Madaktari kuweni na huruma kwa wagonjwa-Askofu Nyaisonga

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Askofu Gervas Nyaisonga amewataka madaktari nchini kuwa na huruma.

Sambamba na kujiepusha na vitendo vya rushwa wakati wa kuwahudumia wagonjwa wanaofika kupata huduma za afya kwenye maeneo yao mara kwa mara.
Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Askofu Gervas Nyaisonga akizungumza wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 84 wa mwaka wa Chama cha Madaktari wa Kikristo Tanzania (TCMA) uliofanyika leo Septemba 6,2021 jijini Dodoma.Ameyasema hayo leo Septemba 6,2021 jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 84 wa mwaka wa Chama cha Madaktari wa Kikristo Tanzania (TCMA).

“Hapa juzi niliona clip ya video na kuelezwa kuwa kuna daktari kamshona mgonjwa, lakini inadaiwa kuwa baada ya kukosa fedha alimfumua huyo mgonjwa,bahati nzuri sio wa hospitali zetu za dini ya Kikristo,hivyo tuwe na huruma kwanza bila kujali masilahi ya fedha,"amesema.

Baba Askofu huyo amesema, kazi ya kuwahudumia wagonjwa ni ya wito,hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa moyo wa kuthamini maisha ya binadamu na kujituma bila kushawishika au kuwa na tamaa ya kujinufaisha wao.
Rais wa Chama cha Madaktari wa Kikristo Tanzania (TCMA), Dkt.Bwire Chirangi akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa 84 wa mwaka wa maaadaktari hao.

Pia amesema madaktari hao wamepewa dhamana ya kutunza afya za watu, hivyo wanatakiwa kuzingatia maadili ya kazi yao na wajitume katika kuokoa maisha ya watu.

Amewataka kujiepusha na mienendo inayochafua maadili ya udaktari na kuchafua kanisa kwa sababu kazi zao zina kiapo na ndani ya kiapo hicho huishi kusema Mungu anisaidie maana yake ni kazi muhimu sana kila siku.

Askofu Nyaisonga ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuruhusu na kushirikiana na mashirika ya dini zote nchini katika kuanzisha na kutoa huduma za kijamii hususan za afya.

“Nawashukuru madaktari nchini kwa jinsi wanavyofanya kazi katika mazingira magumu hasa tangu ulipoingia ugonjwa wa homa ya corona pamoja na kukabiliwa na tatizo la rasilimali fedha, lakini wamejitoa kuwasaidia wagonjwa,”amesema.
Baadhi ya washiriki wakifuatilia hotuba ya Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Askofu Gervas Nyaisonga,(hayupo pichani).

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Madaktari wa Kikristo Tanzania, Dkt. Bwire Chirangi amesema mkutano huo wa 84 wa mwaka unajumuisha madaktari zaidi ya 300 kutoka vituo,zahanati na hospitali za makanisa yote nchini.

Amesema kuwa, mashirika hayo ya dini yanachangia kwa kiwango kikubwa huduma za afya na ustawi wa jamii na kuna hospitali 105 ambapo kati ya hizo 38 ni teule za halmashauri na 10 zimepewa hadhi ya rufaa ya ngazi ya mkoa nchini.

Wakati huo huo amesema mashirika hayo yanamiliki zahati 720 na vituo vya afya 100 kote nchini na wanaendesha baadhi ya vyuo vya mafunzo ya uuguzi na madaktari pamoja na vyuo vya kufundisha wataalamu wa ngazi mbalimbali nchini.

Post a Comment

0 Comments