Afya ya Jose Chameleone yazua taharuki

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Daniella Atim ambaye ni mke wa msanii mkongwe Afrika Mashariki, Jose Chameleone amewajia juu watu waliosambaza picha za mumewe wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Nakasero nchini Uganda mwishoni mwa wiki.
Staa huyo alikimbizwa hospitali Alhamisi wiki iliyopita baada ya kudaiwa kuwa ameathiriwa na bakteria aina ya Helicobacter pylori (Campylobacter pylori) anayesababisha vidonda vya tumbo.

Baada ya kupatiwa matibabu saa chache baadae aliruhusiwa lakini Ijumaa alizidiwa na kurejeshwa tena hospitali ambako alilazwa.

Baada ya taarifa za kuugua kwake kusambaa sambamba na picha akiwa amelazwa, baadhi ya vyombo vya habari vilidai msanii huyo anasumbuliwa na maradhi ya figo kutokana na matumizi ya pombe kali.

Hata hivyo, mkewe alijibu tuhuma hizo na kudaiwa kuwa mumewe alikuwa ameathiriwa na bakteria.

Pia alieleza kukasirishwa na kitendo cha watu kusambaza picha za mumewe na kudai hali hiyo itaweza kuleta mshtuko kwa wanawe watano.

Kwa nini Helicobacter pylori (Campylobacter pylori)?

Baadhi ya tafiti zinaonyesha kuwa, asilimia kubwa ya watu duniani wana vimelea vya bakiteria huyo katika utumbo.

iMongoni mwao, karibu asilimia 80 huwa hawaoneshi dalili yeyote ya kuugua ugonjwa wa vidonda vya tumbo.

Hii aina ya vimelea vya bakteria husababisha karibu asilimia 60 ya vidonda vinavyotokea kwenye tumbo na zaidi ya asilimia 90 ya duodenal ulcers.

Hali hii husababishwa zaidi na kushindwa kwa mfumo wa kinga mwilini kuwaua na kuwaondoa kabisa vimelea hawa ndani ya mwili.

Matokeo ya kushindwa huku husababisha kuwepo kwa maambukizi ya kudumu katika kuta za tumbo (chronic active gastritis), maambukizi ambayo huharibu mfumo na uwezo wa kuta za tumbo kutunza homoni au kichocheo aina ya Gastrin, ambacho ni muhimu katika kuhakikisha mazingira ya tumbo yanakuwa na kiwango salama cha tindikali.

Kwa kawaida, kazi ya gastrin ni kuchochea utolewaji wa tindikali (gastric acid) kutoka kwenye seli za ukuta wa tumbo zijulikanazo kama Parietal cells. 

Iwapo bakteria hawa watashambulia na kuharibu ukuta wa tumbo, mfumo wa gastrin pia uharibika, na hivyo kusababisha gastrin kuzalishwa kwa wingi hali ambayo pia huchochea uzalishaji wa gastric acid kwa wingi. 

Matokeo ya kuzalishwa kwa wingi kwa tindikali hii hupelekea kuchubuka kwa ukuta wa tumbo na hivyo kusababisha vidonda vya tumbo.

Wataalamu wanaeleza kuwa,unywaji wa pombe pekee hausababishi vidonda vya tumbo.

Hata hivyo, unywaji wa pombe sambamba na maambukizi ya vimelea vya Helicobacter pylori huongeza madhara ya ugonjwa wa vidonda vya tumbo ambalo ni tatizo linalodaiwa kumsumbua staa huyo wa Afrika Mashariki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news