Tanzania yazidi kuhimili mfumuko wa bei EAC

 Na Doreen Aloyce, Diramakini Blog

IMEELEZWA kuwa Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Juni,2021 umeongezeka hadi asilimia 3.6 kutoka asilimia 3.3 kwa mwaka ulioishia mwezi Mei,2021.Takwimu hizo zimetolewa jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii, Ruth Minja wakati alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari juu ya mfumuko wa bei, ambayo utolewa kila mwezi.

Minja amesema kuwa, kuongezeka kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Juni ,2021 kumechangiwa hasa na kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa bidhaa zisizo za vyakula.

Ametaja bidhaa hizo kuwa ni pamoja na vitambaa vya nguo kwa asilimia 8.5,nguo za wanawake kwa asilimia 6.3,viatu vya wanaume kwa asilimia 6.2,kodi ya pango kwa asilimia 4.9 ,vyakula kwenye migahawa kwa asilimia 5.6 na gharama za malazi kwenye nyumba za kulala wageni kwa asilimia 5.7.

"Mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Juni 2021 umepungua hadi asilimia 4.7 kutoka asilimia 4.9 kwa mwaka ulioishia mwezi Mei 2021,"amesema Minja.

Akiongea kuhusu kupanda kwa mafuta ya Petroli amesema kuwa, mabadiliko hayo bado hayana athari kwenye mfumuko wao wa bei na kama bei zitaendelea kupanda wataaona athari mwezi ujao.

"Kuhusu nguo za wanawake na viatu kupanda ni kutokana na uhaba wa bidhaa sokoni ikiwa ni pamoja na uzalishaji, uingizaji na kuna sababu nyingi na sisi tukishatoa takwimu wale wachumi ndiyo wanaenda kufuatilia kujua ni kwa nini vimepanda,"amesema.

Minja ameongeza kuwa, kwa upande wa nchi za Afrika Mashariki nchini Kenya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Juni 2021 umeongezeka hadi kufikia asilimia 6.32 kutoka asilimia 5.87 kwa mwaka ulioishia mwezi Mei 2021.

"Kwa upande wa Uganda mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Juni 2021 umeongezeka pia hadi asilimia 2.0 kutoka asilimia 1.9 kwa mwaka ulioishia mwezi Mei 2021,"amesema.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi,Daniel Maswola amesema Ofisi ya Takwimu kuanzia mwezi huu wamejipanga kuwa na tovuti kwa ajili ya kurahisishia wananchi kupatakwimu badala ya kutumia muda mreful kutuma barua pepe wakiomba takwimu hizo.

Pia ameongeza kuwa, katika utekelezaji wa majukumu ya ofisi hiyo kwa mujibu wa sheria za Takwimu Sura 351 itaanza kutangaza kwenye tovuti yake viashiria vya kiuchumi kwa kipindi cha kila mwezi na kila robo mwaka kuanzia mwezi Julai 2021.

Amesema viashiria hivyo ambavyo vitaanza kusambazwa kwenye tovuti ya Ofsi ya Taifa ya Takwimu ni pamoja na uzalishaji wa umeme,uzalishaji wa saruji,idadi ya watalii wanaoingia nchini ,idadi ya watumiaji wa simu nchini na fahirisi ya uzalishaji wa vifaa vya ujenzi nchini.

"Viashiria hivi ni muhimu katika kufanya tathimini na ufuatiliaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi katika kipindi cha muda wa kila mwezi na kila robo mwaka ,"amesema. Maswola.

Post a Comment

0 Comments