Dkt.Chamuriho ataja mafanikio lukuki Sekta ya Ujenzi, Uchukuzi

Na Siti Said-WUU

ALIYEKUWA Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho, amesema wizara hiyo imeendelea kutekeleza kwa mafanikio Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka mitano (2021/22 - 2025/26) kwa kukamilisha miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa madaraja makubwa tisa.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (wapili kulia), akiwa katika picha ya pamoja na aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho ( wa pili kushoto), mara baada ya kukabidhiana ofisi. Kulia ni Katibu Mkuu wa Sekta ya Uchukuzi, Bw.Gabriel Migire na kushoto ni Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi, Mhandisi Joseph Malongo. (Picha na Siti Said-WUU).

Akizungumza leo Septemba 23,2021 wakati wa kumkabidhi ofisi kwa Waziri mpya wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa jijini Dodoma, Dkt. Chamuriho ameyataja madaraja yaliyokamilika kuwa ni daraja la Magufuli (Kilombero), Nyerere (Kigamboni -Dar es Salaam), Magara (Manyara), Kavuu (Katavi), Mlalakuwa (Dar es Salaam), Momba (Rukwa), Lukuledi (Lindi), Mara (Mara) na Sibiti mkoani Singida.

Aidha, Dkt. Chamuriho amesema daraja jipya la Selander, daraja la Msingi (Singida), daraja jipya la Wami, Kitengule, Ruhuhu na Kigongo – Busisi, ujenzi wake unaendelea na uko katika hatua nzuri.

“Kuhusu usafiri wa anga, jumla ya ndege 11 zimenunuliwa na tayari mkataba wa ununuzi wa ndege nyingine mpya tano umeshafanyika,”amesisitiza.

Naye Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amemuomba aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dkt. Leonard Chamuriho kuendelea kushirikiana na wizara hiyo, ili kuwatumikia vyema watanzania.

Aidha, amemuelezea Dkt. Chamuriho kuwa ni kiongozi makini, mwenye utaalamu na ambaye amefanya mambo makubwa nchini kwa weledi ili kuhakikisha Watanzania wanapata miundombinu iliyo bora.

"Siwezi kuandika historia yangu bila kukutumia, tumetatua changamoto nyingi za Wizara hii hususani Sekta ya Uchukuzi tukiwa pamoja, hivyo nakuomba tuendelee kusaidiana kuwatumikia Watanzania," amesisitiza Prof. Mbarawa.

Makabidhiano hayo ya ofisi yanafuatia mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan hivi karibuni.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news