Waziri Biteko atoa maagizo kwa Maafisa Madini Mikoa

Na Tito Mselem-WM

Waziri wa Madini, Doto Biteko, amewataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa yote ya kimadini nchini kuimarisha mahusiano baina yao na viongozi wengine wa Serikali waliopo katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na wakuu wa mikoa, wilaya, watendaji wa kata na viongozi wa vijiji wanakohudumia.
Waziri wa Madini Doto Biteko akizungumza jambo katika ufunguzi wa mkutano wa Maafisa Madini Wakazi Wakazi wa Mikoa uliofanyika Septemba 10, 2021 jijini Dodoma.

Amesema wao ndio sura ya wizara katika mikoa na wilaya wanazozisimamia na kuwataka kuweka historia nzuri kwenye maeneo yao. “Likitokea jambo baya lolote sote tunachafuka hivyo tuwe makini katika kujenga taswira njema ya sekta yetu” Biteko amesisitiza.

Amesema hayo alipokuwa akifungua Mkutano wa robo ya kwanza ya Mwaka wa Fedha 2021/2022 ambao upo katika almanac ya Tume ya Madini ya Mwaka 2021/2022 wenye lengo la kujadili juu ya uboreshaji wa mikakati mbalimbali ya namna ya kufikia na hata kulivuka lengo la kukusanya Shilingi 650,000,000,000 walilopangiwa na Serikali kwa mwaka huu wa fedha.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Yahya Samamba (kulia) akufuatilia Mkutano wa Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa uliofanyika Septemba 10, 2021 jijini Dodoma (kushoto) Kamishna wa Tume ya Madini Prof. Abdulkarim Mruma.

“Suala hili ni jema, na Wizara ya Madini inawaunga mkono na kama ilivyo ada itaendelea kuunga mkono juhudi hizi ambazo zina tija kwa Sekta ya Madini katika kuhakikisha Sekta inafikia mchango wa asilimia 10 kwenye Pato la Taifa ifikapo 2025,” ameongeza Biteko.

Amesema, kiu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ni kuifanya Sekta ya Madini inaendelea kuwa kinara kwa ukuaji wa uchumi wa nchi na kubainisha kikao hicho ni muhimu kwani kimewahusisha wataalamu wanaosimamia kwa ukaribu zoezi la ukusanyaji wa maduhuli ya serikali.

Aidha, Waziri Biteko amewataka watendaji hao kutumia mkutano huo kubadilishana uzoefu wa kiutendaji kutokana na mazingira tofauti tofauti waliyotoka, pia kuchangia kwa uhuru na uwazi ili kutoa nafasi kwa viongozi kuona namna bora ya kushirikiana nao katika kutatua changamoto watakazoziibua.
Waziri wa Madini Doto Biteko (katikati), Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya (kulia), Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula wakiwa na baadhi ya viongizi wa Wizara na Tume ya Madini baada ya ufunguzi wa mkutano wa Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa uliofanyika Septemba 10, 2021 jijini Dodoma.

“Wizara imepewa lengo la kukusanya Shilingi bilioni 650,000,000,000 ni kubwa lakini msivunjike moyo kaendeleeni kufanya kazi ili kuifanya Sekta ya Madini iendelee kuwa kinara katika kuchagiza ukuaji wa uchumi wa nchi,” amesema Waziri Biteko.

Pamoja na hayo Waziri Biteko, amewapongeza Maafisa hao kwa namna wanavyofanya kazi katika maeneo yao na kueleza kunapokuwa na hoja inayomlazimu kupata ufafanuzi kutoka kwao asilimia 90 ya Maafisa hao wanakuwa wanaufahamu wa suala husika na wamelifanyia kazi.

Aidha, amewataka Maafisa hao kusimamia haki na kujitenga na mambo ya kuchukua rushwa kutoka kwa wachimbaji kwani litawaharibia sifa kama viongozi walioaminiwa.
Waziri wa Madini Doto Biteko (kulia) akiteta jambo na Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya Septemba 10, 2021 jijini Dodoma.

“Toa ushauri wako kwa viongozi wako wa Mkoa na Serikali ili kupeana mawazo namna ya kutatua changamoto mnazokutana nazo, "isifike mahali ukaona Sekta ya Madini ni yako, kuna viongozi wengine huko shirikiana nao,” amesisitiza Biteko.

Akieleza suala la leseni zinazotajwa kufuta, Waziri Biteko amewataka kufuta leseni mara baada ya kujiridhisha kuwa kweli leseni inasifa ya kufutwa na sio kwa kufuata majungu ya watu na kutaka haki itendeke.

Pia, Waziri Biteko ameelekeza kuwa maeneo yote yenye mfumuko wa Madini (rush) ambayo kuna uwezekano wa kutoa leseni, leseni zitolewe kwa mujibu wa Sheria ili kurahisisha usimamizi.
Baadhi ya Washiriki walioshiriki Mkutano wa Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa uliofanyika Septemba 10, 2021 jijini Dodoma wakiwa kwenye sala ya pamoja.

“Wasaidieni watanzania kufurahia uwepo wa Sekta ya Madini, wahudumie kwa upendo na endeleeni kufanya kazi kwa haki, kwa uaminifu na kila mmoja atende haki", alisisitiza Waziri Biteko.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha waziri Biteko, Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya amewapongeza Maafisa hao kwa kazi kubwa wanayoifanya ukilinganisha na ukubwa wa eneo wanalolisimamia na idadi ya watumishi walionao.

Amewataka kuifanyia kazi imani waliyopewa na Serikali kwa kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kikamilifu na kuifanya sifa njema ya Tume ya Madini tangu kuanzishwa kwake inaendelea kuwepo. “Kupitia nyie Wizara ya Madini inaendelea kutengeneza jina jema na tuendelee hivyo” alimaliza Prof. Manya.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Prof. Idris Kikula amewataka maafisa hao kuimarisha utendaji kazi wa taasisi na kuwa na mtazamo wa pamoja wa namna ya kuhakikisha wanashirikiana kuimarisha utendaji wao.

Amesema suala la kuhakikisha maduhuli ya serikali yanakusanywa si suala la mzaha na kuhimiza wasimamie kikamilifu suala hilo. “Kama hatuwezi kufikisha malengo hatufai kila mmoja atumie nguvu katika kuhakikisha anafikia malengo aliyowekewa na ikiwezekana kuvuka lengo ulilowekewa,”amesema.
Waziri wa Madini Doto Biteko (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya menejimenti ya Wizara na Tume ya Madini pamoja na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa uliofanyika Septemba 10, 2021 jijini Dodoma.

Mkutano hui wa siku moja umefanyika katika ukumbi wa Mruma uliopo katika jengo la Taasisi ya Jiolojia na Utafiti Tanzania (GST).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news