Mbisso:Tume ya Utumishi wa Umma ilianzishwa ili kufanya Utumishi wa Umma uongeze ufanisi

Na Mwandishi Maalum,PSC

Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. John Mbisso amesema kuwa Tume ni matokeo ya maboresho mbalimbali yaliyoanzishwa na Serikali kwa lengo la kuufanya Utumishi wa Umma uongeze ufanisi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. John Mbisso (kulia) akitoa ufafanuzi wakati wa Kikao cha Kazi cha Tume na Wadau kujadili Mpango Mkakati, Mkoani Morogoro kushoto ni Bw. David Pwele, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Mipango, Tathmini na Ufuatiliaji. (Picha na PSC).

Bwana Mbisso amesema haya jana Mkoani Morogoro wakati wa Kikao kazi cha Tume na wadau kujadili Mpango Mkakati wa Tume ya Utumishi wa Umma ulioandaliwa wa kipindi cha mwaka 2021/22 hadi 2025/2026.

Amesema kuwa pamoja na malengo makuu ya Sera ya Menejimenti na Ajira ya mwaka 1999, kukabiliana na changamoto mbalimbali katika Utumishi wa Umma, Sera hii ililenga pia kuunganisha Tume tofauti zilizokuwepo na kuunda Tume moja ya Utumishi wa Umma ambayo ingesimamia taratibu zote za ajira na nidhamu katika Utumishi wa Umma.

Madhumuni ya kuundwa kwa Tume ya Utumishi wa Umma ilikuwa ni kuhakikisha kuwa Utumishi unakuwa mmoja na watumishi wote wana taratibu za usimamizi, hadhi, haki na maslahi yanayofanana amesema Bwana Mbisso.
Picha ya pamoja ya Washiriki kutoka Tume ya Utumishi wa Umma na Wadau kujadili Mpango Mkakati wa Tume, Kikao kinachofanyika Mkoani Morogoro. (Picha na PSC).

“Jukumu la msingi la Tume ni kurekebu (regulate) Utumishi wa Umma nchini ili kuimarisha utawala bora na uwajibikaji kwa Viongozi na watumishi wa ngazi zote katika Utumishi wa Umma. 

Aidha, Tume inasimamia, kufuatilia na kutathmini uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu zinazosimamia Utumishi wa Umma nchini. 

"Kazi kubwa ya Tume ni kufuatilia na kusimamia uendeshaji wa shughuli za Rasilimali Watu katika Taasisi za Umma, kuhakikisha kuwa Utumishi wa Umma unaendeshwa kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu, pamoja na kupokea na kushughulikia rufaa za watumishi wa umma kupinga maamuzi yaliyotolewa na Mamlaka zao za Nidhamu," amefafanua Bw. Mbisso.

Bw. Mbisso alihitimisha kwa kusema kuwa, Tume itaendelea kutekeleza majukumu yake iliyonayo chini ya Sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298 (marejeo ya mwaka 2019) katika kuhakikisha kuwa Waajiri, Mamlaka za Ajira na Mamlaka za Nidhamu katika Utumishi wa Umma zinatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayotolewa ili azma ya Serikali ya kuwa na Utumishi wa Umma uliotukuka iweze kufikiwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news