Wahitimu shule za msingi na sekondari watadharishwa kuhusu 'watoto wa ibilisi'

Na Hadija Bagasha, Tanga

Wanaohitimu elimu ya msingi na kidato cha nne jijini Tanga wametakiwa kuepuka kujiunga na kikundi cha kihalifu cha watoto wa ibilisi ambao wana umri kati ya miaka 12 mpaka 18 kwani Serikali imejipanga kukomesha kikundi hicho ambacho kimekuwa kikiwapora watu mali zao pamoja na kuwajeruhi kwa kutumia silaha za mapanga, bisibisi, visu na hata nyundo.
Ushauri huo umetolewa na mwakilishi wa mkuu wa wilaya ya Tanga  Leonard Paul Sembe ambaye ni afisa tarafa Ngamiani Kaskazini wakati alipokuwa mgeni rasmi katika mahafali ya darasa la saba na kidato cha nne katika Shule ya Eckenford jijini Tanga.

Mwakilishi huyo wa mkuu wa wilaya amesema kuwa, Serikali imejipanga kukomesha vitendo hivyo,kwani kumeibuka wimbi la watoto wenye umri mdogo kujihusisha na vitendo vya kihalifu jambo ambalo limekuwa likiwatia hofu wakazi wa jiji la Tanga.

"Niseme tu wazi kwamba hatutavumilia watoto wanaohitimu na kujiingiza katika vigenge vya kihalifu, kubwa tu niwashauri mjiepushe na makundi yatakayoweza kuwakatishia ndoto zenu, nendeni mkawe vijana wa kuwaelimisha wenzenu,"amesistiza.

Ameongeza kuwa, mnapokwenda kule mtaani mtakutana na vijana wenzenu wanaitwa watoto wa ibilisi ni imani yetu kwa malezi mazuri mliyoyapata hapa nyinyi hamtokwenda kuwa sehemu yao, lakini pia niwaambieni wale watakaokwenda kujiingiza kule kwa kujiona wamemaliza shule sasa wanakwenda kuwa wahalifu nafasi hiyo haipo.

Awali akizungumzia shule hiyo mwakilishi huyo wa mkuu wa wilaya aliiomba taasisi hiyo kuendelea kuwaelimisha vijana wao juu ya athari zinazochangiwa na utandawazi na badala yake wametakiwa kuwaelimisha wafahamu uzalendo wa nchi yao.

"Waelimisheni na muwaandae vizuri ili baada ya kumaliza elimu yao ekawe tayari kwenda kujitegemea badala ya kutoka hapo wakiwa tegemezi vijana hawa wamweandaliwa vizuri na wanajua kutumia teknolojia kwa ajili ya kupambana na maisha, "amesema Sembe.

Amewaasa wazazi kutumia taasisi hiyo kuwapeleka watoto wao kwa ajili ya kujiunga na taasisi hiyo kwani imekuwa na mazao chanya kwa wale wote waliopita katika taasisi hiyo na hivi sasa wanafanya kazi ya kulitumikia taifa katika maeneo mbalimbali ikiwemo serikalini.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Eckernford, Daniel Tarimo akizungumza wakati wa Sherehe za Mahafali ya darasa la saba na kidato cha nne yaliyofanyika kwa pamoja kwenye Viwanja vya Taasisi hiyo jijini Tanga. (Picha na Hadija Bagasha Tanga).

Kwa upande Mkurugenzi wa Taasisi ya Eckenford, Daniel Tarimo amesema kuwa pamoja na malengo mahususi ya kuwawezesha wanafunzi kubobea kitaaluma katika karne hii ya sayansi na teknolojia taasisi hiyo imekuwa ikiwaleta na kuwakuza, wanafunzi kikamilifu kiroho, kiakili na kimwili.

"Madhumuni ya yote haya tusingeweza kuyatimiza bila ushirikiano, mshikamano na msaada uliopo kati ya shule na wazazi hivyo taasisi itazidi kuhakikisha inatoa wanafunzi wenye sifa na weledi na watakaoweza kulitumikia taifa mahali popote, "amesisitiza Tarimo.
Naye Mkuu wa Shule ya Eckernford English Medium Primary School,  Geldart Msonde amesema kuwa, wamewaanda vyema wanafunzi wao wa msingi na sekondari kufanya vizuri katika mitihani yao wanayotarajia kufanya hivi karibuni na hatimaye kupata matokeo mazuri.

"Nitumie fursa hii kuwaomba wazazi na jamii watuamini kama walivyoeleza kutumiani kipindi chote kuwa tunaweza na hivyo waje waandikishe watoto wao katika taasisi yetu, "amebainisha Msonde.

Wanafunzi 43 wa darasa la saba katika shule ya Eckenford wanatarijiwa kufanya mtihani wao wa taifa Septemba 8 na 9,mwaka huu huku wanafunzi 17 wakitarajiwa nao kufanya mtihani wao wa taifa mwezi Novemba.

Post a Comment

0 Comments