Malezi FC kutoka Butiama yatwaa Kombe la Malkia mkoani Mara

NA FRESHA KINASA

Timu ya kitongoji cha Malezi FC iliyopo Kijiji Cha Kinyariri kata ya Buhemba Wilaya ya Butiama imefanikiwa kunyakua Ubingwa wa kombe la ''Malkia Cup'' baada ya kuichapa timu ya kitongoji cha Bukambiro FC iliyopo ndani ya Kijiji hicho bao 1 - 0 katika mchezo wa fainali uliochezwa Uwanja wa Shule ya Msingi Kinyariri ambapo bao limefungwa dakika ya 87 ya mchezo huo na Rajab Christmas
Picha zikimuonyesha, Lilian Athanas kutoka Shirika la HGWT akimkabidhi kikombe kwa Nahodha wa timu ya Malezi FC, Rajab Christmas. (Picha zote na DIRAMAKINI Blog).
Afisa Mhamasishaji Jamii Madhara ya Ukatili wa Kijinsia Kutoka Shirika la HGWT, Emmanuel Goodluck akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi kwa timu ya Malezi FC. (Picha zote na DIRAMAKINI Blog).
Timu ya Bukambiro FC wakiwa wamekaa chini kabla ya kupokea zawadi sh. 100,000 kwa kuwa washindi wa pili.
Wachezaji wa timu ya Malezi FC wakiwa wamekaa chini wakisubiria kukabidhiwa kikombe na zawadi.
Lilian Athanas kutoka Shirika la HGWT katikati,kushoto kwake Mwenyekiti wa Kijiji cha Kinyariri l,Winfrida Wangwe na kulia kwake, Emmanuel Goodluck kutoka HGWT wakifuatilia mchezo wa fainali.
Mashabiki wa timu ya Malezi FC wakicheza kufurahia ushindi.
Kufuatilia ushindi huo, timu ya Malezi FC imeweza kukabidhiwa kikombe chenye thamani ya Shilingi 300,000 pamoja na fedha Shilingi 200,000. Huku Mshindi wa pili timu ya Bukambiro FC ikipokea Shilingi 100,000 na mshindi wa tatu Kinyariri FC ikipata Shilingi 50,000 na timu yenye nidhamu bora Kurusanzati FC ikijipatia Shilingi 30,000.

Mchezo huo wa fainali umechezwa Septemba 17, 2021 uwanjani hapo, na kushuhudiwa na umati mkubwa wa mashabiti kutoka sehemu mbalimbali za kata ya Buhemba pamoja na viongozi wa Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania ambao ndio walioandaa mashindano hayo chini ya Mkurugenzi wake,Rhobi Samwelly.

Ambapo mashindano yalianza kutimua vumbi kuanzia Agosti 31, 2021 katika uwanja wa Shule ya Msingi Kinyariri yakishirikisha vitongoji vitano vya kijiji cha Kinyariri ikiwemo kitongoji cha Malezi, Kinyariri chini, Bukambiro Kurusanzati na Kusaya ambapo kila timu ilipewa jezi na mpira na Shirika hilo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi kwa washindi wa mashindano hayo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Shirika hilo, Rhobi Samwelly, Lilian Athanas kutoka Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania amesema,   yalilenga kuwahamasisha vijana kuwa mabalozi wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia, kupinga vitendo vya kihalifu pamoja na kuwajenga kiafya na kiakili katika shughuli zao za maendeleo.

Ameongeza kuwa, vitendo vya kikatili kwa watoto wa kike ikiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni vimekuwa vikiwanyima fursa ya kufikia malengo yao na hivyo Kupitia mashindano hayo, elimu ya madhara ya vitendo hivyo imewafikia vijana na wananchi kwa ujumla na hivyo wanajukumu la kushiriki kuunga mkono jitihada za serikali na wadau wote katika mapambano dhidi ya Ukatili. Huku akiwataka vijana pia kutojihusisha na vitendo vya kihalifu na uvunjifu wa amani katika maeneo yao.

Afisa Uhamasishaji Jamii madhara ya Ukatili wa Kijisia kutoka Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT),Emmanuel Goodluck amesema, shirika litaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya Ukatili kwa njia mbalimbali ikiwemo michezo kwa vijana, ngoma za asili mikutano ya hadhara lengo ni kuwafanya Watoto wa kike wathaminiwe na wapewe fursa ya kusoma ili waje kutoa mchango wa maendeo yao kwa Jamii na taifa kwa siku za usoni.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji Cha Kinyariri, Winfrida Wangwe, amesema kuwa mashindano hayo yameweza kuwa chachu kubwa kwa vijana na wananchi kuwaamsha katika kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, ambapo amewataka kuzidi kuwa mabalozi wa kutoa elimu hiyo kwa wengine na kuwafichua wale watakaobainika kufanya vitendo vya kikatili kwani wanarudisha nyuma juhudi za Serikali za kutokomeza Ukatili. Huku akisisitiza vijana kudumisha amani na wajitume kufanya kazi halali kwa manufaa yao na taifa pia.

Nahodha wa timu ya Malezi FC, Rajab Christmas amepongeza Shirika la HGWT kwa namna ambavyo limeweza kuwakutanisha vijana na wananchi Kupitia mashindano hayo, ambapo amesema Kupitia mashindano hayo elimu imewafikia wote na hivyo kila mmoja anawajibu wa kuifanyia kazi. Huku akiomba Serikali izidi kuchukua hatua kali kwa wanaobainika kukwamishwa malengo ya watoto wa kike ikiwemo kukatisha masomo yao na kuwaozesha kwa lengo la kupata mali.

Mwajuma Paul ni mkazi wa Kitongoji Cha Kinyariri ambapo amesema, Watoto wa kike wanamchango mkubwa wa Maendeleo kwa Jamii na taifa ambapo ametolea mfano Rais Samia Suluhu Hassan kufikia hatua aliyonayo ya Urais wazazi wake walimsomesha kwa juhudi zote na kwa sasa ni Rais ambaye anawatumikia Watanzania kuwaletea maendeleo akaomba wazazi na Wananchi wote kushiriki kuwaondolea vikwazo wafikie mafanikio, badala ya kuwakwamisha kwa tamaa ya mali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news