Mradi wa maji Mkata kunufaisha wananchi 44,663

Na Yusuph Mussa, Diramakini Blog

UPANUZI wa Mradi wa Maji Mkata uliopo Wilaya ya Handeni mkoani Tanga utaongeza idadi ya wananchi watakaopata huduma ya maji kutoka 16,678 na kufikia 44,663 ifikapo mwishoni mwa Julai, mwaka huu.
Mafundi wa RUWASA wakiunganisha mabomba kwenye Upanuzi wa Mradi wa Maji Mkata uliopo Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, wakiongozwa na Mhandisi Rebius Fortunatus (kushoto). (Picha na Yusuph Mussa).

Ni baada ya upanuzi huo wa Awamu ya Kwanza wenye mtandao wa mabomba wa kilomita 4.68 kuongeza upatikanaji wa maji kwa wananchi 27,985, kwani utakuwa na tenki lenye ujazo wa lita 500,000 na vituo vya kuchotea maji (vilula) vitano.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Julai 10, 2021, Meneja wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Handeni Mhandisi Hosea Mungizi, alisema katika Awamu ya Kwanza ya upanuzi wa mradi huo utagharimu sh. milioni 551,632,353.
Mtaro utakaopita mabomba. Ni upanuzi wa Mradi wa Maji Mkata uliopo Wilaya ya Handeni mkoani Tanga. (Picha na Yusuph Mussa).

Mhandisi Mungizi alisema mradi huo ulioanza kwa ujenzi wa tenki Januari 12, mwaka huu chini ya mkandarasi Kampuni ya D&L ya Dar es Salaam linalojengwa kwa gharama ya sh. milioni 253,987,715, na ujenzi wake kufikia asilimia 93, ujenzi wa utandazaji mabomba unafanywa na wataalamu wa RUWASA, na umefikia asilimia 80, na mradi wote unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Julai, mwaka huu.
Tenki lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita 500,000 likijengwa kwenye upanuzi wa Mradi wa Maji Mkata uliopo Wilaya ya Handeni mkoani Tanga. (Picha na Yusuph Mussa).

"Ujenzi wa Mradi wa Maji Mkata Awamu ya Kwanza, ulianza kwa ujenzi wa tenki Januari 12, 2021. Lakini ujenzi wa utandazaji mabomba wa kilomita 4.68 ulianza Juni 29, 2021, ambapo gharama ya mradi wote ni sh. milioni 551,632,353, na utakamilika mwishoni mwa mwezi wa saba, mwaka huu.

"Mradi huu wa upanuzi wa maji Mkata ni wa mtandao wa mabomba wa kilomita 13.311, lakini kwa Awamu ya Kwanza ni kilomita 4.68, na Awamu ya Pili itakapoanza mara baada ya upatikanaji wa fedha, tutaingia Awamu ya Pili yenye mtandao wa mabomba wa kilomita 8.631, na makadirio yetu ni mradi huu utakapokamilika Awamu ya Kwanza na Awamu ya Pili, ni kuhudumia watu 41,314 ifikapo mwaka 2041," alisema Mhandisi Mungizi.

Mungizi alisema mradi huo chanzo chake ni bwawa, ambapo maji kutoka kwenye bwawa hadi kwenye tenki hilo yatasukumwa kwa kutumia pampu. Na kutoka kwenye tenki hilo hadi tenki lenye ujazo wa lita 300,000, maji yatakwenda kwa mserereko.
Mabomba yakiwa yamewekwa eneo la kazi (site) kabla ya kufukiwa kwenye mtaro. Ni upanuzi wa Mradi wa Maji Mkata uliopo Wilaya ya Handeni mkoani Tanga. (Picha na Yusuph Mussa).

"Mradi huu wa upanuzi ambao utanufaisha wananchi wa Kata ya Mkata ni muhimu sana, hasa baada ya Mkata kuwa Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni. Na mradi huu, pamoja na kuongeza upatikanaji wa maji kwa wananchi, lakini pia yatakwenda kwenye taasisi za Serikali ikiwemo Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni na Ofisi za Halmashauri.

"Na tunapenda kuwahakikishia wananchi kuwa maji ya mradi huu hayatamalizika, kwani maji yaliyopo kwenye bwawa yana uwezo wa kutosheleza mradi huu kwa miaka miwili bila mvua kunyesha. Hivyo kikubwa, ni wananchi kulinda miundombinu ili mradi uwe endelevu, na makadirio ya mradi ni kuhudumia wananchi kwa miaka 20 bila kuwepo matatizo makubwa," alisema Mungizi.
Mafundi wakiwa kazini. Ni katika ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji lita 500,000. Ni upanuzi wa Mradi wa Maji Mkata uliopo Wilaya ya Handeni mkoani Tanga. Mhandisi wa RUWASA Wilaya ya Handeni Rebius Fortunas (katikati) na Mhandisi Muganyizi Kahama (kulia) wa Kampuni ya D&L (T) Ltd inayojenga tenki hilo. (Picha na Yusuph Mussa).

Mji Mdogo wa Mkata umekuwa una changamoto kubwa ya maji. Na hata mradi uliokuwepo ulikuwa hautoshelezi mahitaji ya wananchi, kwani ulikuwa na na uwezo wa kuwahudumia wananchi 16,678, huku tenki lake likiwa na ujazo wa lita 300,000, hivyo kilio cha maji kilikuwa kikubwa

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news