Waziri Mkuu akabidhi vifaa mbalimbali kwa vikundi vya wajasiriamali

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekabidhi vifaa mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 357 kwa vikundi vitano vya wajasiriamali vilivyotolewa kwa mkopo na Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa ikiwa ni asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri, anaripoti Mwandishi Diramakini (Ruangwa).

Pia, Waziri Mkuu amepokea msaada wa madawati 100 yenye thamani ya shilingi milioni 10 kutoka katika Kampuni ya vinywaji baridi ya Cocacola Kwanza ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha sekta ya elimu nchini.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akipokea madawati Mia Moja kutoka kwa Mkurugenzi wa Mahusiano na Mawasiliano ya Jamii wa Kampuni ya Cocacola, Salum Nassor, katika uwanja wa Likangala mjini Ruangwa. Februari 27, 2021.

Waziri Mkuu amekabidhi vifaa hivyo Februari 27, 2021 katika viwanja vya shule ya msingi Likangara wilayani Ruangwa na kuwataka wanufaika wa mikopo hiyo wakaitumie kama ilivyokusudiwa na wahakikishe wanarejesha kwa wakati.

Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kwa kuamua kutoa mikopo ya vifaa mbalimbali kwa wajasiriamali na pia ameitaka ihakikishe inawasimamia vizuri wanufaika hao.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikata utepe ikiwa ni ishara ya kukabidhi vifaa kwa vikundi vya vijana na uzinduzi wa miradi wanayokwenda kutekeleza baada ya mikopo waliyopewa, katika uwanja wa Likangala mjini Ruangwa. Februari 27, 2021.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Frank Chonya amesema halmashauri yao imeendelea kutenga na kutoa mikopo kwa vikundi vya ujasiriamali vya wanawake, vijana na wenye ulemavu kupitia asilimia 10 ya makusanyo ya mapato ya ndani.

Mkurugenzi huyo amesema kwa mwaka 2020/2021 halmashauri ya wilaya ya Ruangwa imetoa mikopo mikubwa yenye thamani ya shilingi milioni 357 ambazo wanavikundi wamenunua vifaa kwa ajili ya shughuli zao na wengine wameanzisha biashara ndogondogo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akimakabidhi ufunguo wa lori kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Vijana Jafar Chimulika, ikiwa ni sehemu ya mkopo uliotolewa na Halmashauri ya Ruangwa kwa kikundi hicho, katika uwanja wa Likangala mjini Ruangwa. Februari 27, 2021.

Amesema halmashauri ilifanya utafiti na kuunda vikundi vitano vya kimkakati ambavyo vimepewa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 319,910,000. ”Vikundi viwili vyenye wanufaika 20 ambavyo vinavyojishughulisha na ufugaji wa kuku vimepewa mkopo wa shilingi 13,010,000 na wamenunua kuku 2,000 aina ya chotara.”

”Kikundi kingine ni cha vijana 39 wanaofyatua matofali ambacho tumekipa mkopo wa shilingi milioni 186, ambapo wameweza kununua lori la tani nane la kusombea mchanga na kubebea tofali, mtambo wa kufyatulia tofali, mifuko ya saruji 600 na fedha zingine ni kwa ajili ya shughuli za uendeshaji.”
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akimkabidhi ufunguo wa trekta kwa Abuu Muunguja ikiwa ni mkopo uliotolewa na Halmashauri ya Ruangwa kwa Jukwa la wanawake, , katika uwanja wa Likangala mjini Ruangwa. Februari 27, 2021.

Amesema kuwa kikundi kingine kilichonufaika na mkopo huo ni Jukwaa la Wanawake Ruangwa lenye wanufaika 37 ambalo linajishughulisha na usafi wa mazingira lililopewa mkopo wa shilingi milioni 72.5 ambazo wamezitumia kwa kununua trekta na tela lake na vifaa vya kufanyia usafi. Kikundi hicho kinafanya usafi kwenye mji wa Ruangwa.

Mkurugenzi huyo amesema kikundi kingine kilichonufaika na mkopo huo ni cha vijana 10 wanaojishughulisha na uendeshaji wa bodaboda na bajaji ambao wamepewa mkopo wa shilingi milioni 48.4 na wameweza kununua bajaji tano na pikipiki nne.
Waziri Mkuu Kassim Majalaiwa, akizungumza na wananchi na vikundi 20 vya vijana na wanawake katika uwanja wa Likangala mara baada ya kupokea madawati na kuvikabidhi vikundi hivyo mikopo ya vifaa. Februari 27, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Baada ya kupokea vifaa hivyo wanufaika hao waliishukuru Serikali kupitia ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ruangwa kwa kuamua kuwakopesha vifaa kwa kuwa vitawezesha kuboresha shughuli zao za ujasiriamali na kwamba watahakikisha wanarejesha fedha hizo kwa wakati ili wananchi wengine waweze kunufaika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mahusiano na Mawasiliano kwa Umma wa Kampuni ya vinywaji baridi ya Cocacola Kwanza, Salum Nassor amesema kampuni yao imekabidhi madawati 100 yenye thamani ya shilingi milioni 10.

Nassor amesema wametoa msaada huo ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha elimu nchini, hivyo wamewaomba wadau wengine wa maendeleo wajitokeze na kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha shule zinakuwa na madawati ya kutosha.

Post a Comment

0 Comments