Wakulima:Mfumo wa Stakabadhi Ghalani unalipa, Serikali isonge mbele

NA MWANDISHI MAALUM

Wakulima wa Mkoa wa Ruvuma wameiomba Serikali kuendelea kusimamia na kuimarisha Mfumo wa Stakabadhi Ghalani kwa sababu umeleta mafanikio makubwa kwa wakulima, Serikali, Vyama vya Msingi na Ushirika na wadau wengine wa mfumo huo.
Mbunge wa Jimbo la Mlalo Mhe. Rashid Abdallah Shangazi,akizungumza na wakulima wa Mkoa wa Ruvuma wakati wa ziara ya Kamati Maalum ya Bunge inayofuatilia na kujengewa uelewa juu ya Mfumo wa Stakabadhi Ghalani.

Wakulima wameeleza hayo mbele ya Kamati Maalum ya Bunge inayofuatilia na kujengewa uelewa juu ya Mfumo wa Stakabadhi Ghalani inayoongozwa na Mhe. Rashid Abdallah Shangazi Mbunge wa Jimbo la Mlalo iliyoambatana na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe kufanya ziara katika Wilaya za Mbinga, Songea, Namtumbo na Tunduru Mkoani Ruvuma ili kujua mwenendo wa mfumo huo kwa mazao ya Ufuta, Soya, Mbaazi, korosho, kahawa na mazao mengine.

Akiongea katika kikao kilichowakutanisha Wakulima na Kamati Maalum ya Bunge Bw. Ally Hassan Chemka, Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha SONAMCU ameeleza kuwa Mfumo wa Stakabadhi ghalani umewasaidia kuwakutanisha wakulima na wanunuzi na kuwafanya wawe na maamuzi na kuuza mazao yao kwa umoja na kwa bei nzuri, vilevile umesaidia ukusanyaji wa mapato, kabla ya mfumo huo Halmashauri ilikuwa inakusanya mapato kwa shida kwa kuweka jamba na vizuizi barabarani.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe,akizungumza na wakulima wa Mkoa wa Ruvuma wakati wa ziara ya Kamati Maalum ya Bunge inayofuatilia na kujengewa uelewa juu ya Mfumo wa Stakabadhi Ghalani.

“Kabla ya mfumo huu Wakulima walikuwa hawana uwezo wa kulalamikia bei kwa pamoja, lakini mfumo umetuisaidia kuunganisha nguvu sisi wanyonge na kuweza kuwakabili watu waliokuwa wanachukua mazao kwa bei ya chini ili wakauze bei ya juu, kwa hiyo sisi kama wana Ruvuma tunasema mfumo huu sio wa kuelimishana tena bali imeshakuwa falsafa ya biashara ya mazao ya nafaka hivyo mtu akisema mfumo haufai mwananchi wa Ruvuma hawezi kukuelewa,” amaeeleza Bw. Ally Hassan Chemka.

Nae, Bw. Ally Ibango, Mwenyekiti wa Chama cha Msingi Rwinda amebainisha kuwa Mfumo wa Stakabadhi ghalani unatoa ajira nyingi na unawasaidia vijana na akina mama pale mazao yanawekwa ghalani kuna kazi zinapatikana kama kubeba kufungasha mizigo pia ameiomba Serikali kusimamia changamoto ya wanunuzi kuchelewa kufanya malipo kwa siku saba mpaka kumi na nne.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe,akiwa katika picha ya pamoja na Kamati Maalum ya Bunge inayofuatilia na kujengewa uelewa juu ya Mfumo wa Stakabadhi Ghalani mara baada ya kutoa elimu kwa wakulima wa Mkoa wa Ruvuma.

Nao Wakulima wengine tofauti wameeleza mafanikio waliyoyapata kutokana na mfumo wa Stakabadhi ghalani ambayo ni kuwepo kwa matumizi halali ya vipimo kwa kutumia mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo, Kuongezeka kwa bei na uzalishaji wa mazao ya Ufuta, Soya na Mbaazi.

Wakati huo huo, Wakulima wamebainisha baadhi ya changamoto ambazo wameomba Serikali izifanyie kazi ambazo ni wafanyabiashara wanaotumia wanasiasa ili kuchochea Serikali kuzuia mfumo usifanye kazi, kuwepo kwa miundombinu isiyo rafiki hasa barabara katika baadhi ya maeneo .

Kwa Upande wake, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe ameeleza kuwa kazi kubwa ya Serikali kupitia maoni yaliyotolewa ni kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya kufanya biashara kwa kuwaka Sera, Mipango na Mikakati, Kanuni na Sheria zinazotekelezeka bila kuwa kikwazo kwa wadau kwa maana ya wakulima, wafanyabiasha na wenye viwanda.

“Niwahakikishie wananchi wote wa Ruvuma kuwa tutaendelea kutatua changamoto ambazo zinajitokeza ndio maana tukafika kuwasikiliza na kujifunza kwenu, na nimeshawaelekeza Bodi ya Sitakabadhi Ghalani kutoka maofisini ili waje kuwaelimisha wakulima faida ya mfumo huu badala ya kusubiria wakuliwa waanze kulalamika” ameeleza Mhe. Exaud Kigahe

Awali, Mwenyekiti wa Kamati Maalumu ya Bunge, Mhe. Rashid Abdallah Shangazi Mbunge wa Jimbo la Mlalo amesema kuwa ziara yao bado inaendelea kwa mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi na wamekuja kujifunza kupitia wakulima na kuona Mfumo wa Sitakabadhi Ghalani unavyofanya kazi

“Tumekuja kujifunza na mafuzo tuliyoyapata ni halisi kwa sababu tumekuja kwa wahusika moja kwa moja na naamini Mfumo wa Sitakabadhi Ghalani ndio soko huria kwasababu unatoa uwazi kwa kushindana kwenye zabuni pia mfumo huu umesaidi AMCOS kujitoa kusaidia katika shughuli mbalimbali za kijamii, mfano tumeona AMCOS moja ya Kimuli imetoa Zaidi ya shilingi milioni 170 kwenye shughuli za kijamii”

Vilevile, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge wakati akiikaribisha kamati hiyo Maalumu ya Bunge alibainisha kuwa Mkoa wa Ruvuma una ziada kubwa ya chakula, lakini ili kuendeleza uhimilivu wa chakula ni lazima wajikite kwenye mazao ya kimkakati ya kibiashara wanayoweza kuyalima kama kilimo cha mahindi na vyakula vingine na dawa pekee ya kusaidia hayo sio kuboresha sitakabadhi ya ghala bali ni kuboresha mnyororo mzima kuanzia kwenye mbegu hadi kwenye mavuno.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news