Rais Dkt. Mwinyi aipongeza TAKUKURU kwa ushirikiano mkubwa kwa ZAECA

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amepongeza ushirikiano mkubwa unaotolewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) kwa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA), anaripoti Mwandishi Diramakini (Zanzibar).

Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU), Brigedia Jenerali John Mbungo akiwa amefuatana na ujumbe wake.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi alisisitiza haja ya kuendelezwa kwa ushirikiano huo hasa ikizingatiwa kwamba (TAKUKURU) ni taasisi ya siku nyingi na ina uzoefu mkubwa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Husssein Ali Mwinyi akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Brigedia Jenerali John Mbungo (kushoto kwa Rais) akiwa na Ujumbe wake alipofika Ikulu kwa mazungumzo na kujitambulisha na (kulia kwa Rais) Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said, mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.(Pichana Ikulu).

Alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina azma ya kuijengea uwezo hivyo, katika masuala ya uchunguzi, mafunzo na shughuli zote zinazofanywa na (TAKUKURU) basi watajifunza kutoka taasisi hiyo.

“Tunashukuru kwa milango yenu kuwa wazi na tutaomba kuendelea kwa sababu tunataka kukifanya chombo hichi kuwa imara zaidi na hatuna sehemu nyengine ya kupata uzoefu kama si TAKUKURU,"amesisitiza Rais Dkt. Mwinyi.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi alieleza haja ya kuwa na muundo kama ule wa (TAKUKURU) ikiwa ni pamoja na kushuka katika ngazi za Mikoa na Wilaya licha ya hali hiyo kuhitaji uwezo mkubwa lakini ni vyema wakaanza ili kazi wanazozifanya ziwe rahisi zaidi badala ya kutegemea ngazi za makao makuu pekee.

Amesema kuwa ni vyema (ZAECA) ikajifunza kutoka Taasisi ya (TAKUKURU) kutokana na mambo mbali mbali ya kuiendesha Taasisi hiyo.

Ametoa shukurani kwa Taasisi ya TAKUKURU kwa kuonesha utayari wao wa kuwasaidisa ZAECA, na kusisitiza kwamba katika wakati huu uliopo taasisi hiyo ina umuhimu wa pekee kwani uzoefu unaonesha duniani kwamba katika kuhakikisha rushwa inadhibitiwa ni lazima kuwepo kwa chombo cha kusimamia uadilifu.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Brigedia Jenerali John Mbungo (kushoto kwa Rais) akiwa na ujumbe wake walipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha na (kulia kwa Rais) Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said, mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar. (Picha na Ikulu).
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akikabidhiwa Kitabu cha Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa na Mpango wa Utekelezaji wa Awamu ya Tatu 2017/2022 akikabidhiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Brigedia Jenerali John Mbungo, baada ya kumaliza mazungumzo yao alipofika Ikulu kujitambulisha hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Brigedia Jenerali John Mbungo, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha akiongozana na Ujumbe wake na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa ZAECA Bw. Makame Kh. Hassan (kushoto kwake) mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.(Picha na Ikulu).
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Brigedia Jenerali John Mbungo, baada ya kumaliza mazungumzo yao alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha leo 25-2-2021.(Picha na Ikulu).
 
Nae Brigedia Jenerali John Mbungo, Mkurugenzi Mkuu wa (TAKUKURU) huyo aliyeteuliwa mwaka jana Mei 2020, ambaye mwanzo alikuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu amesema kuwa, ujio wake ni kwa ajili ya kujitambulisha pamoja na kuwatembelea washirika wenzao (ZAECA).

Amesema kuwa, TAKUKURU imekuwa ikishirikiana vyema na (ZAECA) katika mambo mali mbali ikiwa ni pamoja na kushirikiana katika mafunzo ya weledi hasa ikizingatiwa kwamba (TAKUKURU) ina uzoefu mkubwa kutokana na kutangulia kuanzishwa kwani Taasisi hiyo imeanzishwa mwaka 1975 ambapo (ZAECA) imeanzishwa mwaka 2013.

Amesema kwamba, TAKUKURU ni Taasisi ya kwanza kuanzishwa katika bara la Afrika, hivyo ina uzoefu mkubwa katika kuendesha shughuli zake.

Pamoja na hayo, Bregedia Jenerali Mbugo alisema kuwa Taasisi hizo mbili zimekuwa zikishiriki vyema katika vikao mbali mbali vya Kimataifa kwa pamoja na kuangalia vipi Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaweza kunufaika na vikao hivyo.

Amesema kuwa, wamekuwa wakikaa pamoja na kujadili mambo kadhaa kuhusu vikao hivyo ambapo pia, kwa vile wote ni wanachama wa Mkataba Mkuu wa Kimataifa wa Mapambano dhidi ya Rushwa, hivyo wamekuwa wakihudhuria pamoja vikao hivyo na kuangalia vipi nchi inaweza kunufaika sambamba na kuhudhuria vikao vya Afrika Mashariki ambapo pia ina sehemu ya masuala ya rushwa.

Aidha, alieleza namna wanavyoshiriki pamoja vikao vya nchi za Kusini mwa Afrika ambavyo hukaa pamoja mara baada ya kumaliza vikao hivyo na kujadili kwa pamoja namna ya utekelezaji wa masuala hayo.

Wakati huo huo, Rais Dkt. Mwinyi alikutana na uongozi wa Jumuiya ya Wazee Zanzibar (JUWAZA) katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar na kuipongeza Jumuiya hiyo kwa ushirikiano wanaotoa kwa Serikali.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa, jumuiya hizo zinahitajika kutokana na umhimu wake mkubwa ikiwa ni pamoja na kutoa msaada wake kwa Serikali kwani si mambo yote Serikali inaweza kuyafanya.

Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Jumuiya hizo kwa azma ya kuhakikisha wazee nao wananufaika.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza mafanikio makubwa yatakayopatikana kutokana na vitambulisho vinavyotolewa kwa ajili ya wazee.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi kwa Naibu Katibu Mkuu Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Abeida Rashid Abdallah kwa ushirikiano wake mzuri anaouonesha kwa Jumuiya hizo na kumtaka kuendelea.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news