Biashara United yawatonesha Simba SC

NA GODFREY NNKO

Simba SC ambao ni watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara wamekubali ndani ya dakika tisini kutoka suluhu dhidi ya Biashara United.

Ni kupitia kabumbu safi ambapo wanajeshi wa mpakani wanaonekana, kuimarika zaidi.

Huu ni mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ambapo mtanange huo umepigwa katika Dimba la Karume lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Musoma mkoani Mara.

Licha ya nafasi muhimu waliopata Simba SC dakika za nyongeza, baada ya kupata penati, mambo yalikwenda mrama tofauti na matarajio baada ya nahodha wao John Bocco kukosa penati hiyo.

Kwa msingi huo, Simba SC wamegawana alama moja moja na Biashara United. 

Klabu hiyo yenye maskani yake mtaa wa Msimbazi chini ya Bilionea Mohamed Dewji, wameendelea kuchechemea kwani hii ni mechi ya tatu mfululizo kwa Simba SC bila kupata bao lolote.

Ni kuanzia mechi ya Simba Day waliofungwa bao 1-0 na TP Mazembe, mechi ya Yanga ya Ngao ya Jamii ambapo Simba aliambulia kichapo cha bao 1-0 katika Dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam.

Aidha, Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, bao pekee la Cleophace Mkandala dakika ya 33 limewapa wenyeji, Dodoma Jiji FC ushindi wa 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

Pia Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, bao la Peter Mapunda dakika ya 90 na limeipa Mbeya City ushindi wa 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons.

Septemba 27,2021 wao Namungo FC wameanza vyema Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Geita Gold katika Uwanja wa Ilulu mjini Lindi.

Shiza Kichuya dakika ya 13 na Relliant Lusajo dakika ya 81 ndiyo waliowapa raha mashabiki wa Namungo FC kutoka mjini Ruangwa mkoani Lindi.

Kwa upande wa Coastal Union walilazimishwa sare ya 1-1 na Azam FC Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, wageni wakitangulia kwa bao la beki Mghana, Daniel Amoah dakika ya 49, kabla ya Hance Masoud kuwasawazishia wenyeji dakika ya 90.

Huku Mbeya Kwanza wakiibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar ambapo ni bao pekee la William Edgar dakika ya 50 Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.

Post a Comment

0 Comments