Msaki:Polepole kama hauwezi kutulia turudishie kadi ya CCM

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Mjumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Lindi na Mkutano Mkuu Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa,Peter Ibrahim Msaki amemtaka Mbunge wa Kuteuliwa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Humphrey Polepole kutulia na kama hawezi basi arudishe kadi ya chama.
“Ndugu Humphrey Polepole kama huwezi kutulia Chama Cha Mapinduzi (CCM) bila cheo turudishie kadi yetu,Shule ya Uongozi unayotoa haina mantiki wala tija na sio muumini wa unayozungumza bali unasakatonge bila kujali matokeo ya maneno yako,”ameeleza Msaki.

Ndugu Msaki anayasema hayo ikiwa Mheshimiwa Polepole kupitia darasa hilo la Shule ya Uongozi ambalo alilianzisha hivi karibuni kupitia runinga mtandao kuonekana kuwa, linakwenda kinyume na maadili na taratibu za Chama Cha Mapinduzi (CCM) hususani kutokana na kauli zake ambazo zinatafsriwa kuwa na utata.

Polepole kupitia darasa hilo ambalo lilianza na utangulizi alieleza awali kuwa, dhamira ni kuwapa maarifa Watanzania ili kuufahamu kwa kina uongozi.

"Uongozi ni uwezo wa kushawishi wengine,uwezo wa kuwa na maono, ukiwa na mamlaka au bila mamlaka. Uongozi una nafasi mbili, uongozi katika nafasi ya wewe kama wewe, lakini wewe kama wewe una uwezo wa kuwashawishi wengine bila kushurutisha. Na uongozi katika nafasi ya madaraka;

Polepole kabla ya kuteuliwa na Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Novemba 29, 2020 kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikuwa ndiye Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

"Inashangaza sana, ndugu yetu Humphrey Polepole ameendelea kusema mambo ambayo yeye mwenyewe si muumini wake, lakini, kila mmoja ana uhuru wa kuzungumza, sioni haja wala umuhimu wa yeye kutufundisha Darasa la Uongozi kwa sasa, kwa nini hakutufundisha hayo wakati ule Magufuli alikuwa madarakani? Polepole aache kutupumbaza, afanye mambo yake ya kibunge, yakimshinda ajiuzulu akafundishe huko vyuoni, mbona mwenzake walioteuliwa pamoja Riziki (Bi.Riziki Said Lulinda) yupo kimya?

"Imefika mahali tuweze kuwakemea wazi wazi wanasiasa ambao huwa wanataka kutumia kila namna kujionyesha wapo vizuri mbele ya umma, lakini kivitendo hakuna,"ameeleza mmoja wa wafuasi waliozungumza na DIRAMAKINI Blog mkoani Dar es Salaam.
 
Haya yanajiri ikiwa hivi karibuni, video fupi ambayo ilitokana na darasa hilo, Humphrey Polepole alionekana kutoa elimu yenye kutafakarisha zaidi.

Post a Comment

0 Comments