua ya lenta, wazazi waliotoa michango hiyo mpaka sasa ni 77. Naomba ikiwezekana Mheshimiwa Mbunge utusaidie kuezeka vyumba hivi. amesema Mwal.Hagai.

Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini Michael Kembaki akizungumza na Wananchi wa Kitongoji Cha Magena Senta wakati wa ziara yake iliyofanyika Februari 25, 2021 kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Tarime Mji Daniely Komote na Kulia kwake ni Katibu wa CCM Tarime Hamis Mkaruka. (Picha na Amos Lufungilo/ Diramakini).

"Changamoto nyingine inayoikabili shule ya Sekondari Nkende yenye wanafunzi 880 ni pamoja na umeme kukatika katika mara kwa mara, ukosefu wa huduma ya maji safi na salama kwa ajili ya kuwezesha wanafunzi kufanya usafi wa vyoo na matumizi mengine, haya yakipatiwa ufumbuzi yatasaidia sana kuimarisha ufaulu wa wanafunzi katika masomo yao,"amesema Mwalimu Hagai.

Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini, Michael Kembaki amemuomba Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Daniely Komote ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nkende kufanya haraka kuezeka vyumba hivyo ili kuondoa msongamano wa wanafunzi darasani, huku akibainisha kuwa, huduma ya maji shuleni hapo atahakikisha inapatiwa ufumbuzi mapema kusudi wanafunzi waondokane na tatizo hilo.

Aidha, Mheshimiwa Kembaki akiwa na timu ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi wa wilaya hiyo, viongozi wa Serikali katika shule shikizi ya Legoryo ambayo Kembaki amewezesha kuezeka vyumba vitano na ofisi moja na kuikabidhi ambapo kwa sasa hatua inayoendelea ni kujenga matundu ya vyoo 8 kusudi wanafunzi waanze kusoma karibu na maeneo wanayoishi tofauti na hapo awali walikuwa wakitembea umbali mrefu.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Tarime Mji, Daniely Komote pia ameweza kuchangia milango mitano ya vyumba vya madarasa katika shule hiyo kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Mbunge, ambapo pia alisema amejipanga vyema kwa kushirikiana na madiwani kufanya kazi kwa bidii kuwatumikia wananchi ikiwemo kuimarisha miundombinu, sekta ya afya pamoja kutatua kero za wananchi waliowachagua kuwatumikia.

Naye Mratibu wa Elimu Kata ya Nkende, Juma Majengo amesema kuwa wamekwishafanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo pamoja na Afisa Elimu wa Wilaya ambapo baada ya kukamilika ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule ya Legoryo, itasajiliwa kuwa Shule ya Msingi kutokana na kuwa na majengo mengi yaliyojengwa chini ya juhudi kubwa za Mbunge Michael Kembaki na wadau mbalimbali wa elimu jimboni humo.

Mh. Kembaki akizungumza katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kitongoji cha 'magena Senta' kata ya Nkende ambapo alisikiliza changamoto mbalimbali za wananchi hususan kero ya wananchi kutounganishiwa umeme kwa wakati licha ya kulipia fedha,Kembaki alisema suala hilo atalifikisha ngazi za juu haraka iwezekanavyo, huku akisisitiza kuwa Wananchi kutounganishiwa huduma hiyo kwa haraka halifai hata kidogo kwani linarudisha nyuma juhudi za serikali za kila Nyumba kuwa na umeme.

Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini Michael Kembaki (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wanafunzi wa Sekondari ya Nkende alipofanya ziara shuleni hapo akiwa na Viongozi wa CCM Wilaya ya Tarime. Kushoto kwake ni Mkuu wa Shule hiyo Meal Samson Hagai na Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Tarime Mji,Daniely Komote.(Picha na Amos Lufungilo/ Diramakini).

Katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Tarime, Hamis Mkaruka amesema kuwa , anapongeza kazi kubwa za maendeelo zinayofanywa na Mbunge wa jimbo hilo Michael Kembaki katika kuwajibika kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa ufanisi, ambapo pia amewaomba watumishi wa Serikali wilayani humo kufanya kazi kwa bidii na kutatua changamoto za wananchi kwa wakati kama ilivyodhamira ya Rais Dkt.John Magufuli kuona Watanzania wakiondokana na umasikini.

Rebeka Daniel na Eveline Marwa wakazi wa Legoryo kata ya Nkende wakizungumza kwa nyakati tofauti walipongeza juhudi zinazofanywa na Mbunge wao Michael Kembaki hususan katika kujitolea kuchangia Miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo elimu na afya, na hivyo kuyagusa maisha ya wananchi waliomchagua awatumikie.

Post a Comment

0 Comments