WASANII WAASWA KUSAIDIA WAGONJWA HOSPITALI

Na Robert Kalokola, Diramakini Blog

Watanzania wanaojihusisha na fani ya maigizo nchini wameaswa kujitokeza kusaidia baadhi ya watu wanaougua Hospitalini ambao hawana huduma mbalimbali kama chakula kwasababu ya kukosa ndugu zao wa kutoa huduma hizo.

Ushauri huo umetolewa na Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Geita Charugamba Jackson wakati akizungumza na vyombo vya Habari baada ya Wasanii wa Mkoa wa Geita kutoka Kampuni ya Kapaya The Great kutoa Msaada wa Sabuni kwa Wagonjwa katika Hospitali ya mkoa wa Geita.

Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Geita Charugamba Jackson amesema kuna wagonjwa wengi wanalazwa katika Hospitali hiyo wakiwa hawana ndugu zao hivyo wanakosa baadhi ya huduma hivyo ni muhimu jamii kujitolea kuwasaidia watu hao kama wasanii kutoka mkoa wa Geita walivyo jitokeza kutoa huduma ya sabuni kwa wagonjwa.
Mkurugenzi wa Kapaya The great Maiko Kapaya ambaye ni Msanii wa Maigizo akikabidhi msaada wa sabuni kwa mgonjwa katika Hospitali ya Mkoa wa Geita (Picha na Robert Kalokola).

Amesema kuwa kutokana na watu wengi kuja Mkoa wa Geita kwenye shughuli za Uchimbaji Madini ya Dhahabu wanajikuta wanaugua na kulazwa bila kuwa na ndugu wa kuweza kuwahudumia hivyo kutegemea Hospitali ambayo inakadiliwa kupokea wagonjwa wasio na ndugu hadi 30 kwa mwezi .

Charugamba Jackson amewataka wasanii wa kuigiza kujenga tabia ya kusaidia makundi hayo kwa kutoa huduma kama kama ambavyo kundi hilo la Kapaya The Great limeweza kutoa msaada wa sabuni kwa wagonjwa katika wodi za wanaume,wanawake ,watoto wenye utapiamlo,na mama wajawazito waliojifungua na wanaosubiri kujifungua.

Muuguzi wa zamu katika Wodi ya Watoto wenye Utapiamlo Prisca Challo amewaomba wasamalia wema wanapo jitokeza kusaidia watoto hao wazingatie mahitaji yao hasa vyakula vya lishe na mahitaji kama sabuni kama ilivyotolewa na wasanii hao.
Muuguzi wa zamu katika Wodi ya watoto wenye Utapiamlo Prisca Challo akipokea msaada wa Sabuni kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Kapaya The Great Maiko Kapaya ambaye ni Muigizaji wa Mkoa wa Geita (Picha Robert Kalokola).

Mkurugenzi wa Kampuni ya Kapaya The Great Maiko Kapaya amesema kuwa yeye na waigizaji wenzake wameamua kutoa msaada wa Sabuni kwa wagonjwa katika Hospitali ya Mkoa wa Geita ili kusaidia moja ya changamoto zinazo wakabili wakati wakiwa wanatibiwa katika Hospitali hiyo.

Kapaya amesema hii siyo mara ya kwanza kwao kutoa msaada kwa jamii, na mpango wao ni kuendelea kutenga sehemu ya kipato wanacho kipata ili kukipeleka kwa jamii kama shukrani kwao kwa kutumia bidhaa zinazo tolewa na kampuni hiyo ikiwa kazi ya maigizo.

Amesema kuwa hivi karibuni Kampuni ya Kapaya The Great ilizindua filamu ambayo inaitwa Kosa la Mama ambayo maudhui yake ni kueleza umuhimu wa mwanamke katika kuandaa jamii bora hivyo kutoa msaada huo ni mwendelezo wa kutambua na kuthamini mchango wa Mwanamke katika jamii.
Waigizaji wa Mkoa wa Geita kutoka Kampuni ya Kapaya The Great Magadrena Kapela(wa kwanza kushoto),Delphina Joachim (wa kwanza kulia) na Hawa Ismail ( wa pili kulia) wakikabidhi boksi la Sabuni kwa mgonjwa katika Hospitali ya Mkoa wa Geita ( Picha na Robert Kalokola).

Maiko Kapaya amewataka wasanii kutoka makundi mengine katika jamii kujitokeza kusaidia wagonjwa katika Hospitali ikiwa ni pamoja na kujitolea damu kwa wagonjwa wanakabiliwa na uhaba wa mahitaji mbalimbali ya kijamii.

Nancy Mlemi ambaye ni muigizaji kutoka kampuni hiyo ya uigizaji amesema kuwa baada ya kutembelea wodi mbalimbali za wagonjwa katika Hospitali hiyo amebaini kuna watu wanaotibiwa katika Hospitali wakiwa hawana huduma mbalimbali japo wanapata dawa za matibabu.
Muigizaji wa Mkoa wa Geita Nancy Mlemi kutoka Kampuni ya Kapaya The great akikabidhi msaada wa Sabuni kwa mgonjwa katika Hospitali ya Mkoa wa Geita (picha na Robert Kalokola)

Nancy ameongeza kuwa wadau wajitokeze kusaidia wanawake wanaojifungua hasa kwa kutoa mahitaji muhimu kama sabuni na taulo za kike ili waweza kupata huduma bora wakati huo wa kujifungua na kurudi kwenye hali zao za kawaida.
Waigizaji wa mkoa wa Geita kutoka kampuni ya Kapaya The great wakiwa wodi ya wagonjwa katika Hospitali ya mkoa wa Geita wakitoa Msaada wa Sabuni ( picha na Robert Kalokola)

Mwezi Julai,mwaka huu Kampuni ya Kapaya The Great ilizindua filamu ya maigizo yenye jina la Kosa la Mama ilikuwa na maudhui ya kutoa elimu ya umuhimu wa mwanamke katika jamii yetu na kwa kutambua hilo wasanii hao wameendelea kutoa msaada kwa wanawake wanatibiwa katika Hospitali hiyo ya mkoa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news