Mshumaa wa matumaini wawashwa Rwanda kumbukumbu ya mauaji ya kimbari

Jamhuri ya Rwanda imeanza wiki ya kumbukumbu ya maombolezo ya mauaji ya kimbari yaliyotokea katika nchi hiyo miaka 27 iliyopita.

Huu ni mwaka wa pili sasa kumbukumbu za mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi wa Rwanda zikifanyika katika hali isiyo ya kawaida kutokana na kuwepo kwa janga la corona.

Rais Paul Kagame wa Rwanda akiwasham mshumaa wa matumaini. (Picha na Reuters).
Zoezi lilianza jana ambapo Rais wa Rwanda, Paul Kagame aliwaasha mshumaa wa matumaini ambapo utawaka kwa siku 100 sawa na muda ambao yalidumu mauaji hayo.

Rais Kagame alisema, hakuna wakati hata mmoja ambao nchi yake imeweza kuwa pamoja zaidi ya wakati huu, lakini akasema mafanikio hayo bado yanakumbwa na changamoto kutoka kwa baadhi ya nchi za nje.

"Baadhi ya hawa watu pale walipo wakijaribu kuandaa masomo kwetu sisi, kuhusu jinsi demokrasia inavyoendeshwa na haki za binadamu. Lakini wakati huo huo unakuja wao hao hao wakiwakumbatia wale waliofanya mauaji haya tunayo yakumbuka hii leo. Wanawalinda,wanawasemea na kuwasaidia huku wakisema hawa ndiyo watu wanaotaka kuibadili Rwanda,"alisema Kagame.

Kumbukumbu za mauaji hayo zimefanyika huku kukiwepo na itikadi za mauaji hayo zinazoendelea kusikika huku na kule ulimwenguni kutoka kwa wale wanaotajwa kama wapinzani wa Serikali ya Rwanda lakini ambao serikali inashikilia walihusika kwenye mauaji hayo. Rais akiwazungumzia hao pia na kwa kutumia lugha ya mafumbo amesema

"Yaani ni jambo la kuvutia unapowaona mataifa hayohayo yakiwakamata watu hao kwa makosa kwa mfano ya ubakaji au wizi wa pesa waliofanya katika nchi hizo zilizowakumbatia na wanapofikishwa mahakamani bado utazisikia sauti zinazosema, imesababishwa na maagenti wa Kagame, hivi ni kwa jinsi gani unaweza kwenda kwenye nchi ya kigeni na kumlazimisha mtu kulifanya kosa la ubakaji au kosa la wizi? Lakini unakuta haya yote tunakuwa tumeyasema mapema bila kusikilizwa kwa sababu za kimaslahi,"alisema.

Rais Paul Kagame alisema, ukweli kwamba bado kuna miili ya waathirika wa mauaji inayoendelea kuokotwa hapa na pale miaka 27 iliyopita ni ishara nyingine, huku akisema serikali yake na wananchi kwa ujumla hawatakubali kufumba macho wakati waliofanya hayo wakiendelea kubeza kutokea kwa mauaji hayo.

Awali ilizoeleka watu kukusanyika katika maeneo mbalimbali, lakini safari hii hilo halikuwepo kutokana na kupambana na maambukizi ya virusi vya corona. 

Rais Kagame alisema, kwamba hali hii imesababisha machungu zaidi kwa manusura lakini akawapa matumaini kwamba huenda ikaisha.

Rwanda inaendelea kutoa chanjo ya corona kwa wananchi wote hali ambayo kwa kiasi fulani imeleta matumaini miongoni mwa wananchi.Kumbukumbu zilizoanza leo zitaendelea kutimia siku mia moja muda ambao mauaji hayo yaliyoua zaidi ya watu milioni moja yalidumu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news