Wizara ya Madini, NHC zasaini Mkataba ujenzi wa ofisi Dodoma

Asteria Muhozya na Steven Nyamiti-Dodoma

Wizara ya Madini imesaini Mkataba wa Shilingi Bilioni 22.02 na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wa kuanza ujenzi wa Ofisi za Wizara katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Hafla ya kusaini Mkataba wa ujenzi huo imefanyika katika Ofisi za Wizara ya Madini Mtumba jijini Dodoma Septemba 7, 2021 ambapo pia, Wizara imekabidhi rasmi eneo la ujenzi kwa Mkandarasi NHC baada ya kushinda zabuni.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila (Kulia) na Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Dkt. Maulid Banyani (Kushoto) wakisaini Mkataba wa kuanza kwa ujenzi wa Ofisi za Wizara katika Mji wa Serikali Mtumba, Septemba 7, 2021 jijini Dodoma.

Aidha, katika hatua nyingine, wizara imesaini Mkataba na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa ajili kuwa msimamizi wa ujenzi wa jengo hilo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Msanjila ameipongeza NHC kwa kushinda kandarasi hiyo na kutaka ujenzi uwe wa haraka kwa kuzingatia ubora, viwango na kasi kama ilivyo kwa sura ya Madini.

“Ni matumaini yangu kwamba NHC wana uzoefu mkubwa, siku za karibuni wamekamilisha miradi mikubwa ya Kitaifa, hospitali ya rufaa ya Kanda ya Kusini, lakini pia hospitali ya Kanda ya Mara na majengo mengine mengi,” amesema Prof. Msanjila.
Mkurugenzi wa Ushauri wa TBA Wenzelaus Kizaba, akizungumza baada ya kusaini Mkataba wa kuanza kwa ujenzi wa Ofisi za Wizara katika Mji wa Serikali Mtumba, Septemba 7, 2021 jijini Dodoma.

Aidha, Prof. Msanjila amesema, msimamizi wa ujenzi huo ambaye ni (Consultant) Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ndiye aliyesanifu ramani inayokwenda kutumika kujenga jengo la Wizara ya Madini.

“Kitu walichokisanifu watakuwa na mazingira mazuri ya kukisimamia wao wenyewe na hatutegemei changamoto za nenda rudi, na kwa sababu ni taasisi zote za Serikali na zimefanya kazi kwa pamoja katika miradi mingi, ninaamini wanauelewa mkubwa wa karibu na utekelezaji wa maradi huu utakuwa kwa ufanisi sana,” ameongeza Prof. Msanjila.

Naye, Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Dkt. Maulid Banyani amemueleza Prof. Msanjila kuwa, NHC watatekeleza mradi huo kwa ustadi mkubwa kwa kuhakikisha dhamira wizara inayo kwao katika muda ambao mradi unatakiwa kukamilika.
Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Dkt. Maulid Banyani, akisaini Mkataba wa kuanza kwa ujenzi wa Ofisi za Wizara katika Mji wa Serikali Mtumba, Septemba 7, 2021 jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila, akisaini Mkataba wa kuanza kwa ujenzi wa Ofisi za Wizara katika Mji wa Serikali Mtumba, Septemba 7, 2021 jijini Dodoma.

“Tutajitahidi kuwa ndani ya muda kwa asilimia 100, ombi langu kwa wenzetu TBA twende haraka kwa pamoja ili tufike kama kauli mbiu ya Rais inavyosema. Kwa hiyo tujitahidi kwenda haraka kwa pamoja ili tufike kwa haraka kule ambapo tunataka kwenda,” ameongeza Dkt. Banyani.

Aidha, Dkt. Banyani amehaidi kutekeleza mradi huo kwa kasi na ameishukuru Serikali kwa kutoa kiasi kikubwa cha fedha zitakazowezesha kutekelezwa kwa mradi na akiishukuru wizara kwa kuiamini NHC.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ushauri wa TBA Wenzelaus Kizaba, ameshukuru Wizara ya Madini kwa kuwapatia nafasi ya kuweza kuwa wabunifu na wasanifu wa jengo la wizara. Amesema Serikali iliwapatia kusanifu majengo yote ya Mji wa Serikali kwa Wizara zote 24 pamoja na taasisi mbili.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila na Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Dkt. Maulid Banyani na wataalam wengine wakiangalia eneo la ujenzi wa jengo la Ofisi za Wizara katika Mji wa Serikali Mtumba, Septemba 7, 2021 jijini Dodoma.

“Sisi na NHC tumefanya kazi nyingi, wamekuwa wakandarasi sisi tumekuwa wasimamizi, na kuna sehemu nyingine sisi tumekuwa wakandarasi na wenyewe wasimamizi kwa hiyo tunajuana. Kwa mantiki hiyo tutashirikiana kwa pamoja, na kuhakikisha kwamba hili jengo linajengwa kwa viwango vilivyokusudiwa na hakutakuwa na ucheleweshwaji wa aina yoyote kwa sababu vitu vyote vimezingatiwa ndani ya ubunifu na usanifu wa jengo la wizara,” ameeleza Kizaba.

Katika makubaliano hayo yaliyosainiwa leo, Wizara ya Madini imeonyesha eneo la ujenzi litakalojengwa jengo la Wizara ya Madini na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Madini, NHC, TBA ili kuanza rasmi kwa ujenzi.

Kukamilika kwa ujenzi wa jengo hilo, kutapelekea Idara na Vitengo vyote vya wizara kuhamia katika jengo hilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news