Waziri Simbachawene:Ni marufuku kufanya fumanizi

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani George Simbachawene amekea tabia ya watu kukusanyana na kuvamia watu walioko kwenye faragha.

Ni kwa kisingizio cha fumanizi akisema kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na utu na watakamatwa wakigundilika popote walipo.
Mheshimiwa Simbachawene ametoa kauli hiyo Agosti 6,2021 ambapo amesema baadhi ya watu wamejijengea mazoea ya kuwavamia watu wenye uhusiano ya kimapenzi wakiwa kwenye faragha zao mahali wanapokuwa katika nyumba au hotelini.

“Tabia hii imeshamiri sasa kama ambavyo video nyingi zinarushwa rushwa mitandaoni, leo nitumie fursa hii kutoa msingi wa kisheria lakini kukemea tabia hii ambayo imeanza kuonekana inaota mizizi. Ni kinyume cha sheria kabisa kuwaingilia watu walio kwenye faragha.

“Wakati mwingine watu wanafanya hivyo kwa kisingizo kuwa wamefumania, hakuna fumanizi ambalo linaweza kupangwa na kikundi cha watu, wanawake na wanaume wanapanga kwenda kuwavamia na kuwaingilia uhuru wao waliopo faraghani, kitendo hicho ni kinyume cha sheria,”amesema.

Waziri huyo amesema, hata kama ni fumanizi litakuwa pale ambapo si jambo la kupangwa na huyo anayefumania awe na ndoa halali na cheti halali cha ndoa lakini sio kwa mtu ambaye ulikuwa naye tu.

“Huwezi kusema umemfumania hawara yako, mahusiano ya hawara ni ya kupita,”amesema.

Waziri amesema tabia hiyo inakiuka misingi ya utawala bora, heshima na utu na hasa heshima ya wanawake kwa kuwa wanaodhalilishwa sana katika hilo ni kina mama ambao walishakuwa na uhusiano na mwanaume fulani wakaachana akawa na mwingine halafu yule wa mwanzo anamfumania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news