Ngano, nyama,viazi vyachangia mfumuko wa bei nchini

Na Doreen Aloyce, Diramakini Blog

Kaimu Mkurugenzi wa Sensa za Watu na Makazi, Ruth Minja amesema Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Julai 2021 umeongezeka hadi asilimia 3.8 kutoka asilimia 3.6 kwa mwaka ulioishia mwezi Juni,2021.
Takwimu hizo amezitoa leo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya Mfumuko wa Bei wa Taifa ambapo utolewa mila mwezi.

Minja amesema kuwa, kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei kwa mwaka ulioishia mwezi Julai ,2021 kumechangiwa na kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa baadhi ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula.

"Kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei kumechangiwa na baadhi ya bidhaa za vyakula ikiwemo ngano kwa asilimia 6.5, unga wa ngano kwa asilimia 6.1, nyama kwa asilimia 3.7, viazi mviringo kwa asilimia 7.9 , viazi vitamu kwa asilimia 8.4 na mihogo mibichi kwa asilimia 6.4," amesema Minja.

Pia ameongeza kuwa baadhi ya bidhaa zisozo za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei ni pamoja na nguo za wanawake kwa asilimia 6.4 ,viatu vya wanaume kwa asilimia 7.1, viatu vya watoto kwa asilimia 6.4 na kodi ya pango kwa asilimia 4.9.

Vile vile amebinisha kuwa Mfumuko wa Bei wa Bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Julai ,2021 umeongezeka hadi asilimia 5.1 kutoka asilimia 4.7 kwa mwaka ulioishia mwezi Juni ,2021.

Akizungumzia hali ya Mfumuko wa Bei kwa Baadhi ya nchi za Afrika Mashariki kwa mwaka ulioishia mwezi Julai 2021,kwa nchini Kenya umeongezeka hadi asilimia 6.44 kutoka asilimia 6.32 kwa mwaka ulioishia mwezi Juni ,2021.

Aidha, amesema kuwa kwa upande wa nchini Uganda , Mfumuko wa Bei kwa mwaka ulioishia mwezi Julai ,2021 umeongezeka pia hadi asilimia 2.1 kutoka asilimia 2.0 kwa mwaka ulioishia mwezi Juni ,2021.

Post a Comment

0 Comments