Marais 10, wawakilishi 50 kuuaga mwili wa Hayati Dkt.Magufuli jijini Dodoma kesho

Dkt.Hassan Abbas ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo amesema, viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa wanatarajiwa kuhudhuria kwenye mazishi ya Kitaifa ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Joseph Magufuli yanayofanyika kesho Machi 22, 2021 jijini Dodoma,anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Dodoma).
Katibu Mkuu huyo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali ameyasema hayo leo Machi 21, 2021 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Jamhuri ambapo shughuli hiyo ya mazishi itafanyika.

Dkt.Abbas amesema, viongozi hao watapata fursa ya kuaga mwili wa Hayati Dkt.Magufuli na baada ya hapo wananchi pia watapata fursa hiyo.

Amesema, pamoja na marais na wakuu hao wa nchi 10 ambao wamethibitisha kuwepo Dodoma kesho pia wawakilishi kutoka asasi za kikanda na mabalozi zaidi ya 50 wamethibitisha kuwepo katika shughuli hiyo ya maziko ya kitaifa.

Rais wa Rwanda amemtuma Mwakilishi wake ambaye ni Waziri Mkuu wake, Rais wa Angola amemtuma Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi hiyo kumwakilisha wakati Rais wa Burundi amemtuma Makamu wake wa Rais kumuwakilisha. 

"Mwili wa mpendwa wetu Hayati Dkt. Magufuli utawasili jioni ya leo hapa Dodoma na utaelekea Ikulu Chamwino ambapo wananchi wa jiji la Dodoma mnaombwa kujitokeza barabarani wakati mwili ukipita ili tumpe heshima kiongozi wetu. Mara baada ya kuwasili mwili huo utaelekea Ikulu ya Chamwino kwa kupitia barabara za Chako ni chako, Barabara ya Nyerere, Round about ya Mkuu wa Mkoa, Bunge, Morena, Bwigiri- Chamwino-Ikulu, wanachi wote wa maeneo haya wanaombwa kujipanga kwenye barabara hizo kutoa heshima zao,”amesema Dkt.Abbas.

Dkt.Abbas amesema, watakaoshiriki ni Rais wa Kenya, Rais wa Malawi, Rais wa Comoro, Rais wa Msumbiji, Rais wa Zimbabwe, Rais wa Zambia, Rais wa Namibia, Rais wa Botswana, Rais wa Afrika Kusini na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news