Waziri Bashungwa afunga Wiki ya Mashujaa wa Majimaji

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa amefunga Wiki ya Mashujaa wa Majimaji Februali 27, 2021 Mjini Songea Mkoa wa Ruvuma ambapo aliongozana na Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt. Damas Ndumbaro, pamoja na Chifu wa Wangoni Emmanuel Zulu Gamma, anaripoti Mwandishi Diramakini (Ruvuma). Katika kilele cha Wiki ya Majimaji na kumbukumbu ya mashujaa hao 61 mmoja wapo akiwa ni Mwanamke Bi Mkomanile shujaa wa vita vya Majimaji, Mhe. Waziri Bashungwa ametilia mkazo somo la Historia kufundishwa katika shule za msingi na sekondari na kusisitiza kutunza maeneo yote ya kumbukumbu za kihistoria katika nchi yetu iliyotoa mchango mkubwa sana katika Ukombozi wa Bara la Afrika.

Katika hotuba yake aliyomwakilisha Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Mhe. Bashungwa ametumia nafasi hiyo kuwashukuru wananchi wa Ruvuma kwa kuwa mstari wa mbele katika kutunza na kuhifadhi kumbukumbu hiyo kubwa ya historia ya nchi yetu maana mkoa huu ulikuwa kama adhimu kwa wapigania uhuru wa Msumbiji.

Pia namshukuru Mhe. Rais kwa kurudisha somo la Historia kwenye shule zote nchini na pia ameupongeza uongozi wa manispaa ya Songea kwa kuanza kutekeleza kwa vitendo kufundisha somo la Historia kama ilivyoagizwa. “Serikali inafanya jitihada ya kufungamanisha utalii na Utamaduni wetu".Pia Mhe. Waziri Bashungwa ameendelea kupongeza Serikali kwa kuendelea kupigia chapuo lugha ya Kiswahili kama Mhe. Rais Dkt. Magufuli alivyoagiza na kutekeleza kwa kuhamasisha hukumu za kesi mbalimbali nchini ziwe zinasomwa kwa Kiswahili mahakamani ili kulinda haki za watu wengi zaidi.

Kutokana na maelekezo ya Mhe. Rais, "naipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Programu ya Urithi wa Ukombozi na wadau wengine, kwa kuandaa rasimu ya mihtasari ya somo la historia ya kufundishia ngazi mbalimbali za elimu na kwa sasa vinaandaliwa vitabu vyake.

"Naendelea kutoa wito kwa vijana kuwa wazalendo na kutumia nguvu zao katika kulinda nchi yetu na kujiletea maendeleo. Pia, naomba kuwashukuru wananchi wote na vikundi mbalimbali vya burudani na machifu wetu kwa kujitokeza leo katika kuwaenzi mashujaa wetu wa vita vya majimaji,"amesema.
"Natambua kuwa Mkoa wa Ruvuma umeongeza Kumbukumbu nyingine ambayo ni Makumbusho ya Dkt. Hayati Rashid Mfaume Kawawa; “Simba wa Vita” ambaye ni miongoni mwa mashujaa wa nchi yetu. Hatua hii hakika inahitaji pongezi kwa uongozi wa Mkoa kwa kuhakikisha kumbukizi hizi zinahifadhiwa ili kujenga uzalendo na kuleta utaifa kwa kizazi kilichopo na kijacho. Kwa mantiki hiyo, Mkoa wa Ruvuma kwa sasa una makumbusho mbili ambazo ni Makumbusho ya Maji Maji na Makumbusho ya Dkt. Hayati Rashid Mfaume Kawawa.

Pamoja na makumbusho haya, Mkoa huu ndio kitovu cha kusaidia wana harakati wa ukombozi wa Afrika hususani nchi jirani ya Msumbiji. Najisifu kusema Mkoa huu ulikuwa kama Maka au Jerusalemu ya Chama cha FRELIMO cha Msumbiji,"amefafanua Waziri Bashungwa.

Post a Comment

0 Comments