MBUNGE SAGINI AWEZESHA UNDP KUWANOA MADIWANI, WATAALAMU BUTIAMA

Na Fresha Kinasa Diramakini Blog

MBUNGE wa Jimbo la Butiama Mkoa wa Mara Jumanne Sagini, ameratibu na kufanikisha mafunzo kwa Madiwani na Wataalamu wa Halamshauri ya wilaya hiyo chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ili kuwajengea uwezo wa kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo ambazo zitachochea ukuaji wa uchumi kupitia rasilimali zilizoko katika maeneo yao na wilaya kwa ujumla.
Mafunzo hayo yamefanyika kwa siku mbili, ambapo yamelenga kuwapa uelewa mpana wa namna ya kushiriki kikamilifu kutekeleza majukumu yao katika kusukuma mbele ajenda ya maendeleo ya wilaya hiyo kupitia fursa mbalimbali ikiwemo ufugaji, kilimo waweze kuwajibika ipasavyo kuleta Maendeleo kwa Wananchi.

"Baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2020, hakujatokea mafunzo mahususi ya kuwawezesha madiwani kutekeleza majukumu yao. Hii siyo mara ya kwanza niliongea na Uongozi wa UNDP mara ya kwanza kabisa tukifanya mafunzo ambapo yalilenga kuwakumbusha majukumu yao mara tu baada ya uchaguzi huo.

"Niliongea na UNDP tukakubaliana kwamba wakati mwingi mabaraza haya yanapoundwa watu hawajui namna gani wanapaswa kutekeleza majukumu yao kunakuwa na migongano. Ombi hili lilikubalika tukafanya mafunzo kwa madiwani wa Butiama tukawaunganisha na Madiwani wa Bunda kuwajengea uelewa wa majukumu yao. Baada ya miezi sita, tumeona tunazo changamoto nyingi zinazohitaji uelewa mpana wa madiwani na wataalamu wao kusukuma ajenda ya maendeleo ya Butiama niwashukuru UNDP kuwezesha mafunzo haya tena," amesema Mhe. Sagini.
Mhe. Sagini amesema Wilaya ya Butiama ambayo ilitoa Mwasisi wa Taifa la Tanzania licha ya kuwa na rasilimali nyingi, lakini bado kiwango cha uchumi wa wananchi uko chini watu bado ni masikini, lakini wanazo rasilimali nyingi. 

Hivyo kupitia wataalamu wa UNDP na wataalamu walionao aliona wasaidie kutoa mafunzo kwa Madiwani na Wataalamu wa Halmashauri kusudi rasilimali zilizopo wazisimamie zilete mapinduzi chanya ya kimaendeleo.

Aliongeza kuwa, kupitia mafunzo hayo kila mmoja akiwajibika kikamilifu maendeleo yatapatikana kwa kasi kwa wananchi kuanzia ngazi ya za vijiji, kata na Wilaya kwani Wananchi watafuga mifugo yao kwa njia ya kisasa, kulima kilimo cha kisasa na kupata tija kutoka katika mazao mbalimbali wanayolima na sambamba na kutojihusisha kwenye kilimo cha mazao ya chakula pekee Bali hata mazao ya mifugo Kutokana na Wikaya hiyo kuwa na Wakulima wengi na hivyo kuuza mazao yao kwa bei ndogo.

"Ng'ombe wetu wakiboreshwa watazalisha maziwa kwa wingi, Watoto watasoma bila shida na wananchi wataondokana na hali ngumu ya maisha. 

"Haiwezekani mtu uuze ng'ombe watatu ndo upate shilingi milioni moja, kumbe kuna uwezekanao ng'ombe akibooreshwa anaweza kutoa hata lita 10 za maziwa kwa siku. Wananchi wataondoka na adha ya kupata shida kupeleka Watoto shule hasa za kidato cha tano kwani baadhi yao wanapofaulu wazazi hupata shida kutafuta nauli wakikosa Mwanafunzi hubakia nyumbani," amesema Sagini.

Ameongeza kuwa, halmashauri hiyo imeanzisha kampuni kwa lengo la kuongeza mapato itakayofahamika kwa jina la NTUZU COMPANY LTD ambapo itakuwa na miradi mbalimbali inayotekelezwa na kampuni itapata gawio lake hatua ambayo itawezesha Halmashauri kuhudumia Wananchi. Huku akisisitiza elimu hiyo ifikishwe hadi ngazi za chini kuwafikia Wananchi na vijana kusudi washiriki kujenga uchumi imara kwa maendelo yao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news