Mgongolwa asisitiza umuhimu wa chanjo, atoa angalizo kwa viongozi wa dini

Na Mwandishi Wetu, Iringa

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Iringa Mjini, Joseph Mgongolwa amewashauri viongozi wa dini kuendelea kuwa mstari wa mbele kuwahubiria Watanzania habari njema, kuwaombea na kuwaunganisha pamoja ikiwemo kuacha kabisa kutumia umaarufu wao kupotosha mambo yanayohusiana na utekelezaji wa mipango ya Serikali kwa maslahi mapana ya Taifa na watu wake.

"Viongozi wa dini wana dhamana kubwa sana, wamekuwa kiungo muhimu katika kutuunganisha na kutuokoa katika maovu mengi ambayo pengine tungeendelea kuyatenda kama binadamu tungejikuta katika hatari mbaya siku za usoni. Hivyo basi, imani yetu kwao ni kubwa mno, ndiyo maana wakisema jambo tunaliamini na kulifuatilia kwa umakini maana wao ni wapakwa mafuta wa Mungu.

"Kwa msingi huo basi, wengi wamekuwa na ushawishi mkubwa katika jamii, lakini wakati mwingine aidha kwa kufahamu au kutofahamu wamekuwa wakitumia nafasi zao vibaya kuyatafsri mambo yanayohusu Serikali kinyume, hivyo kuleta mkanganyiko hususani kuhusiana na msimamo wa Serikali kuleta chanjo ili kuhakikisha watu wake wanajikinga dhidi ya virusi vya Corona, miongoni mwao, hao viongozi wamekuwa wakipotosha, lakini kwa kuwa Watanzania wamepewa upeo mpana wa kupambanua mambo wamekuwa wakiyazingatia yaliyo muhimu na yasiyo ya msingi wanayapa kisogo;

Mgongolwa ameyasema hayo mjini hapa wakati akizungumzia kuhusiana na umuhimu wa Watanzania kupata chanjo dhidi ya virusi vya Corona ambayo imekuwa ikitolewa hapa nchini kwa sasa.

Amesema kuwa,licha ya chanjo kuwa hiyari ya mtu, lakini ni muhimu kila Mtanzania kuhakikisha anaipata ili kujikinga dhidi ya virusi vya Corona ambavyo vinasambaa kwa kasi duniani kote.

"Msikubali kupotosha, eti Wazungu wametuletea chanjo ili kutuua, hapa hawawezi kutufanyia hivyo, maana kama wangetaka tufe basi wangefanya hivyo toka zamani, mfano mdogo tu, watu wengi sana wanatumia kondomu kujikinga dhidi ya virusi vya Ukimwi, na zimekuwa zikiwasaidia, hivi tujiulize kama hao Wazungu waliozitengeneza hizo kondomu walitaka kutuua si wangeamua tu kuweka mtego na hizo kondomu zisiwe na matokeo kabisa.

"Vivyo hivyo, watoto na hata wengi wetu tumepata chanjo nyingi sana na zinaendelea kutolewa mara kwa mara. Chanjo zote hizo zimetoka kwa Wazungu, leo hii tunasema hii ya Corona ndiyo imeundwa mahususi kutuua? Hii si kweli, dhana hizo ni potofu, Watanzania twendeni tukachanje kwa ajili ya kujiweka salama, Taifa letu linatutegemea, watoto wetu na ndugu zetu wanatutegemea, hivyo tukipoteza maisha kwa Corona, itakuwa si sawa. Chanjo ni muhimu kwa kila mmoja wetu,"amesema Mgongolwa.

Mgongolwa amesema kuwa,pamoja na kuwepo kwa chanjo hiyo lakini ni lazima wananchi waendelee kuchukua tahadhari kwa kufuata maelekezo kutoka kwa wataalamu wa afya.

Amesema,moja ya maelekezo hayo ni kunawa mikono kwa maji tiririka,kuvaa barakoa, kutumia vitakasa mikono pamoja na kuzingatia umbali wa mtu na mtu.

Mgongolwa alitoa wito huo ikiwa Julai 28, 2021 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiongozana na viongozi mbalimbali waandamizi wa Serikali walizindua rasmi chanjo ya corona nchini.

Uzinduzi huo ulifanyika Ikulu jijini Dar es Salaam ambapo Rais Samia Suluhu Hassan alisema, chanjo hiyo ni salama na asingekuwa tayari kuhatarisha maisha yake kwa kuchanjwa chanjo ya Corona kama ingekuwa si salama.

Hatua hiyo ilikuja baada ya Tanzania kupokea zaidi ya dozi milioni 1.05 za chanjo aina ya Johnson & Johnson zilizotolewa na Marekani kupitia mpango wa upatikanaji wa chanjo wa Covax.

Katika mpango huo, wapo baadhi ya watu wanaopingana na harakati hizo wakieleza chanjo hizo sio salama na wapo wanaounga mkono, lakini kiongozi huyo mkuu wa nchi amewaondoa hofu wananchi kuhusiana na hilo.

Rais Samia alisema, yeye ni mama wa watoto wanne, ni bibi wa wajukuu kadhaa wanaompenda sana na yeye kuwapenda, ni mke pia lakini mbali ya yote ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi wa nchi hii.

“Nategemewa kama mama, kama bibi, kama Rais, kama Amiri Jeshi Mkuu, nisingejitoa mwenyewe nikajipeleka kwenye kifo, nikajipeleka kwenye hatari nikijua kwamba nina majukumu yote haya yananitegemea .

“Lakini nimetoka kuonyesha umma wanaonifuata nyuma nikijua kama Rais ni mchungaji na nina watu wengi nyuma nawachunga na wananitazama mimi hivyo nisingetoka kujihatarisha,”alisema Rais Samia.

Rais alibainisha kuwa, amekubali kwa hiari yake kuchanja akijua kwamba ndani ya mwili wake ana chanjo kadhaa ambazo ameishi nazo kwa miaka 61 sasa kwani tangu amezaliwa kuna chanjo mbalimbali wamekuwa wakichanjwa, mbali na zingine wanazochanjwa njiani wakiwa wanasafiri ikiwemo ya homa ya manjano.

Hivyo kwake haoni hatari iliyoko na baada ya wanasayansi kujirishisha hivyo yupo tayari kuchanja na kuwa kuwaomba Watanzania wapuuze yote wanayoyasikia kuhusiana na chanjo hiyo.

“Kwa wale ambao koo zao hazijaguswa, hawajapata madhara ya maradhi haya wanaweza kusema wanavyotaka. Lakini nenda leo Moshi, nenda Arusha ,nenda Kagera, hata Dar es Salaam uonane na zile koo ambazo zimeshaguswa na haya maradhi wana maneno ya kukuambia na kama wangeweza leo wote wangekuwa hapa kutaka kuchanja kuepukana na ile hasara walioipata,”alisema Rais Samia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news