Serikali yaziagiza wizara zote zenye sera za muda mrefu kuzifanyia mapitio

Na Doreen Aloyce, Diramakini Blog

WAZIRI wa Nchi,Ofsi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge, Kazi,Ajira,Vijana na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama amezitaka wizara zote nchini zenye sera za muda mrefu kuhakikisha wanazifanyia mapitio na kuandaa taarifa ya utekelezaji wake kwa kuziwekea mkataba na muda ili kuendana na mazingira ya sasa.
Mhagama ameyasema hayo jijini Dodoma wakati alipokuwa akizindua mfumo wa kielektroniki wa uratibu na ufuatiliaji wa shughuli za Serikali (Dashboard).

Amesema, utekelezaji huo wa mapitio ya sera utaongeza hali ya uwajibikaji ikiwa ni pamoja na kuisaidia serikali katika uratibu wa shughuli zote kwa njia ya utendaji na upokeaji wa taarifa sahihi ,kwa wakati sahihi katika sekta zote nchini.

Pamoja na hayo amesema, kupitia mfumo huo wa kielekroniki shughuli za Serikali zitafanyika na kuratibiwa kwa weledi hali itakayochochea maendeleo kwa kiasi kikubwa.

"Niwaombe watendaji wote wa serikali nchini kuwajibika ipasavyo katika majukumu yenu kwa kuwa mfumo huo utakwenda kubaini utekelezaji wa shughuli zote za serikali katika kila sekta, ni lazima kila mmoja ahakikishe anasimamia majukumu yake ipasavyo,"amesisitiza.

Naye Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Dkt. Faustine Ndugulile ambaye alihudhuria uzinduzi huo alisema kuwa mfumo huo ni muhimu kwa wizara yake kwa kuwa unakwenda kutimiza sera ya TEHAMA nchini na kuongeza uwajibikaji,ufanisi na uwazi kwa watumishi.

"Tunatarajia mfumo huu utarahisisha shughuli zote za kiserikali na uongeza ufanishi kwa watendaji wote katika sekta mbalimbali nchini,"amesema.

Naye, Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango, Mhe. Mhandisi Hamad Masauni ameeleza kuwa kuzinduliwa kwa mfumo huo wa Kielektroniki wa uratibu na ufuatiliaji wa shughuli za Serikali (DashBoard) utaongeza ufanisi wa kazi na uwazi.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tixon Nzunda amesema kuwa katika mfumo huo wa Kielektroniki wa uratibu na ufuatiliaji wa shughuli za Serikali (DashBoard) moduli zimeongezwa kutoka mbili (2) za awali hadi moduli tano ikiwa ni pamoja na taarifa za utekelezaji wa Ilani ya chama tawala kutoka kwenye Wizara, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news