UVCCM wamuibukia Mbunge wa Kawe, Askofu Gwajima kuhusu chanjo

Na Doreen Aloyce,Diramakini Blog

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa umelaani vikali kufuatia kauli za Mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima za kupinga Serikali juu chanjo ya CORONA.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM)Taifa, Keenan Kihongosi wakati alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma.

Kihongosi amesema, kutokana na kauli zake inaonyesha dhahiri kuwa ana nia mbaya na ovu juu ya Serikali na watu wake kwani yeye kuwaeleza wananchi uongo inaonyesha kuwa anataka kuangamiza jamii na sio daktari ambaye amebobea kwenye afya za watu.

Aidha, amesema kuwa kitendo hicho ni utovu wa nidhamu kwenye chama na Taifa kwa ujumla kwani dhamana ya ubunge aliyonayo ni kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, hivyo viongozi wa ngazi za juu wanapaswa kumchukulia hatua kali za kinidhamu.

"Sisi vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) tumelaani vikali kauli za Askofu Gwajima kama mbunge alipaswa kupeleka maoni yake sehemu husika ili yafanyiwe kazi na sio kuanza kutumia nafasi yake kutoa mahubiri kanisani ambayo ni ya upotoshaji jambo hilo hatukubaliani nalo kabisa,"amesema Keenan.

"Viongozi wa dini tunaomba mjielekeze kwenye mahubiri na kutoa elimu kwa jamii juu ya chanjo na namna ya kujikinga na Ugonjwa huo wa CORONA na wale viongozi wengine wenye tabia kama hizo muache mara moja kuropoka kwani suala la chanjo ni hiari ya mtu, tumekwazika sana,"amesema Keenan.

Akizungumza msimamo wao kama umoja wa Vijana CCM amesema kuwa, wako na Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu chanjo kwani nia yake ni njema kwa Taifa na wanaokinzana na Serikali wana nia mbaya .

Pia amewasihi wananchi kuwa makini na watu wanaojitokeza Kama madaktari feki Kutoa taarifa za uongo bali wajikite kuisikiliza wizara husika yenye mamlaka ya kutoa taarifa sahihi juu ya ugonjwa wa Corona.

"Sisi vijana tunasimama na Mama katika mambo ya maendeleo tumpe ushirikiano kwani ni maendeleo ya watu wote ni kwa manufaa ya umma na tunasimama kulinda heshima ya viongozi wetu wote na atakeyeenda kinyume tunamchukulia hatua, hivyo tunapinga kauli ambazo hazina tija aacheni Mara moja,"ameongeza Keenan.

Hata hivyo,amewasihi wananchi kuendelea kujikinga na ugonjwa huo kwa kuzingatia masharti ya afya sambamba na kufanya mazoezi ya mara kwa mara jambo ambalo litaimarisha miili yao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news