WAZIRI BITEKO AZINDUA RASMI NMB MINING CLUB JIJINI DODOMA

 Aipongeza Benki ya NMB kwa ubunifu wa kutafuta wateja kwenye Sekta ya Madini

 Asisitiza ushirikiano kwa mabenki kwa msaada wa kitaalamu

Na Steven Nyamiti, Dodoma

Waziri wa Madini Doto Biteko amezindua rasmi Jukwaa la Wadau wa Madini kupitia Benki ya NMB lenye lengo la kuwakutanisha pamoja wafanyabiashara, wachimbaji na wadau wa madini ili kuwa na sauti moja katika kujadili changamoto wanazokabiliana nazo na kuzitafutia ufumbuzi kwa pamoja.
Hafla ya Uzinduzi wa Jukwaa hilo unaokwenda kwa jina la NMB MINING CLUB umezinduliwa tarehe 28 Juni, 2021 katika Hotel ya Morena Jijini Dodoma na kuhuhudhriwa na wadau mbalimbali wa Sekta ya Madini.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Biteko amesema kuwa, ili kuwarahisishia wachimbaji kupata mikopo kwa urahisi katika mabenki ikiwemo vifaa vya uchimbaji, Wataalam wa Wizara ya Madini hawanabudi kutoa ushirikiano kwa mabenki pindi yanapohitaji msaada wa kitaalamu ili yaweze kutoa mkopo kwa wateja wao kwani baadhi ya mabenki yameshindwa kutoa mkopo kwa wachimbaji kutokana na kukosa elimu ya kutosha kuhusu sekta ya madini.

” Ninatoa rai kwa mabenki nchini kuungana kwa pamoja na kutoa mikopo mikubwa kwa wawekezaji wakubwa wa madini wanaotaka kuwekeza nchini ili faida inayotokana na mikopo hiyo ibaki nchini,” amesema Waziri Biteko.

Akijibu hoja mbalimbali zilizowasilishwa na watoa mada, Waziri Biteko amesema Wizara ya Madini inapokea mapendekezo yatakayowasilishwa katika kuangalia njia sahihi ya wachimbaji wa madini kukopesheka kupitia jukwaa hilo na kusisitiza njia rahisi ni kupitia vyama vyao vya uchimbaji pamoja na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambalo pia linafanya kazi ya kuwalea wachimbaji wadogo.

” Kwa kupitia STAMICO tumeanzisha mchakato wa kuangalia dhamana kwa wale wote wanaokwenda kukopa kwenye mabenki ili kujiridhisha na utaratibu huo utakamilika hivi karibuni,” amesisitiza Biteko.

Aidha, Waziri Biteko ametoa wito kwa jukwaa hilo kuendelea kutoa elimu kwa wadau wa Sekta ya Madini kuhusu umuhimu wa kupendana na kuthaminiana kwani bila upendo Sekta ya Madini haiwezi kufika popote.

Waziri Biteko ameipongeza Benki ya NMB kwa ubunifu huo kwenye Sekta ya Madini na kueleza kuwa kupitia klabu hiyo iliyoanzishwa na benki ya NMB itapata fursa ya kupata wateja wengi waliopo kwenye Sekta ya Madini.

Naye, Afisa Mkuu wa Mikopo wa Benki ya NMB Daniel Mboto amesema lengo la kuandaa jukwaa hilo ni kutoa nafasi ya kuimarisha mahusiano ya kibiashara kati ya wadau na benki ya NMB na kuongeza kwamba, uzinduzi huo mkoani Dodoma ni mwanzo wa kuzungumza na wadau wa Sekta ya Madini katika kutoa huduma mbalimbali ili kuwapa uelewa zaidi wa huduma za NMB.

Jukwaa hilo la NMB Mining Club lililozinduliwa leo na Waziri Biteko mkoani Dodoma, linatarajia kufanyika katika mikoa mingine saba hapa nchini .

Wengine waliohudhuria Uzinduzi huo ni pamoja na Kamishna wa Madini Mhandisi David Mulabwa, Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo Tanzania (FEMATA) John Bina, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Dodoma Chagwa Marwa, wataalam kutoka Wizara na Tume ya Madini, wafanyakazi wa Benki ya NMB na wadau mbalimbali wa Sekta ya Madini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news