Madiwani endeleeni kuheshimiana-DC Mgandilwa

Na Hadija Bagasha, Tanga

Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Hashim Mgandilwa amesisitiza suala la nidhamu kwa madiwani wa Halmashuri ya Jiji la Tanga kwa kuendelea kuheshimiana wao kwa wao,watendaji,viongozi wa Serikali au wa chama ikiwemo wananchi wanaowaongoza kwa sababu wao kwa kiwango kikubwa ndio waajiri.
Mgandiliwa ameyasema hayo wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani kilichoketi ambapo amesema kwamba ameamua kusema hivyo kutokana na kwamba bado kuna changamoto za kinidhamu, hivyo aliwaomba madiwani kwamba vyeo vyao ni vikubwa mno hivyo kukosekana nidhamu hakutaleta picha nzuri.

Hatua ya Mkuu huyo wa wilaya inatokana na kuonekana kwa baadhi ya vitendo vya kutokuheshimiana wakati wa kikao hicho kikiendelea jambo ambalo lilimlazimu kutumia muda wake wakati akizungumza kwenye kikao hicho kutoa kauli hiyo.

“Ndungu zangu waheshimiwa madiwani nisisitize suala la nidhamu kwa madiwani tuendelee kuheshimiana sisi kwa sisi,watendaji,viongozi wa serikali au wa chama pamoja na wananchi tunaowaongoza kwa sababu wao kwa kiwango kikubwa ndio waajiri,”amesema DC Mgandilwa.

“Nimesema hivyo kutokana na kwamba bado kuna changamoto za kinidhamu, hivyo niwaombe waheshimiwa madiwani kwamba vyeo vyenu ni vikubwa mno kukosekana nidhamu hakuleti picha nzuri,”amesema.

Hata hivyo katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa wilaya alisema ameanza kufanya ziara katika kata mbalimbali jijini Tanga ambapo alibaini mambo mawili ambapo la kwanza ni baadhi ya miradi ambayo Jiji wanaitekeleza kwa gharama kubwa sana.

Amesema, hizo fedha wanazozipata ziwe za Serikali Kuu za kwao ni wajibu wao kuhakikisha wanazitumia vizuri ziwe kufanya miradi mikubwa hapo hapo kwenye eneo husika.

“Mheshimiwa Mstahiki Meya kuna sehemu niliwahi kwenda katika ziara hii nilikutana na vyooo vimejengwa kwa milioni 12 na bado havijaisha, Serikali kila tundu moja la choo inatoa fedha milioni 1.1 sisi tumejenga kwa milioni 12 matundu sita na bado hatujamaliza huo ni mfano mmoja, lakini ipo mingi hivyo tunapopita huko na kusema hiki hapana tunamaanisha tunataka fedha zinazokuja zinafanya miradi ikiwezekana zifanye na jambo jingine,”amesema Mkuu huyo wa wilaya.

Mkuu huyo wa wilaya pia amesema yapo baadhi ya maeneo ya shule ambazo alifanya ziara akikuta angalau kuna vyoo vya walimu, lakini wapo wengine wanatumia choo kimoja na wanafunzi na baadhi yao maeneo hakuna kabisa ni changamoto.

“Niwaombe washehimiwa madiwani fedha zinazokuja tuzisimamie ili kama tutafanikiwa kubakiza fedha zitawasaidia ziweze kufanya kazi kwenye kufanya mradi mwengine hata matundu ya vyoo vya walimu na tukifanya hivyo vichwa vyetu kesho na kesho kutwa vitanapanuka na kuweza kufanya miradi mengine,”amesema Mkuu huyo wa wilaya.

Hata hivyo, alilishukuru Baraza la Madiwani kufanya maamuzi ya kuamua kuanza kujenga madarasa sasa akieleza ni hatua nzuri na yenye tija kubwa.

“Nikushukuru Baraza la Madiwani nimepata taarifa kuna zoezi la ujenzi wa madarasa 100 ya awali kwa shule za msingi ni 75 na sekondari 25 mimi ninachotaka kusema hayo madarasa serikali inatoa fedha milioni 20, lakini kuna maeneo wameokoa fedha wamejenga chini ya hapo,”amesema.
Amesema kwamba, wanaweza kujenga madarasa chini ya milioni 20 wana uwezekano wa fedha iliyosalia ikapelekwa kwenye eneo huko kujenga vitu vingine na wasimamie fedha itumike vizuri iweze kujenga kitu kingine.

Hata hivyo, alisema katika pitapita zake kwenye kata amebaini wengi wa wajenzi wa miradi wanatoka mbali iweni ni choo tundu moja au nyingine na wao wakikubaliana kupitia 'force account' mafundi watoke eneo husika kwa sababu ni sehemu ya kutoa ajira kwao na kubakiza fedha kwenye eneo husika na kuwekeza eneo hilo.

Pia amesisitiza kwa sasa zabuni za madarasa zimefunguliwa, hivyo mafundi wahakikishe wanahamasishwa wajitokeze kushiriki kwenye miradi hiyo ambayo ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya elimu.

Awali akizungumza Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga,Abdurhaman Shiloo alimuonba Mkuu wa wilaya aendelee na ziara zake na kukagua miradi yao na kutoa maelekezo kila atakapoona inafaa afanye hivyo.

Amesema, kwa sababu ni wajibu wake ni mwakilishi wa Rais, hivyo ni Jicho la Rais katika fedha za serikali kwa hiyo aendelee kutimiza wajibu wake wao kama baraza hawana hofu wala wasiwasi kwa sababu anasaidia kuliweka baraza hilo lionekane kwamba linafanya kazi kwa ufanisi,uwazi na weledi zaidi.

“Kuna swali liliulizwa Mkuu wa wilaya aliagiza Takukuru ni haki yake yeye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na ana vyombo vyake vinamsaidia kufanya kazi kwa niaba ya Serikali mahali popote anapoona kuna ualakini kwa maslahi mapana ya Serikali,Baraza na wananchi tunakushuru tunamuambia tupo nyumba yako.

"DC suala la nidhamu ukimuona mtu mzima anarudia jambo mara kwa mara kuna kitu sasa ni wajibu wetu kama viongozi tujiulize, kwa nini DC akija anazungumza nidhamu jiongeze mwenyee, jitathimi, jipime na uone kama unaendana na maadili ya uongozi au ukibaini kasoro, jirekebishe,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news