RC Makongoro:Eti mwaka mzima, Wabunge acheni kona kama zote, alikeni wageni bungeni

Na Mary Margwe, Manyara

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Makongoro Nyerere amesema ni kitendo cha aibu kwa wabunge kukaa bungeni mwaka mzima bila kuwa na mgeni hata mmoja aliyemwalika bungeni.
Ameyasema hayo mbele ya Mbunge wa jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, hiyo, Dkt. Suleiman Serera, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Baraka Kanunga, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM ) Awadhi Omary, Katibu wa CCM Wilaya hiyo, Ally Kidunda alipokuwa kwenye majumuisho ya ziara yake ya siku nne wilayani Simanjiro mkoani humo.

Makongoro amesema wapo baadhi ya wabunge wamekuwa wakiishia kuwaangalia tu wabunge wenzao wakipeleka wageni bungeni huku wao wakiishia kuwaangalia macho tu, hivyo ni vema wabunge wakaangalia namna hata ya kusaidiana kuchanga pesa na madiwani ili mradi tu walau madiwani ama baadhi wa wananchi ama makundi muhimu waweze kuwatembelea wabunge wao ili kujifunza mambo mbalimbali ya huko bungeni.

"Unakuta mwaka mzima unaisha au miaka miwili Mbunge hajaalika bungeni mgeni hata mmoja, hakika hii ni aibu tena ni aibu kubwa sana wewe ukiwa kama mwakilishi wa wananchi ni wajibu wako kuwaalika baadhi ya wananchi ama madiwani walau mbunge ahakikishe mwaka usiishe bila kuwa na mgeni jamani ni aibu narudia tena ni aibu kubwa," alisema Makongoro mbele ya Mbunge wa Jimbo la Simanjiro,Christopher Ole Sendeka.

Aidha, alisema huenda wabunge wanashindwa kuwaalika kutokana na kuogopa gharama za kuwahudumia pindi wanapokuwa na wageni huko bungeni, basi sio vibaya madiwani ama baadhi ya wananchi wakashirikishwa mapema ili waweze kuchanga fedha kwa ajili ya kupunguza gharama mbalimbali badala ya kumuachia gharama zote mbunge.

"Na nyie ndio maana wabunge wanaogopa kuwapeleka bungeni, mnataka kila kitu agharamie Mbunge ataweza wapi gharama za kula yeye, kulala aangaikie yeye, usafiri wa kwenda na kurudi agharamie yeye, jamani gharama hizo ni kubwa sana, hivyo changishaneni pesa ili kumpa unafuu mbunge,maana kuna wageni wengine wanataka hadi kulipwa posho na mbunge jamani badilikeni, ndio maana unakuta mbunge akikuona tu anakupiga chenga kama zote,"alisema Makongoro.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Msitu wa Tembo, Kaleya Melita Mollel alisema yeye kama mwakilishi wa wananchi wa kata hiyo yuko tayari kuchangia ili kwenda bungeni kwani kule kuna kujifunza mengi ya kuweza kuwaletea wananchi wa kata yake ya Msitu wa Tembo.

Aidha, Mollel alisema Mbunge Sendeka ni Mbunge mwenye utu kwa jamii, hivyo iwapo atakua tayari tu kupokea wageni wao kama madiwani wako tayari kuchanga ili kuhakikisha wanakwenda kutembelea bunge, badala ya kumuachia gharama zote Mbunge.

" Mbunge wetu Christopher Ole Sendeka ni Mbunge wa aina yake, hivyo hashindwi kutualika sisi kwenda bungeni, isipokua kubwa ni kupata mwaliko mengine yote tutashirikiana kugharamia, hivyo yeye mheshimiwa mbunge wetu iwapo atakua tayari atupe tu mwaliko sisi tutajitolea mengine," alisema Mollel.

Hata hivyo, diwani wa Kata ya Mirerani, Salome Mnyawi pamoja na Diwani wa viti maalumu Tarafa ya Moipo, Paulina Makeseni, diwani wa viti maalum tarafa ya Naberera, Bahati Mosses, Diwani wa viti maalum tarafa ya Msitu wa Tembo, Neema Isaya Sinjore, diwani Mwanjaa Jacob, na diwani Namnyaki Edward wamesema wao kwa upande wao wako tayari kuchangia juu ya hilo isipokuwa wanasubiria mualiko toka kwa mbunge wao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news