Vuta ni kuvute yaendelea dhidi ya mapambano ya virusi vya Corona

Mamlaka nchini Uingereza  zimependekeza kuwa chanjo ya virusi vya coorna ya AstraZeneca isitolewa kwa watu walio chini ya umri wa miaka 30.
Uamuzi huo umefikiwa baada ya kuwepo ushahidi usio wa moja kwa moja kuwa chanjo hiyo inahusishwa na visa vya nadra vya kuganda kwa damu. 

Pendekezo hilo lilitolewa wakati wasimamizi wa sekta ya tiba nchini Uingereza na Umoja wa Ulaya wanasisitiza kuwa faida za kutumiwa chanjo ya AstraZeneca ni kubwa kuliko madhara yanayoripotiwa. 

Mamlaka za Uingereza zimetaka wale walio chini ya umri wa miaka 30 wapatiwe chanjo nyingine mbadala ya AstraZeneca, lakini wakala wa dawa wa Umoja wa Ulaya ulisema hakuna sababu ya kuweka zuio kama hilo. 

Mataifa kadhaa mengi ya Ulaya yalichukua uamuzi wa kusitisha kwa muda matumizi ya chanjo ya AstraZeneca mnamo mwezi Machi baada ya kuripotiwa visa kadhaa vya kuganda kwa damu kwa waliopatiwa chanjo hiyo.

Wakati huo huo, Rais Alberto Fernandez wa Argentina ametangaza amri ya kuzuia watu kutoka nje usiku kwa muda wa wiki tatu baada ya taifa hilo kurekodi idadi kubwa ya maambukizi ya virusi vya corona kwa siku ya pili mfululizo. 

Akitoa tangazo hilo kupitia ujumbe mfupi wa video, Rais Fernandez ambaye mwenyewe yuko karantani tangu alipoambukizwa COVID-19 alisema marufuku hiyo itaanza kufanya kazi leo na itaendelea hadi Aprili 30,mwaka huu. 

Alisema amri hiyo kwa sehemu kubwa itatekelezwa kwenye maeneo ya miji iliyo kwenye hatari huku maduka ya vileo na mikahawa itafungwa mapema. 

Hatua hiyo inafuatia wizara ya afya kutangaza visa vipya 22,039 vya covid-19 vilivyogundulika ndani ya saa 24 hususani kwenye kitovu cha mji mkuu Buenos Aires.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela, Jorge Arreaza amesema kuwa bila kuwepo vikwazo vya kiuchumi dhidi ya utawala wa Rais Nicolas Maduro taifa hilo lingekuwa limekwishanunua dozi zote milioni 30 za virusi vya corona zinazohitajika. 

Kwenye mahojiano na shirika la habari la AFP, Arreaza alisema iwapo rasilimali za Venezuela zisingezuiliwa nchi hiyo ingeweza kuwa imenunua chanjo za kutosha kwa ajili ya raia wote tangu miezi mitatu iliyopita. 

Hadi sasa taifa hilo ambalo limewekewa vikwazo vya kiuchumi na mataifa kadhaa ikiwemo Marekani limepokea shehena ya dozi 250,000 ya chanjo iliyotengezwa Urusi na dozi nyingine 500,000 kutoka China. 

Marekani, mataifa ya Ulaya na mengine kadhaa duniani hayautambui ushindi wa Rais Maduro wa kwenye uchaguzi wa mwaka 2018 wakidai ulighubikwa na dosari kubwa ya udanganyifu ikiwemo madai ya wizi wa kura.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news