Mradi wa Graphite kuanza uzalishaji 2022-Majaliwa

 Na Steven Nyamiti,WM- Ruangwa

Imeelezwa kuwa, Kampuni ya Lindi Jumbo Limited iliyotafiti na kuamua kuwekeza kwenye uchimbaji wa madini ya Kinywe ( Graphite) katika Mkoa wa Lindi wilayani Ruangwa inatarajia kuanza rasmi uzalishaji mwezi Agosti, 2022.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akikagua eneo la utekelezaji wa uchimbaji wa madini ya Kinywe (Graphite) katika kijiji cha Matambarale Wilaya ya Ruangwa Mkoa wa Lindi. (Picha na Steven Nyamiti-WM).

Hayo yameelezwa leo Agosti 20, 2021 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa alipotembelea Mgodi wa Kati wa Kampuni ya Lindi Jumbo Ltd katika Kijiji cha Matambarale wilayani Ruangwa kutakakojengwa mgodi huo.

Amesema, uzalishaji wa madini ya Graphite utakuwa mradi mkubwa wa kwanza kwa uzalishaji hapa nchini, mradi ambao utatoa fursa mbalimbali kwa wananchi wa Ruangwa na Mkoa wa Lindi.

"Mgodi wa Kati wa Graphite unaomilikiwa na Kampuni ya Lindi Jumbo Ltd utatoa ajira kwa wananchi zisizopungua 200 katika kipindi cha ujenzi kuanzia mafundi, madereva, wapishi, usafi na ulinzi lakini uzalishaji ukianza rasmi mgodi utatoa ajira 100 kwa kada mbalimbali mgodi ukikamilika," amesema Mhe. Majaliwa.

Pia, amesisitiza kuwa mgodi utalipa kodi mbambali zitokanazo na shughuli za mgodi ambazo zitalipwa serikalini, kusaidia shughuli za maendeleo katika Kijiji cha Matambarale na Wilaya ya Ruangwa.

Ameongeza kuwa, katika Mgodi wa Lindi Jumbo yatachimbwa na kuuzwa madini ya Graphite yenye ubora duniani.

Waziri Mkuu amesema, kulingana na bei ya soko la Kinywe duniani, "tunategemea kuuza kuanzia Dola za Marekani 1,000 kwa tani hadi dola 1,800 kwa tani,"amesema.

Aidha, Waziri Mkuu ameipongeza Kampuni ya Lindi Jumbo kwa kuwezesha kulipa fidia kwa watu wote hususan mali zilizokuwa kwenye eneo la mradi wa Kampuni ya Lindi Jumbo (Compensation).
Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa alipotembelea eneo kutakakojengwa mgodi wa uchimbaji wa madini ya Kinywe na Kampuni ya Lindi Jumbo Ltd. (Picha na Steven Nyamiti-WM).

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuwekeza fedha nyingi katika miradi mikubwa hususan kwenye Sekta ya Madini.

Amesema, CRDB ndio benki ya kwanza kuingiza pesa ambapo watakwenda kupata faida kubwa kupitia mradi huo.

Akizungumzia kuhusu kulipa fidia kwa wananchi, Prof. Manya amemueleza Waziri Mkuu kuwa Kampuni ya Lindi Jumbo wamekamilisha kulipa fidia na kusisitiza kampuni zingine zihakikishe zinalipa fidia kwa wananchi ili kuondoa migogoro na wanachi ya mara kwa mara.

Naye Meneja Mkuu wa Kampuni ya Lindi Jumbo, Paul Shauri amemueleza Waziri Mkuu kuwa wanategemea kufanya uzalishaji wa madini ya Kinywe katika kipindi cha miaka 24.
Meneja wa Kampuni ya Lindi Jumbo Ltd, Paul Shauri akieleza taarifa fupi ya maendeleo ya uanzishwaji wa mgodi wa madini ya kinywe kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa. (Picha na Steven Nyamiti-WM).

Aidha, amesema Kampuni ya Lindi Jumbo imefanikiwa kulipa fidia jumla ya shilingi bilioni nne kwa wananchi wanaozunguka eneo la mgodi huo.

Kuhusu huduma za kijamii, Meneja Shauri amesema Lindi Jumbo Ltd imechangia mabati 100 na mifuko ya saruji 100 wakati wa ujenzi wa shule ya Sekondari ya Majaliwa na wamefanya matengenezo ya pampu ya maji ya mkono Matambarale Kaskazini.

Kuanza kwa mradi huu wa Madini ya Kinywe kutawezesha Serikali kupata hisa huru asilimia 16 kwa mujibu wa Sheria ya Madini Sura ya 123.

Waziri Mkuu anaendelea na ziara ya kukagua shughuli za maendeleo katika Jimbo la Ruangwa ambapo amezungumza na wachimbaji wadogo na kutembelea eneo la mradi wa madini ya Graphite mkoani Lindi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news