Liliani Badi ndiye Mwenyekiti mpya Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali

Na Doreen Aloyce, Diramakini Blog

WAJUMBE wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) wamemchagua, Liliani Badi kuwa mwenyekiti wa baraza hilo mara baada ya kumshinda mpinzani wake Jane Magigita.
Katika uchaguzi huo ulifanyika jijini Dodoma, Liliani Badi aliibuka na ushindi wa kura 21 huku mpinzani wake Jane Magigita akipata kura 8.
Akiongea mara baada ya kutangazwa mshindi wa baraza hilo, Lilian ameahidi kutekeleza yale yote aliyoyasema wakati wa kujinadi na kuomba ridhaa ya kuwa mwenyekiti wa NaCoNGO ambapo amebainisha kwamba, ataanza na vipaumbele muhimu katika kuinyanyua NaCoNGO mpya.

Pia viongozi wengine waliochaguliwa katika mkutano huo ni Katibu Mkuu, Revocatus Somo, Mweka Hazina, Joho Kitete, Kamati ya Maadili Novatus Marandu,Kamati ya fedha na utawala Gaidon Haule, Maendeleo ya Uwezo Rhobi Samwelly,Utanda na mawasiliano Asifiwe Mallya, Mjumbe wa Bodi Jane Magigita, Mjumbe wa Bodi Revocatus Sono,Mjumbe wa Bodi Paulina Majogolo na mjumbe wa bodi Baltazar Komba.
Ikumbukwe kwamba Juni 7, mwaka huu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Dkt.Dorothy Gwajima alifanya uteuzi wa Kamati ya mpito kwa ajili ya kuratibu na kusimamia uchaguzi wa Baraza la Taifa la Mashirika yasio ya Kiserikali (NaCoNGO) ambapo kamati hiyo iliundwa na Wajumbe 10 kutoka Mashirika yasiyo ya Kiserikali ya kitaifa na Kimataifa na ilipewa muda wa siku 30 kufanikisha kazi hiyo.

Akitangaza matokeo Julai 8, mwaka huu jijini hapa Mwenyekiti wa Kamati ya Mpito Wakili Flaviana Charles amesema zoezi la uchaguzi lilifanyika kwa amani na utulivu huku akiwataka wajumbe wote kufanya kazi kwa kushirikiana katika kulisukuma gurudumu maendeleo la Taifa.

"Sasa kazi iendelee, tufanye kazi kwa pamoja na tukayaondoe makundi yaliokuwepo ndani yetu katika kipindi kile cha kampeni mpaka uchaguzi, kikubwa tukumbuke kwamba uchaguzi umekwisha sasa sisi sote ni wamoja ,"amesema Wakili Flaviana.

"Hongereni kwa viongozi wapya wa NaCoNGO kwa ushindi lakini pia poleni kwa wale wagombea waliokosa nafasi,kumbukeni nyinyi pia ni washindi ila tu kura hazikutosha na asiyekubali kushindwa sio mshindani," amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa NGos, Richard Simbaiga amesema wagombea wote wameshinda isipokuwa kwa wale walioshindwa waelewe kuwa kura hazikutosha lakini pia uchaguzi huo umefungua ukurasa mpya.

Amesema, uchaguzi umemalizika sasa kazi iendelee hivyo makundi na kambi zilizokuwepo kipindi cha uchaguzi kazi yake imekwisha na sasa kambi inayojulikana ni Kambi au kundi la NaCoNGO.

"Kikubwa twende tukafanye kazi yenye tija ili kwenye Sekta ya NGos tufanye mabadiliko na tufanye kazi huku tukiimarisha mifumo ya kitaasisi ndani ya mabaraza kuanzia chini, pia tujenge mifumo ndani ya NaCoNGO na tuimarishe mifumo ya mashirika, " amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news