Waziri Ndalichako, Prof.Busagala waainisha faida za teknolojia ya nyuklia

Rachel Balama na Aneth Kagenda, Diramakini Blog

Teknolojia ya nyuklia ni teknolojia mtambuka na inatumika katika sekta mbalimbali ikiwemo viwanda, afya, ujenzi, maji, kilimo na nyinginezo. Kwa mfano kwenye sekta ya kilimo hii teknolojia ya nyuklia huwa inatumika katika utafiti wa kuboresha mbegu


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako ameyasema hayo leo Juni 12, 2021 mkoani Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo ya Kitaifa kwa wahariri na waandishi wa habari juu ya uelewa na udhibiti yakiwemo matumizi salama ya mionzi nchini yaliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ukumbi wa Jengo la Utawala.
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako akifungua semina ya wahariri na waandishi wa habari iliyoandaliwa na Tume ya Nguvu za Atomiki (TAEC) na kufanyika mkoani Dar es Salaam.

Mafunzo hayo ya siku moja yameandaliwa na Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa mikakati yake ya kuyafikia makundi mbalimbali katika jamii ili kuyajengea uwezo kuhusu udhibiti na matumizi salama ya mionzi nchini kwa manufaa ya Taifa na mwananchi mmoja mmoja. 

Pia yameangazia mada mbalimbali ikiwemo vitambuzi vya mionzi, madhara yatokanayo na mionzi, usalama wa mionzi na matumizi ya mionzi.

Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) iliundwa kwa Sheria ya Nguvu za Atomu Na. 7 ya Mwaka 2003 (Atomic Energy Act No.7 of 2003).Sheria ya Bunge Na. 7(2003) ilifuta Sheria Na.5 ya mwaka 1983 (The Protection from Radiation, No. 5 of 1983) iliyoanzisha Tume ya Taifa ya Mionzi (National Radiation Commission).

Sheria hii imeipa TAEC mamlaka ya kudhibiti matumizi salama ya mionzi nchini ikiwemo kuhamasisha matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia nchini.

Ni kutokana na ukweli kwamba, teknolojia ya nyuklia inatumika katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii kama vile afya, kilimo, ufugaji, viwanda, maji na utafiti.Soma hapa, unayopaswa kuyafahamu kwa kina kuhusu Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC)
Waziri Profesa Ndalichako ambaye alikuwa mgeni rasmi katika semina hiyo amesema kuwa, mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wadau mbalimbali ili kuondoa dhana potofu kuhusu kazi za tume ikiwemo madai kuwa, wana jukumu la kutengeneza zana za nyuklia jambo ambalo halina ukweli wowote katika jamii.

"Hivyo, kufuatia mafunzo haya tuna imani kwamba yatasaidia kutoa uelewa kwa kiasi kikubwa pia kupunguza madhara kwa wananchi na mazingira kupitia matumizi ya mionzi isiyo salama, kwa kuwa waandishi wa habari na wahariri ni kiungo muhimu katika jamii kufikisha taarifa na kuijengea jamii uelewa kuhusu jambo fulani,"ameeleza Profesa Ndalichako.

Waziri Ndalichako amesisitiza kuwa, teknolojia ya nyuklia ina faida kubwa kwa jamii na Taifa kwani inatumika katika sekta mbalimbali kwa ajili ya kufanikisha tafiti zinazotoa majibu yenye tija na maslahi mapana kwa Taifa na jamii.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), Profesa Lazaro Busagala amesema kuwa, wamejipanga kuyafikia makundi mbalimbali katika jamii ili kuyajengea uelewa juu ya matumizi salama ya mionzi hapa nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), Profesa Lazaro Busagala akizungumza wakati wa mafunzo ya Kitaifa kwa wahariri na waandishi wa habari yaliyofanyika leo mkoani Dar es Salaam.

Profesa Busagala amesema kuwa, mafunzo hayo yanaweza kusaidia kuondoa zana potofu katika jamii kwani kumekuwa na uelewa hafifu kuhusu matumizi ya mionzi.

TAEC imepewa jukumu la kupima mionzi kutokana na sababu mbalimbali, kwani licha ya kuwa na faida nyingi za mionzi, isipotumika inavyotakiwa ni hatari ikiingia katika mnyororo wa chakula kwa sababu inatoa nishati toka katika kiini cha atomu ambayo haiwezi kuharibiwa kwa aina yoyote ile.

Kwa mujibu wa tume hiyo, viasili vya mionzi vinaweza kuathiri afya ya binadamu na wanyama. Hivyo, sababu kuu za kupima mionzi katika mnyororo wa chakula ni kuhakikisha chakula kinacholiwa na Watanzania hakina mionzi na hivyo kuwa salama kwa matumizi ya kawaida.

Pia ni muhimu kuhakikisha kuwa soko la bidhaa zinazouzwa nje ya nchi zinalindwa ili kuzingatia ubora na viwango vilivyowekwa kulingana na miongozo na taratibu mbalimbali za Serikali.

Katika hatua nyingine, Profesa Busagala anasema kuwa, wanaendelea kutekeleza miradi mbalimbali na sasa wanatarajia kuja na mradi wa kuhifadhi mazao kupitia mionzi na michakato inaendelea, hivyo mwishoni mwa mwezi huu watajua pa kuanzia.Soma hapa, BILIONI 10/- ZATUMIKA KUJENGA MAABARA CHANGAMANO TUME YA NGUVU ZA ATOMIKI TANZANIA

Profesa Busagala amesema, mradi huo utakuwa na tija kubwa kwani, mazao ambayo yatakaushwa kupitia mionzi huwa hayana mabaki ya kemikali au viambata vya kemikali.

Ndiyo maana wanatarajia kufanikiwa kwa mradi huo utasaidia kuimarisha soko la ndani na nje hususani kwa mataifa ambayo huwa hayaruhusu uingizaji wa bidhaa za mazao zilizohifadhiwa kwa kemikali.

Pia amesema, kuhifadhi mazao kupitia mionzi huyawezesha kukaa muda mrefu bila kuharibika. 

"Kwa mfano vitunguu vilivyohifadhiwa kwa mionzi vinaweza kukaa muda mrefu bila kuharibika, hadi miezi mitatu, vivyo hivyo nyanya zinaweza kukaa muda mrefu bila kuharibika, hivyo mradi huo una faida kubwa,"amesema.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Wiliam Anangisye akizungumza wakati wa mafunzo ya Kitaifa kwa wahariri na waandishi wa habari yaliyofanyika leo mkoani Dar es Salaam.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa William Anangisye amesema kuwa, chuo hicho ni mdau mkubwa wa masuala ya nguvu za atomiki kwani wana kozi maalumu kuhusu masuala ya nguvu za atomiki nchini.

“Kwa mwaka wa masomo 2020/2021 Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimedahili wanafunzi 60 wanaosoma kozi inayohusiana na nguvu za atomiki na kuna wanafunzi saba wanaosomea Shahada ya Umahiri kuhusu masuala ya nguvu za atomiki,"amesema.

Amesema kuwa, pia chuo kimeendelea kutoa hamasa kwa wanafunzi kusoma masomo yanayohusiana na nguvu za atomiki ili kuwezesha Taifa kupata wataalamu wengi zaidi.

Post a Comment

0 Comments