BILIONI 35/- KUJENGA UWANJA WA NDEGE MUSOMA

Na Siti Said-WUU

Serikali imesema inatarajia kutumia kiasi cha Shilingi Bilioni 35 kuboresha uwanja wa ndege wa Musoma, mkoani Mara, kwa kuweka lami na kuongeza urefu wa uwanja huo ili kuruhusu ndege kubwa na ndogo kuweza kutua.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, akitoa maelekezo kwa wafanyakazi wa Kampuni ya kikandarasi ya Beijing kutoka nchini China, alipofika uwanja wa ndege wa Musoma, mkoani Mara, kukagua maandalizi ya maboresho ya uwanja huo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, alipofika uwanjani hapo kukagua maandalizi ya ujenzi huo.

“Tunatarajia ujenzi huu utagharimu shilingi Bilioni 35 ambapo utahusisha upanuzi wa uwanja huu na pia uwekaji wa lami, naamini kazi hizi zikikamilika uwanja huu utakuwa wa kisasa zaidi”, amesema Chamuriho.

Aidha,Waziri Chamuriho, ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo na vitongoji vyake ambao watapata ajira katika mradi huo, kuhakikisha kuwa wanatumia vizuri fursa watakayoipata kwa kuwa waaminifu na kufanya kazi kwa bidii.
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Mara, Mhandisi, Ngaile Mlima (katikati), akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho (kulia), alipofika uwanja wa ndege wa Musoma, mkoani Mara, kukagua maandalizi ya maboresho ya uwanja huo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt. Khalfani Haule, amesema kuwa mradi huo ukikamilika utarahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa Musoma na pia kuchochea biashara ya utalii kupitia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo ipo mkoani humo.

Ameongeza kuwa Uongozi wa Wilaya tayari umejipanga kwa kuupokea mradi huo na wameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Mkandarasi huyo kwa kumpatia eneo la kuchimba mchanga na kokoto za ujenzi.
Muonekano wa baadhi ya vifaa vya ujenzi vya mkandarasi Beijing kutoka nchini China ambavyo vinatarajiwa kutumika katika kazi za maboresho ya uwanja wa ndege wa Musoma, mkoani Mara vikiwa vimeshawasili katika eneo la mradi. (PICHA NA WUU).

Naye, Meneja wa Uwanja wa ndege wa Musoma, Mohammed Bakari, amesema kuwa uwanja huo utajengwa na Kampuni ya kikandarasi ya Beijing kutoka China ambapo itatumia miezi 20 kuanzia mwezi Aprili, 2021na kutarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2022.

Amefafanua kuwa Mkandarasi huyo tayari ameshawasilisha vifaa vyake katika eneo la mradi kwa ajili ya kuanza rasmi ujenzi huo, na kusisitiza kuwa ujenzi wa uwanja huo unasimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Mara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news