BALOZI WA MAREKANI AFANYA MAZUNGUMZO NA WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA PAMOJA NA WAZIRI WA UWEKEZAJI

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb) kwa kushirikiana na waziri ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji Mhe. Geoffrey Mwambe (Mb) wamekutana na kufanya mazungumzo na balozi wa Marekani nchini Tanzania Mhe. Donald J. Wright.
Katika kikao hicho Prof. Mkumbo amesema kuwa anaishukuru serikali na wananchi wa Marekani kwa kutufariji hasa katika kipindi cha kuondokewa na Aliyekuwa rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John P. Magufuli. Wananchi wa Tanzania wamefarijika sana kwa ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Marekani hivyo kikao hiko ni muhimu katika kuendeleza mahusiano yaliyokuwepo katika sekta ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Mhe. Prof. Mkumbo ameongeza kwa kusema kuwa lengo la nchi yetu ni kuongeza nguvu ya uhusiano kati ya Tanzania na Marekani na pia kuvutia wawekezaji kutoka nchi mbalimbali ili kuleta ajira kwa wananchi na kodi kwa serikali.

“Kama wizara itaendelea kutengeneza sera na sheria wezeshi ili kuvutia wawekezaji kwa wingi hasa katika uanzishwaji wa viwanda vinavyochakata mazao ya kilimo ili kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje, tumegundua kuwa kuna fursa ya kutosha katika soko la AGOA hasa kuchakata mazao yetu ndani na kusafirisha bidhaa tukauze katika soko hili, ameongeza kuwa Sewrikali ya marekani imetuhakikishia masoko ya uhakika hasa katika mazao ya kilimo hivyo ni jukumu letu kutumia soko hilo, Tanzania tunajivuania mahusiano mazuri kati yetu na nchi ya marekani hasa katika kudumisha uhusiano na ushirikiano uliokuwepo” Amesema Mkumbo.

Naye Waziri wa Uwekezaji Mhe. Geoffrey Mwambe (Mb) amesema kuwa anaipongeza sana serikali ya marekani kwa ushirikiano na uhusiano mzuri uliopo na unaoendelea kuwepo kwani marekani imeshiriki katika miradi mbalimbali hivyo jukumu la Wizara ya uwekezaji ni kuweka mazingira wezeshi kurahisisha ufanyaji biashara nchini.

Serikali inaendelea na ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwemo Afya, Elimu, miundombinu ya barabara, Umeme, maji nk ili kuendelea kuvutia wawekezaji nchini kuja Tanzania kwani tuna mazingira bora ya uwekezaji katika sekta mbalimbali.
Tunajipanga kuongeza uzalishaji wa bidha zetu ili tuuze katika soko la AGOA kwani kuna soko la uhakika ambalo tukilitumia vizuri tutaongeza uzalishaji wa bidhaa nchini ambayo itapelekea kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Naye balozi wa marekani nchini Tanzania Mhe. Donald J. Wright amefurahishwa sana na ushirikiano wa kudumu wa Zaidi ya miaka 70 uliopo kati ya Tanzania na Marekani na kuahidi kuwa Serikali ya Marekani itashirikiana kwa dhati na kwa karibu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha wawekezaji kutoka marekani wanakuja kuwekeza nchini Tanzania kwani nchi hii ina fursa nyingi za uwekezaji pamoja na hali nzuri ya ulinzi na usalama.

Balozi Mhe. Wright amesema kuwa Marekani imetengeneza historoa kubwa katika kusaidia maendeleo ya Tanzania katika miradi ya kupambana na magonjwa, Ulinzi, elimu, miundombinu n.k ambapo hiyo imepelekea uhusiano kati ya Marekani na Tanzania kuimarika zaidi.

Katika hatua nyingine Waziri wa wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb) na waziri ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji Mhe. Geoffrey Mwambe (Mb) wamefanya makabidhiano ya ofisi pamoja na nyaraka.

Katika kikao hicho cha makabidhiano ya ofisi Mawaziri wote wawili wamehaidi kushirikiana kwa dhati kwani wizara hizi mbili zinategemeana kwa kiasi kikubwa katika kufikia adhima ya uchumi wa Viwanda katika kukuza biashara na kuongeza ajira kwa wananchi.

Mhe. Prof. Mkumbo awali alikuwa waziri wa Uwekezaji na sasa ni waziri wa Viwanda na Biashara na Mhe. Mwambe alikuwa waziri wa Viwanda na Biashara na sasa ni Waziri wa Uwekezaji.

Makabidhiano pamoja na kikao na balozi wa Marekani yameshuhudiwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb), Naibu waziri Uwekezaji Mhe. William Olenasha (Mb), Katibu Mkuu Ofisi ya waziri mkuu Uwekezaji Prof. Godius Kahyarara na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Twalib Abdalah.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news