Moto uliokuwa ukisafishia shamba wateketeza nyumba 19

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Mwananchi mmoja ambaye alikuwa anasafisha eneo lake katika Kitongoji cha Shaurimoyo katika Kijiji cha Nyamwage kilichopo Kata ya Mbwara wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani amesababisha kilio kikubwa kwa kaya 19, baada ya nyumba zao kuteketea kwa moto.


Mwananchi huyo akiwa anasafisha eneo lake kwa moto ndipo ulimshinda na kuteketeza nyumba zipatazo 19 za wananchi pamoja na mali na samani zilizokuwepo ndani ya nyumba hizo.

Katika tukio hilo la simanzi ambalo limetokea usiku wa kuamkia leo Agosti 30, 2021 hakuna mtu aliyejeruhiwa.

Aboubakar Kunenge ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani pamoja na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Rufiji wamefika kwenye tukio hilo huku wakitoa pole kwa familia mbalimbali.
Mheshimiwa Kunenge amesema, amefika katika eneo hilo ili kuona athari iliyotokea na jitihada ambazo uongozi wa wilaya wamezichukua kuhakikisha wananchi wanakuwa salama.

Pia Kunenge alitoa pole kwa serikali ya wilaya pamoja na wananchi waliokutwa na madhila hayo na kuwapongeza wakazi wa maeneo ya karibu kuweza kuwapatia hifadhi wananchi wenzao waliokutwa na ajali hiyo.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Kunenge ameuagiza uongozi wa wilaya hiyo kufanya haraka kujua tathimini ya athari iliyopatikana ili kuweza kuwasaidia waliopata ajali hiyo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele ameeleza kuwa, wao kama wilaya wamechukua hatua za haraka baada ya kutokea tukio hilo ili kuhakikisha wananchi hawateseki.

Post a Comment

0 Comments