Watakiwa kutumia Wiki ya Utumishi wa Umma 2021 kutatua changamoto zinazowakabili watumishi waliopo pembezoni

Na James K. Mwanamyoto-Karema

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amewataka viongozi katika Taasisi za Umma kutumia Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka huu kutembelea maeneo ya pembezoni ili kusikiliza na kutatua kero na changamoto zinazowakabili Watumishi wa Umma, ikiwa ni pamoja na kupokea maoni na mapendekezo ya namna bora ya kuboresha Utumishi wa Umma nchini.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akizungumzia masuala ya kiutumishi na watumishi wa Tarafa ya Karema Wilayani Tanganyika.
Watumishi wa Umma wa Tarafa ya Karema wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu huyo ya kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto za watumishi wa tarafa hiyo.
Mwalimu Baraka Ambonile wa Shule ya Msingi Kapalamsenga, Tarafa ya Karema Wilayani Tanganyika akiwasilisha changamoto yake ya kiutumishi kwa Dkt. Laurean Ndumbaro wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu mkuu huyo tarafani humo.Dkt. Ndumbaro amesema hayo katika Tarafa ya Karema akiwa ameambatana na Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome pamoja na Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu ambao kwa pamoja wamehimiza uwajibikaji na ufanisi kiutendaji katika taasisi zinazosimamia utoaji wa haki kwa wananchi.

Aidha Dkt. Ndumbaro amewata viongozi katika Taasisi za Umma kuhakikisha wanajenga utamaduni wa watumishi kufanya kazi kwa bidii, na kuongeza kuwa utamaduni huo utajengwa kwa kutambua na kuwapongeza wanaofanya kazi kwa juhudi na maarifa na kwa wanaolegalega warekebishwe ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi.

Amefafanua kuwa, watumishi wanaochapa kazi wakipongezwa kwa kuandikiwa barua au kupewa cheti kutokana na mchango wao ndio njia pekee itakayowawezesha waajiri kujenga utamaduni wa watumishi kufanya kazi kwa bidii na weledi. tofauti na kuchukua hatua hiyo morali ya watumishi wanaowajibika ipasavyo itashuka kwa kiwango kikubwa.

Akizungumzia kuhusu mtazamo hasi wa baadhi ya watumishi wa Tarafa ya Karema kuamini kuwa wanafanya kazi katika mazingira magumu sana, Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amewataka kubadili fikra zao kwani Serikali imewaajiri kwa lengo la kuwahudumia wananchi wa eneo hilo na si kuwapa adhabu kama baadhi yao wanavyodhani.
Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama akipokea hoja za masuala ya kiutumishi za watumishi wa Tarafa ya Karema toka kwa Afisa wa tarafa hiyo, Bw. Mbonimpaye Nkoronko kwa lengo la kuzifanyia kazi changamoto hizo.

Dkt. Jingu amewaambia watumishi hao kuwa, Utumishi wa Umma ni popote hivyo amewataka kutumia fursa zilizopo katika Tarafa ya Karema kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.

Naye, Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome amesema katika sheria na masuala ya katiba ndio taifa linapata mfumo wa utoaji haki ambapo haki zipo za aina nyingi kama vile haki madai, haki jinai pamoja na haki utawala inayosimamiwa na Katibu Mkuu - UTUMISHI kuhakikisha inakwenda sawasawa ili wananchi wapate huduma bora katika Taasisi za Umma.

Sanjali na hilo, Prof. Mchome amesema, migogoro ya ardhi iliyopo Karema ni changamoto kama ilivyo kwenye maeneo mengine, hivyo amewataka watumishi kushirikiana na wananchi hususani wazee wenye busara katika kutatua migogoro hiyo kwa njia ya usuluhishi badala ya kukimbilia Mahakamani kwani Mahakama kwa mujibu wa Katiba ni chombo cha mwisho cha utoaji haki.

Ziara ya Makatibu Wakuu hao mkoani Katavi ililenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi mkoani humo.

Post a Comment

0 Comments