MARA MSHINDI WA JUMLA UMITASHUMTA 2021

Na Mathew Kwembe, Mtwara

Mkoa wa Mara umefanikiwa kuwa mshindi wa jumla wa mashindano ya 25 ya UMITASHUMTA 2021 baada ya kujikusanyia alama nyingi kuliko mikoa mingine 26 iliyoshiriki mashindano hayo mwaka huu.

Mkoa wa Mara umechukua taji hilo la kuwa mkoa bingwa kutoka kwa mabingwa wa jumla wa UMITASHUMTA wa mwaka 2019 mkoa wa Tabora ambapo mwaka huu wameshika nafasi ya saba.
Nafasi ya pili ya bingwa wa jumla kwa mwaka huu imechukuliwa na mkoa wa Mwanza, huku nafasi ya tatu ikishikwa na mkoa wa Dar es salaam katika mashindano ya UMITASHUMTA yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo cha Ualimu na Shule ya Ufundi Mtwara.

Mkoa wa Mara umefanikiwa kuvuna alama nyingi kupitia michezo ya soka wasichana, na wavulana, mpira wa mikono wasichana, mpira wa wavu wavulana, Netiboli, riadha wasichana na wavulana, na usafi na nidhamu kwa wavulana ambapo timu za mkoa huo zilishika nafasi ya kwanza hadi ya tatu kwa kila michezo hiyo.

Mkoa wa Mwanza umejizolea alama nyingi kupitia soka wasichana, mpira wa mikono wavulana, michezo ya mpira wa wavu kwa wavulana, na Netiboli kwa wasichana ambapo timu hiyo ndiyo mabingwa wa michezo hiyo, huku timu yao ya riadha wasichana ikishika nafasi ya pili.

Kwa upande wa Mkoa wa Dar es salaam ambao ndiyo mabingwa wapya wa UMITASHUMTA katika mchezo wa soka kwa wavulana mwaka huu baada ya kuifunga timu ya soka ya mkoa wa Mara magoli 4-0 umeshika nafasi ya tatu kupitia soka wavulana, soka wasichana na soka maalum mkoa umeshika nafasi ya pili, na sanaa za maonyesho amapo kwaya umeshika nafasi ya tatu na ngoma nafasi ya pili.

Mkoa mwingine ambao umefanya vizuri mwaka huu ni Tanga ulioshika nafasi ya nne baada ya timu zake za mpira wa mikono wavulana, mpira wa goli wasichana, na sanaa za maonesho katika kipengele cha ngoma kushika nafasi za kwanza.

Mkoa wa Morogoro ulishika nafasi ya tano baada ya timu zake za mpira wa goli wavulana na wasichana kushika nafasi ya kwanza na ya pili.

Wenyeji mkoa wa Mtwara ulishika nafasi ya sita baada ya timu yake ya mpira wa wavu wasichana kufanikiwa kutwaa ubingwa mwaka huu,na kufuatiwa na mikoa ya Tabora, na Mbeya walioshika nafasi ya nane baada ya kuwa washindi wa pili katika mpira wa wavu wasichana.

Mgeni rasmi katika kilele cha UMITASHUMTA 2021 ni Naibu Waziri Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Philipo Gekul.

Katika hotuba yake Mhe.Gekul amepongeza ushirikiano wa wizara tatu yaani Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Naibu Waziri amewapongeza wanamichezo walioshinda mashindano ya UMITASHUMTA mwaka huu kwa kuonyesha vipaji vyao na amewataka ambao hawakushinda kutokata tamaa kwa kuwa washindanapo wawili hupatikana mshindi mmoja.

Kilele cha mashindano ya UMITASHUMTA kilihitimishwa kwa fainali ya mchezo wa soka kati ya timu ya mkoa wa Dar es salaam dhidi ya Mara katika mchezo uliochezwa uwanja wa Nangwanda ambapo Dar es salaam ilifanikiwa kuchukua taji la ubingwa wa soka UMITASHUMTA kwa kuifunga Mara magoli 4-0.

Post a Comment

0 Comments