Watanzania washauriwa kutembelea vivutio vya ndani vya utalii

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Mhe. Mary Masanja amesisitiza kuwa fursa zilizoko kwenye Sekta ya Maliasili na Utalii zikitumika ipasavyo zitasaidia kukuza Pato la Taifa na uchumi wa mtu mmoja mmoja, anaripoti John Bera (WMU) Mwanza.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii na Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Mwanza, Mhe. Mary Masanja (kushoto) akiteta jambo na Kaimu Mwenyekiti wa Kikao cha Pili cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Mwanza ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Bw. Emmanuel Kipole wakati wa Kikao cha Bodi hiyo kilichofanyika jijini Mwanza.

Mhe.Masanja ametoa kauli hiyo leo jijini Mwanza wakati wa kikao cha pili cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Mwanza kwa Mwaka 2020/2021.

Amesema, takwimu za watalii wanaoingia hapa nchini kuanzia mwaka 1993 walikuwa 230,000.

Aidha, mwaka 2019 idadi hiyo ya watalii iliongezeka na kufikia milioni 1.5.

‘’Idadi ya Watanzania kwa sasa ni milioni 60, lakini ukingalia takwimu hizo watalii wanaoingia kwenye hifadhi zetu kuangalia vivutio ni milioni 1.5, hii inaonesha sisi Watanzania tuna kazi kubwa ya kufanya, kuwa wazalendo na kupenda vile tulivyo navyo,”amesema Masanja. 

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza, Mhe. Mary Masanja (Wapili Kulia) akipitia baadhi ya Nyaraka za Kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Mwanza akiwa pamoja na viongozi Mbalimbali wa mkoa wa Mwanza wakati wa Kikao cha Pili cha Bodi ya barabara ya Mkoa huo kwa mwaka 2020/2021 Jijini Mwanza.

Katika hatua nyingine, Mary Masanja amewaeleza viongozi wa mkoa huo kuwa uwepo wa vivutio vingi vya utalii katika Kanda ya Ziwa ni fursa pekee ya wananchi kuendelea kunufaika akitoa wito kwa viongozi waliohudhuria mkutano huo wahamasishe utalii wa ndani kwa nguvu zote.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Mwanza , Mhe. Mary Masanja (katikati) akizungumza na Viongozi wa Bodi ya Barabara ya Mkoa leo jijini Mwanza. Pamoja na mambo mengine amewataka viongozi hao watembelee Vivutio vya Utalii vilivyopo katika maeneo yao na kushiriki pia kuhamasisha Utalii wa ndani ili kuongeza Pato la Taifa.

“Ni lazima tuongeze nguvu katika kuhamasisha utalii wa ndani bila kusahau kuhamasisha wageni kutoka nje ya nchi yetu , Utalii wa ndani unatuhusu sisi wenyewe ,nikiuliza hapa wangapi wamefika kwenye hifadhi zetu na kwenye vivutio mbalimbali tulivyonavyo tutabaini idadi kidogo sana, nawaomba sana tuhamasishane,”amesisitiza Masanja.

Ameongeza kuwa, janga la Corona limesababisha kuyumba kwa sekta Utalii duniani kote pia hapa nchini kwa kuwa watalii waliokua wakitegemewa nchi zao zimeathiriwa na Corona hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kuwa Balozi wa kutangaza Utalii na kutembelea vivutio vilivyopo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news