Waganga wakuu wa mikoa waagizwa kusimamia nidhamu za watumishi wao

Serikali imewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini kuhakikisha wanasimamia nidhamu na maadili ya watumishi walio chini yao ili waweze kutoa huduma nzuri kwa wananchi,anaripoti Maiko Luoga, Wanging’ombe.
Agizo hilo limetolewa jana na Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Festo Dugange wakati akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Wangutwa Kata ya Uhambule Wilayani Wanging’ombe Mkoa wa Njombe.

Amesema ni wajibu wa Viongozi hao kuhakikisha kuwa nidhamu na maadili ya kazi yanazingatiwa na watendaji walio chini yao na kuahidi kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi wanaokiuka maadili yao ya kazi.

Agizo hilo la Dkt. Dugange linafuatia malalamiko ya wananchi wa kijiji cha Wangutwa kulalamikia huduma mbovu inayotolewa na watumishi wa afya wa zahanati ya kijiji hicho.

Akizungumza kwa niaba ya wakazi wa kijiji hicho, Mwenyekiti wa Kijiji cha Wangutwa Salumu Ngella amedai kuwa mara nyingi Mganga na manesi wa zahanati hiyo wamekuwa hawapatikani kwenye Kituo chao cha kazi, na pia wamekuwa wakitoa lugha mbaya kwa Wagonjwa.

Mwenyekiti huyo pia ameeleza kero nyingine ni kwa watumishi hao wa afya kutotoa huduma za haraka kwa Wagonjwa huku wakisema hadi wamalize ratiba zao.

“Kwa kweli Daktari aliyepo hapa na baadhi ya wauguzi hawana mahusiano mazuri na Uongozi wa Kijiji, wao wanasema mwenye uwezo wa kuzungumza nao ni yule aliyewaajiri sio sisi wa huku Kijijini,” amesema Ngella na kuongeza:

“Kuna wakati tuliwapoteza wakazi wenzetu wawili hapa kijijini kwa kukosa huduma za haraka, alipofuatwa muuguzi wa zamu alisema anakula kwanza ndio aje kutibu.”

Kufuatia kutolewa kwa kero hiyo Dkt. Dugange ameahidi kuifanyia kazi na kuwa kuanzia sasa serikali itachukua hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi watakaobainika kutoa lugha mbaya kwa wagonjwa.

“Mimi nimelichukua hili, Kuna tatizo kubwa la kusimamia Watendaji wetu, sio wote wabaya lakini tatizo lipo kwenye usimamizi kote nchini tutachukua hatua za kinidhamu kwa kuzingatia Sheria kwa wote wanaofanya mchezo na Afya za Wananchi,” amesema.

Amewataka watumishi wa Afya nchini kufanya kazi kwa kuzingatia Taratibu, nidhamu na maadili ya kutoa huduma kwa Wananchi wanaofika kwenye Vituo vya Afya kufuata matibabu.

Pamoja na kufanya mkutano wa hadhara katika kijiji cha Wangutwa kilichopo kata ya Uhambule pia Dkt. Dugange alipata fursa ya kuzungumza na Wananchi wa Vijiji vya Mtapa na Igwachanya katika Kata ya Igwachanya Wilayani Wanging’ombe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news