Mbunge Askofu Gwajima 'alipuka' saa chache kabla ya kutua mbele ya Bunge

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

SIKU moja baada ya Bunge kutoa taarifa kwa Mbunge wa Kawe (CCM), Josephat Gwajima pamoja na Mbunge wa Ukonga (CCM), Jerry Silaa ya kuitwa mbele ya Kamati ya Maadili na Madaraka ya Bunge ili kujibu tuhuma mbalimbali ikiwemo kusema uongo na kushusha hadhi na heshima ya Bunge, Mheshimiwa Gwajima ambaye pia ni Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima ameshikilia msimamo wake huku akiendelea kutoa maneno mapya.
Hivi karibuni, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima, aliliagiza Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kumtafuta na kumkamata popote alipo mbunge wa Kawe Askofu Josephat Gwajima, kwa kueneza uvumi kuhusu chanjo ya UVIKO-19.

Akofu Gwajma akihubiri katika Kanisa la Ufufuo na Uzima lililopo mkoani Dar es Salaam leo Agosti 22, 2021 amebainisha kuwa, msimamo wake upo pale pale.

"Sisi imani yetu ni kwamba kwa kupigwa kwake Yesu sisi tumepona na kwa imani yetu sisi hatuchanjwi, sasa tisha tisha ya nini? Mbona tumeweka bayana, wiki iliyopita nilisema nafunga mjadala sisi hatujaona tafiti ya kutosha kufanya miili yetu ichanjwe.

"Nini kinachokwamisha? Kinachokwamisha ni kwamba waziri yule yule mkwe wetu, tuna bahati mbaya sana ndani ya ukoo wa Gwajima. Mzee Gwajima pole sana, tumepata matatizo ya mkwe wako, huyu sasa tutafanyaje, hii oa oa ya wadogo zetu imetuletea tabu kwenye familia,"amesema Askofu Josephat Gwajima.


"Kama Dorothy Gwajima na Dkt. Mollel wana akili nzuri, wanatakiwa kujiuzulu ili wampe nafasi Rais kuweka watu wengine kufanya kazi, na ukweli ni kwamba hawa hawakuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, aliwakuta tu. Askofu

"Kiongozi wa serikali akianza kuchokonoa vitu vya kanisani ataharibikiwa kabla ya wakati. Serikali haiwezi kutupangia jinsi ya kuhubiri, huwezi kutukamata kwa kuwa tunahubiri pombe au sigara ni dhambi kisa vinaingizia watu mapato, tumekataa kuchanjwa na hatutachanjwa,"ameeleza.

Aidha, taarifa iliyotolewa Agosti 21, 2021 na Kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Bunge, imeeleza wabunge hao wameitwa mbele ya Kamati hiyo kwa agizo la Spika wa Bunge Job Ndugai.

“Wanatakiwa kufika mbele ya Kamati hiyo kwa mujibu wa kanuni ya 4 (1) (a) na (b) ya nyongeza ya nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge, toleo la Juni 2020 ambayo inaipa mamlaka Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuchunguza mambo yanayohusu maadili ya wabunge yanayopelekwa na Spika” imesema taarifa hiyo.

Mbunge Gwajima anatakiwa kufika kwenye Kamati hiyo siku ya Jumatatu Agosti 23, 2021 saa saba mchana na Mbunge Silaa anatakiwa kufika Jumanne Agosti 24 saa saba kamili mchana.

“Yeyote kati ya waliotajwa hatafika mbele ya Kamati kwa siku na muda uliotajwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake kwa mujibu wa kifungu cha 17 na 34 (1) (a) cha sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge, Sura ya 296, Toleo la mwaka 2020” imesema taarifa hiyo

 

MUHIMU

UNATAMANI DIRAMAKINI BLOG TUWE HEWANI SAA 24 KUKUPA HABARI ZA KINA KILA DAKIKA, TUNAOMBA UTUUNGE MKONO KWA KUCHANGIA GHARAMA ZA MAWASILIANO NA INTANETI KWA WAANDISHI WETU POPOTE WALIPO NDANI NA NJE YA TANZANIA; TUNAPOKEA MCHANGO WAKO KUPITIA 0719254464 (Tigo Pesa-Godfrey Nnko) AU UKIHITAJI NAMBA YA BENKI TUJULISHE. MUNGU AKUBARIKI SANA KWA SAPOTI YAKO. ASANTE

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news