RC wa Geita achangia damu, chupa 288 zapatikana

Na Robert Kalokola, Geita

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule ameongoza wananchi kujitokeza kuchangia damu katika kampeni inayoendeshwa na Chama cha Waandishi wa Habari Mji wa Geita (GMG) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita katika Maonesho ya Uwekezaji na Teknolojia ya Madini mjini Geita.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule akichangia damu katika banda la damu salama kwenye maonesho ya uwekezaji na teknolojia ya madini mjini Geita. (Picha na Robert Kalokola).
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule akiwa na mhudumu wa afya akimpima mapigo ya moyo (presha) kabla ya kuchangia damu. (Picha na Robert Kalokola).

Mkuu wa mkoa wa Geita mara baada ya kuchangia damu amesema kuwa, kampeni hiyo imekuwa na mafanikio makubwa kwani hadi Septemba 25 ,2021 chupa 288 za damu zilikuwa zimepatikana.

Rosemary Senyamule amefafanua kuwa ,chupa hizo zikitumika kwa mgonjwa kuongezewa chupa moja tu, maisha ya watu 288 watakuwa yameokolewa kupitia kampeni hiyo iliyofanyika kwa siku 10 katika viwanja vya maonesho hayo.

Senyamule amesema kuwa, yeye mwenyewe ameamua kutoa damu kwenye banda hilo huku akiungwa mkono na wananchi mbalimbali ambao baada ya kusikia wito wake walihamasika na kuamua kusaidia ili kuokoa maisha ya wananchi ambao wana mahitaji ya kuongezewa damu.
Mkuu wa mkoa wa Geita,Rosemary Senyamule akimkabidhi fedha laki tatu, Makamu Mwenyekiti wa GMG ambayo imetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Geita kwa ajili ya kununua mahitaji ya watu wanaochangia damu. (Picha na Robert Kalokola).
Mkuu wa mkoa wa Geita Rosemary Senyamule akipima uzito kabla ya kuchangia damu.(Picha na Robert Kalokola).

"Niwashukuru wote ambao wameshiriki kwa namna tofauti kuja kutoa damu zao niendelee kuwashukuru wote kuja kuendelea kutoa damu, nataka miseme wazi kwamba ndani ya siku ya 10 tangu maonesho ya madini yalipoanza tumepata chupa 288 mpaka sasa,"amesema Senyamule.

Ameongeza kuwa, Afya ni Jambo la msingi kwa kila mtu na kwamba anatamani wananchi wa mkoa wa Geita wawe na afya njema muda wote pamoja na watanzania.

"Natamani kuwa na wananchi wenye afya njema na nimeona sio jambo sahihi kuwahamasisha wengine halafu mwenyewe nisitoe damu na ndio maana nipo hapa leo na nimeshatoa damu,nawashukuru wote walioniunga mkono na ninamshukuru Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita Constantine Morandi kwa mchango wake laki tatu alionipatia ili kufanikisha jambo hili kwa ajili ya kununulia mahitaji mbalimbali yanayotumiwa na watu wanaochangia damu,"amefafanua Mkuu wa Mkoa.
Mkuu wa mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule akiwa na mtaalam wa damu salama akimjazia dodoso kabla ya kuchangia damu. (Picha na Robert Kalokola).
Mmoja wa wananchi waliongozana na Mkuu wa Geita wa Geita, Rosemary kumuunga mkono kuchangia damu kwa hiari. (Picha na Robert Kalokola).

Makamu Mwenyekiti wa GMG, Mutta Robert amesema kuwa wazo la kuanzisha zoezi hilo lilianza baada ya waandishi kuona taarifa za wanawake wanaojifungua kuwa mahitaji makubwa ya damu, watoto wadogo,na wanaopata ajali.

"Mara nyingi waandishi wa habari tumekuwa tukiandika habari za wananchi tena wengine wakiwa na matatizo mbalimbali ikiwemo kuishiwa damu sasa tukaona tusiishie kuripoti tu nasi tuwe sehemu ya msaada kwa kuchangia na kuhamasisha wengine kutoa damu,"amesema Mutta Robert, Makamu Mwenyekiti wa GMG.

Zoezi la kuchangisha damu kwa hiari limeandaliwa na GMG kwa kushirikiana na mganga mkuu wa mkoa wa Geita kwa kutoa wataalam wa damu salama na kuungwa mkono na wadau mbalimbali wa mkoa wa Geita.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule akizungumza na Afisa Raslimali watu wa Mgodi wa Buckreef Gold Company, Amelda Msuya aliyejitokeza kumuunga mkono baada ya kumaliza kuchangia damu. (Picha na Robert Kalokola).

Magdalena Gumbu kutoka Hospitali ya mkoa wa Geita kitengo cha damu salama amesema kuwa, lita 288 zimeisha kusanywa katika kipindi hiki chote.

Amesema, mahitaji ya hospitali hiyo ni makubwa hivyo zoezi hilo ni muhimu kwa ajili ya kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji kuongezewa damu.

Zoezi hilo lilianza rasmi Septemba 10, mwaka huu na litahitimishwa leo siku ya kufunga maonyesho hayo.

Post a Comment

0 Comments