Dkt.Shaku atoa wito kwa madiwani Musoma kuhusu chanjo ya UVIKO-19

Na Fresha Kinasa, Diramakini Blog

MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara wameombwa kuwa mabalozi katika uhamasishaji wa chanjo ya UVIKO-19 katika maeneo yao ili wananchi wajitokeze kwa wingi kuchanja.
Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Musoma, Dkt.Magreth Shaku akitoa taarifa ya Ugonjwa wa UVIKO-19 katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo ambalo limefanyika Agosti 18,2021 katika ukumbi wa manispaa hiyo.(Picha na Diramakini Blog).

Kauli hiyo imetolewa leo na Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Musoma, Dkt.Magreth Shaku wakati akitoa taarifa ya ugonjwa huo na mikakati ya kujikinga kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Musoma.

Dkt. Shaku amesema kuwa, madiwani wana jukumu la kushiriki kikamilifu kutoa hamasa kwa wananchi katika kata zao kusudi wananchi wajitokeze kwa wingi kuchanja, ambapo alisema chanjo ni salama, bure na haina athari. hivyo wananchi kuanzia miaka 18 na kuendelea wanapaswa kujitokeza kwenda kuchanja katika vituo vilivyoainishwa kikiwemo Kituo cha Afya cha Bweri, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Musoma pamoja na Hospitali ya Nyasho.

Akizungumzia mikakati ya halmashauri hiyo katika kukabiliana na ugonjwa huo, Dkt.Shaku alisema, mikakati mbalimbali imeendelea kufanyika ikiwemo kutoa elimu kwa wananchi namna ya kujikinga katika taasisi za mbalimbali, maeneo ya mikusanyiko, pamoja na kuhamasisha wananchi kuendelea kuvaa barakoa sanjari na kutumia vitakasa mikono mara kwa mara.
Mikakati mingine alisema ni pamoja na kuhakikisha ndoo za maji tiririka na sabuni kwa ajili ya kunawa mikono, kufuatilia na kuwachunguza wageni wote wanaoingia kupitia uwanja wa ndege wa Musoma pamoja na kuweka mfumo sahihi wa kutoa taarifa ofisi ya Mganga Mkuu wa Manispaa kuhusu mtu anayehisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huo.

"Pia, kutoa chanjo ya kujikinga na ugonjwa wa homa kali ya mapafu katika vituo vitatu vya Manispaa ya Musoma kwa watu wote walio tayari wenye umri kuanzia miaka 18 katika vituo vya Nyasho, Bweri na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara sambamba na kuhimiza matangazo kwa njia ya kipaza sauti na mabango juu ya elimu ya UVICO-19 yamewekwa katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Musoma,"alisema Dkt.Shaku.

Aidha, Dkt. Shaku alisema zipo changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa fedha za kununulia vifaa vya kujikinga na Corona (PPE) dawa, mafuta kwa ajili ya ufuatiliaji na matangazo kwenye vyombo vya habari pamoja na upungufu wa mara kwa mara kwa mitungi ya oksijeni na oksijeni Concentratotor kwa ajili ya wagonjwa wanaolazwa wodini.

Mbali na hilo, Dkt.Shaku pia alisema upo uelewa mdogo kwa jamii kuhusu hatua za kujikinga na Corona hasa maeneo ya mikusanyiko Kama masoko, vituo vya mabasi, harusi na maeneo ya misiba.

Alisema, utatuzi wa changamoto hizo ni pamoja na kuhakikisha vifaa vya kujikinga na ugonjwa wa Covid-19 vinakuwepo katika vituo vya kutolea huduma, kuhamasisha wadau wa afya mbalimbali kuendelea kuchangia vifaa vya kujikinga, kuhakikisha kila Kituo kinakuwa na mitungi ya Oksijeni na Oksijeni Concentrator kwa ajili ya wagonjwa pamoja na kutoa elimu ya kujikinga kwa wananchi.

Diwani wa Kata ya Buhare Manispaa ya Musoma Jumbula Macraud aliomba elimu ya kujikinga na Corona itolewe mara kwa mara katika vituo vya afya,hospitalini na zahanati kwa msisitizo ili kuimarisha mapambano dhidi ya janga hilo.
Meya wa Manispaa ya Musoma, William Gumbo akizungumza wakati wa kikao cha baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa hiyo Agosti 18, 2021. Kulia kwake ni Naibu Meya Haji Mtete, kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji,Bosco Ndunguru.(Picha na Diramakini Blog).

Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Musoma, William Gumbo alisema kila mwananchi ana jukumu la kuchukua tahadhari zote na kuzingatia ushauri wa wataalam wa afya kwa kuzingatia maelekezo yote.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news