Waasi wamuua Rais Idriss Deby

Jeshi la Chad limetangaza kuwa Rais wa nchi hiyo Idriss Deby (68)amefariki baada ya kupata majeraha kwenye mapambano dhidi ya waasi.
Deby alienda mstari wa mbele mwishoni mwa wiki kuvitembelea vikosi vya nchi hiyo ambavyo vinapambana na waasi kaskazini mwa nchi hiyo. Waasi hao wamevuka mpaka wakitokea Libya.

Kifo chake kimetokea ikiwa ni saa chache tu tangu matokeo ya awali ya uchaguzi uliofanyika Aprili 11 kuonesha kuwa anaongoza kwa asilimia 80. Kwa ushindi huo, Deby angeiongoza nchi hiyo kwa awamu ya sita mfululizo.

Serikali na bunge vimevunjwa na sasa baraza la kijeshi ndilo litakaloiongoza nchi hiyo kwa kipindi cha miezi 18 ijayo.

Bw. Déby aliingia madarakani mwaka 1990 baada ya mapinduzi ya kijeshi.

Waasi hao kutoka kundi linalojiita Fact (the Front for Change and Concord in Chad), walishambulia kitua cha mpaka wa Libya na Chad siku ya uchaguzi, yaani Aprili 11. Walikuwa wakisonga mbele kuelekea mji mkuu wa N'Djamena.

Mapambano baina ya waasi na wanajeshi wa serikali yaliaza siku ya Jumamosi. Jenerali wa jeshi ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa waasi 300 waliuawa na wengine 150 kukamatwa katika mapambano hayo. Aliongeza kuwa jeshi lilipoteza askari watano na wengine 36 wakijeruhiwa. Hata hivyo idadi hiyo haikuweza kuthibitishwa mara moja.

Bw. Déby kwa muda mrefu amekuwa mshirika mkubwa wa Ufaransa na mataifa mengine ya magharibi. Hata hivyo kumekuwa na ongezeko la ukosoaji ndani ya nchi kwa namna ambavyo serikali yake ilikuwa ikitumia mapato yatokanayo na mauzo ya mafuta.

Wakati wa kampeni za uchaguzi, aliahidi kuboresha amani na ulinzi katika ukanda huo.

'Mtoto wa Deby kuongoza nchi'

Shirika la habari la kimataifa la AFP linamnukuu msemaji wa jeshi kuwa mtoto wa rais aliyeuawa ndiye atakayeliongoza baraza la kijeshi linaloiongoza nchi hiyo.

Mtoto huyo, Mahamat Idriss Deby, 37, ni manajeshi wa cheo cha juu cha jenerali.

Baba yake pia alikuwa mwanajeshi, na alisifika ndani na nje ya nchi kwa harakati zake za kupambana na waasi.

Mwaka jana, 2020, alipewa cheo cha juu zaidi cha kijeshi cha Field Marshall kutokana na harakati zake.

Jeshi limetangaza marufuku ya kutoka nje wakati wa usiku, kuanzia saa 12 jioni mpaka saa 11 alfajiri kuanzia leo. Pia mipaka yote ya nchi hiyo ikiwemo anga imefungwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news