Mwenyekiti ALAT Tanga atoa rai kwa halmashauri

Na Hadija Bagasha, Tanga

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (ALAT) Mkoa Tanga, Sadick Kalaghe amezitaka halmashauri mkoani humo kuhakikisha zinakuwa na nidhamu na matumizi sahihi ya fedha za umma ikiwa ni pamoja na usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo ili iweze kuleta tija kwa maslahi ya wananchi.
Aidha,amewataka wakurugenzi na wenyeviti wa halmashauri kuepuka misuguano isiyokuwa na lazima na badala yake amewasisitiza kuhakikisha wanakuwa na mahusiano mazuri ili kulinda uhai wa hamalshauri zao na hatimaye waweze kuzungumza lugha moja itakayoweza kuwaletea wananchi maendeleo.

Lakini pia amezitaka halmashauri mkoani humo kuhakikisha zinakusanya vizuri mapato ya ndani kwa kuzingatia nidhamu na maadili ya kazi zao.

Mwenyekiti Kalaghe ameyasema hayo wakati wa kikao cha kwanza cha ALAT Mkoa Tanga kilichoketi katika halmashauri ya jiji la Tanga kabla ya kuelekea katika mkutano mkuu wa ALAT Taifa unaotarajiwa kufanyika Septemba 27 hadi 29, mwaka huu mjini Dodoma.

Akifungua kikao hicho cha ALAT Mkoa Tanga, Mwenyekiti Kalaghe amesema yeye kama mwenyekiti ajenda yake muhimu ni ukusanyaji wa fedha za umma, hivyo amesisitiza kuwepo na nidhamu na katika matumizi ya fedha za umma ili ziweze kurudi kwa wananchi katika kuwaletea miradi mbalimbali ya maendeleo.

"Mimi kama mwenyekiti agenda yangu ya muhimu ni fedha mnapaswa kutambua Alat ni chombo muhimu sana ni daraja la kuvuka katika serikali kuu mpaka serikali za mitaa lazima kuwepo na mabadiliko katika halmashauri zetu maisha yamepanda hivi sasa oneni umuhimu wa chombo hiki cha Alat kwa kuwa kinasaidia kusemea watu na kuboresha mambo mengi, "amesisitiza Mwenyekiti Kalaghe.

Sambamba na hayo Mwenyekiti Kalaghe amesisitiza watendaji wa halamashauri Mkoani humo kuhakikisha wanaambia na ukweli juu ya athari ya kupokea rushwa huku akiwataka kuheshimiana na kupendana.

"Tufike mahali tuambiane ukweli rushwa ni adui wa haki tuzingatie maadili yetu ya kazi, huu ni mkutano wetu wa kwanza tokea tumechaguliwa hivyo ni lazima tutengeneze dira tuweze kuifanya Alat yetu ya Mkoa Tanga inoge na kuwa na maslahi kwa jamii, "amesisitiza Mwenyekiti Kalaghe.

Katika kikao hicho paliibuka hoja ya kugawa mkoa wa Tanga kutokana na kuwepo kwa Halmashauri 11 katika mkoa wa Tanga ambao unaufanya mkoa huo kuwa mkubwa.

"Tuutazame mkoa wa Tanga na ukubwa wake,na hata Halmashauri zote za nchi nzima mkoa wa Tanga ndio una Halmashauri nyingi zaidi kuliko mkoa wowote,una Halmashauri 11,lakini mkoa una watu laki sita tu na imepewa hadhi ya kuwa mkoa,ambayo ni sawa na wilaya ya Lushoto hizo ni craiteria kwanini mpate mkoa na tuna watu zaidi ya milioni mbili,"alisema Kalaghe.

Aidha, ameongeza kuwa tuna haja ya kuunga hoja ya RCC na Chama Cha Mapinduzi ya kuiomba Serikali Kuu kuikubaliana nao kugawa mkoa wa Tanga iwe na mikoa miwili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news