Serikali kuwaondoa kwenye mpango wanufaika wa TASAF watakaoshindwa kutumia ruzuku kuboresha maisha yao

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema, Serikali haitosita kuwaondoa wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini watakaoshindwa kutumia vema ruzuku wanayopewa na TASAF ili kuboresha maisha yao kama ambavyo Serikali imekusudia, anaripoti Veronica Mwafisi (Momba).
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akisisitiza jambo kwa Kaimu Meneja Uhawilishaji Fedha wa TASAF Bw. Selemani Masala, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa TASAF katika Kijiji cha Nkala Wilayani Momba.

Mhe. Ndejembi amesema hayo akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika vijiji vya Msangano, Nkala na Chiwanda Wilayani Momba na kuongeza kuwa, baada ya mwaka mmoja atarejea kujiridhisha kama fedha za ruzuku zilizotolewa kwa kaya maskini zimetumika vizuri kuboresha maisha hivyo kaya zitakazobainika kutumia tofauti na malengo zitaondolewa kwenye mpango.

Amesisitiza kuwa, ni wajibu wa kila mnufaika kutumia ruzuku anayoipata katika shughuli zitakazomuongezea kipato kama kilimo na ufugaji ili kuboresha maisha yake, na kuongeza kuwa Maafisa Ugani wana jukumu la kuhakikisha wanawasaidia wanufaika kufuga na kulima kisasa.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wananchi na wanufaika wa TASAF Kijiji cha Nkala wilayani Momba wakati wa ziara yake ya kikazi kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika kijiji hicho.
Mbunge wa Jimbo la Momba, Mhe. Condesta Sichalwe akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kuzungumza na wananchi, kijiji cha Msangano wilayani Momba wakati wa ziara yake ya kikazi kukagua utekelezaji wa Mpango wa TASAF katika kijiji hicho.

Amewaasa wanufaika juu ya ruzuku wanayoipata kuwa si kwa ajili ya anasa kwani Serikali inatoa kwa kaya maskini ili kuziwezesha kujikwamua kwenye lindi la umaskini.

“Serikali inatoa fedha kwa kaya maskini ili ziweze kujishughulisha na ufugaji, kilimo na ujasiriamali na baada ya muda ziweze kuondokana na umaskini” Mhe. Ndejembi amefafanua.

Kuhusiana na Kijiji cha Msangano ambacho hakijanufaika na Mpango wa TASAF toka uanze, Mhe. Ndejembi amewaahidi wananchi wa kijiji hicho kuwa, ifikapo mwezi Julai kaya maskini kijijini hapo zitaanza kunufaika na TASAF.
Baadhi ya wananchi Kijiji cha Msangano Wilayani Momba wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa TASAF katika kijiji hicho.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akimpatia fedha mnufaika wa TASAF Kijiji cha Nkala Wilayani Momba, Bi. Sarafina Simfukwe mara baada ya kumtembelea nyumbani kwake na kuona maendeleo aliyoyapata kutokana na ruzuku anayoipokea kutoka TASAF.
Baadhi ya wananchi Kijiji cha Nkala Wilayani Momba wakinyoosha mikono hewani kuashiria ni wanufaika wa TASAF wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa TASAF katika kijiji hicho.

Sanjali na hilo, Mhe. Ndejembi amewataka Watendaji wa Serikali kutokata fedha za ruzuku za wanufaika kwa ajili ya kuchangia huduma za Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) na michango mingineyo kwani fedha hiyo ni yake kwa ajili ya kuboresha maisha yake.

Mhe. Ndejembi amesisitiza kuwa, kama kuna mchango wowote ni wa hiari hivyo si lazima akatwe ruzuku yake, na kuongeza kuwa mnufaika apewe fursa ya kuitumia fedha kujiendeleza kiuchumi katika ufugaji au kilimo ili akifuga na kuvuna achangie kwa hiari yake mwenyewe.

Aidha, Mhe. Ndejembi amewahakikishia wananchi wa vijiji vya Msangano, Nkala, Chiwanda na maeneo mengine kuwa, Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuzijali kaya maskini kwa kuzipatia ruzuku, hivyo amezitaka kutumia vizuri ruzuku hizo ili kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha maisha ya kaya maskini nchini.

Mhe. Ndejembi amefanya ziara ya kikazi ya siku moja Wilayani Momba kwa lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wilayani humo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi aliyoitoa hivi karibuni kwa Mbunge wa Jimbo la Momba Mhe. Condesta Sichalwe wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news